|
Wauaji wa Azam leo mjini Tabora, Gaudence Mwaikimba na Seif Abdallah |
USHINDI wa mabao 3-0 iliyopata jioni ya leo dhidi ya Prisons ya Mbeya, imeifanya JKT Ruvu inayonolewa na kocha Mbwana Makatta kukalia kiti cha uongozi wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiziacha Yanga, Simba, Azam na Mtibwa zikiwa nyuma yao katika msimamo wa ligi hiyo.
Maafande hao walipata ushindi huo wa pili mfululizo ikiwa ndiyo timu pekee iliyoweza kuvuna pointi sita na bila kuruhusu lango lao kuguswa mpaka sasa ligi ikiwa raundi ya pili kaika uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Mabao ya Salum Machaku 'Balotelli', Emmanuel Switta na Abdallah Bunu yalitosha kuwaweka Ruvu kileleni baada ya kuiengua Yanga waliolazimishwa sare ya 1-1 na Coastal Union kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Yanga iliyoinyoa Ashanti United mabao 5-1 katika mechi ya kwanza ilianza kupata bao kupitia kwa Mrundi Didier Kavumbagu kabla ya Coastal kuchomoa dakika ya 90 kwa mkwaju wa penati iliyofungwa na Jerry Santo, huku timu zote zikipoteza mchezaji mmoja Simon Msuva wa Yanga na Crispian Odullah.
Katika mechi nyingine za leo za ligi hiyo, Simba ikiwa ugenini uwanja wa Sheikh Amri Abeid ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wao JKT Oljoro kwa bao lililofungwa na Haruna Chanongo, huku Gaudence Mwaikimba na Seif Abdallah waliifungia Azam mabao yaliyoipa ushindi dhidi ya Rhino Rangers mjini Tabora.
Wageni wa ligi hiyo, Mbeya City walipata ushindi usiotarajiwa nyumbani mjini Mbeya dhidi ya Ruvu Shooting waliokubali kichapo cha mabao 2-1 kwenye uwanja wa Sokoine.
Bao la jioni la Steven Mazanda lilitosha kuizamisha Ruvu ambayo mechi iliyopita waliishindilia Prisons kwa mabao 3-0 wakiwa kwao Mlandizi, Pwani.
Nao Mgambo JKT ya Tanga iliilaza Ashanti United kwa bao 1-0, huku Mtibwa Sugar ikiwa nyumbani kwao Manungu, iliwazaba 'ndugu' zao Kagera Sugar kwa bao 1-0.
Matokeo ya mechi za leo ni kama ifuatavyo:
JKT Oljoro vs Simba (0-1)
Yanga vs Coastal Union (1-1)
Mbeya City vs Ruvu Shooting (2-1)
JKT Ruvu vs Prisons (3-0)
Mtibwa Sugar vs Kagera Sugar (1-0)
Rhino Rangers vs Azam (0-2)
Mgambo JkT vs Ashanti United (1-0)