* Chelsea kujiuliza upya kwa Atletico JumatanoMABINGWA watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Bayern Munich ya Ujerumani kesho itakuwa na kibarua cha kuamua kusuka au kunyoa, watakapoikaribisha Real Madrid katika mechi ya mkondo wa pili wa Nusu Fainali ya michuano hiyo kabla ya Chelsea na Atletico Madrid wakijiuliza siku ya Jumatano.
Watetezi hao walicharazwa bao 1-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyochezwa wiki iliyopita nchini Hispania ambao mabingwa wa kihistoria, Real Madrid walikosa mabao mengi ya wazi na kuwapa presha kubwa Bavarians.Bayern italazimika kubadilisha matokeo hayo mbele ya vijana wa Carlo Ancelotti ambao wana kiu ya kutaka kunyakua taji la michuano hiyo baada ya kulikosa kwa miaka 12 na pia wakitaka kufikia idadi ya kulibeba mara 10.
Hofu ya Bavarians watakaokuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Allianz Arena ni kurejea tena kwa Cristiano Ronaldo ambaye katika mechi ya kwanza aliicheza akiwa na maumivu kabla ya kutolewa kipindi cha pili kumpisha Gareth Bale aliyekuwa akisumbuliwa na mafua.
Hata hivyo Bayern chini ya Pep Guardiola haitabali kufanywa daraja na wapinzani wao kuelekea kwenye fainali zitakazofanyika nchini Ureno katikati ya mwezi ujao.
Ikiwategemea nyota wake kama Franck Ribery, Arjen Robben, Mario Gotze, Mario Mandzukic, Dante, Thomas Muller na kiungo matata Bastian Schweinsteiger ina uhakika na kuivusha tena timu hiyo katika mchezo wa fainali kama ilivyokuwa mwaka uliopita ilipoenda kukumbana na Borussia Dortmund na kubeba taji hilo baada ya kulikosa mikononi mwa Chelsea mwaka 2012.
Kivumbi kingine cha nusu fainali kitakuwa siku ya Jumatano mjini London wakati Chelsea itakapokuwa uwanja wa Stanford Bridge kuikaribisha vinara wa La Liga, Atletico Madrid ambao wiki iliyopita wakiwasimamisha na kwenda nao suluhu ya kutofungana mjini Madrid.
Chelsea iliyofufua tumaini la kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya England baada ya jana kuizabua Liverpool wanaoongoza msimamo watashuka Stanford Bridge ikiwakosa baadhi ya wachezaji wake nyota akiwamo kipa Petr Cech na nahodha John Terry walioumia katika pambano la awali.
Hata hivyo mbinu za kocha Jose Mourinho katika kukabiliana na wapinzani wake inawapa matumaini mashabiki wa Chelsea kuamini kuwa wanaweza kuwasimamisha vijana wa Diego Simeone ambayo msimu huu imekuwa moto wa kuotea mbali.
The Blues watakuwa na kazi ya kuwachunga nyota wa Atletico, Diego Costa, Diego, Koke, Thiago, David Villa, Gabi na Raul Garcia ambao wameifanya timu yao msimu huu kuzima ubabe wa Real Madrid na Barcelona nchini Hispania.
Mashabiki wana hamu kubwa ya kutaka kujua ni timu zipi mbili zitakazofuzu hatua fainali na kushuhudia moja wapo ikitawazwa kuwa bingwa mpya mjini Lisbon Ureno mnamo Mei 24.
Je Bayern itakubali kuvuliwa taji na Real Madrid au Chelsea itatepeta nyumbani dhidi ya Atletcio Madrid? Tusubiri tuone.