|
Ruvu Shooting |
|
Simba |
KOCHA Mkuu wa Ruvu Shooting, Mkenya Tom Olaba ametamba kuwa wataishukia Simba kesho kwenye uwanja wa Taifa kwa mbinu zilizotumiwa na 'kaka' zao baada ya kurekebisha makosa yaliyowapelekea kufumuliwa mabao 7-0 na Yanga wiki iliyopita.
Vijana wa Olaba walikumbana na kipigo hicho kwenye uwanja wa Taifa Jumamosi iliyopita siku chache baada ya 'ndugu' zao JKT Ruvu kufumuliwa mabao 6-0 na Prisons Mbeya, lakini wenzao JKT waliwaangukia Simba siku inayofuata (Jumapili) kwa kuilaza mabao 3-2.
Akizungumza na MICHARAZO, Olaba alisema kama JKT Ruvu waliweza kujiuliza baada ya kipigo cha jijini Mbeya ndivyo nao walivyojiuliza na kurekebisha makosa na kwamba kwa sasa kikosi chake kipo tayari kuchochea zaidi 'machafuko' ndani ya Simba.
Oloba alisema vijana wake wapo fiti kwa mchezo huo licha ya kuwakosa Ibrahim Susan na George Osei ambao wanasumbuliwa na majeraha na watalikosa pambano hilo.
'"Nashukuru vIjana wangu wapo vyema na tumefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha tunapata ushindi dhidi ya Simba Jumapili, kipigo cha Yanga hakijatukatisha tamaa, badala yake tumerekebisha makosa kama zinavyofanya timu nyingine ambazo kwenye duru la pili zimepoteza kama sisi na kupata mafanikio katika mechi zao zilizofuata," alisema Olaba.
Olaba alisema pamoja na kujiamini kuibuka na ushindi mbele ya Simba, lakini watashuka dimba la Taifa kwa tahadhari kubwa kesho ili wasitoe nafasi kwa wapinzani wao ambao klabu yao kwa sasa siyo shwari tangu walipopata matokeo mabaya katika mechi zao nne zilizopita ili kumalizia hasira zao kwao.
"Tunaijua Simba ni timu nzuri na inayotafuta mahali pa kumalizia hasira zao, hivyo tutacheza kwa tahadhari ilimradi tuhakikishe tunapata ushindi utakaoturudisha kwenye nafasi za juu kama ilivyokuwa kabla ya kufungwa na Yanga," alisema Mkenya huyo.
Simba inayonolewa na kocha Mcroatia, Zdrakov Lugarusic, itashuka dimbani Jumapili ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 3-2 toka kwa JKT Ruvu ikiwa ni kipigo chao cha tatu msimu huu, huku ikiwa imepoteza pointi 10 kati ya 12 ya michezo minne iliyochezwa hivi karibuni.
Timu hiyo ilianza kwa kuambulia sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar kabla ya kulala 1-0 kwa Mgambo JKT na baadaye kwenda Mbeyana kupata sre ya 1-1 mbele ya wenyeji wao Mbeya City na kukumbana na kipigo hicho kilichoibua maneno toka kwa wadau wa klabu hiyo shutuma zikienda kwa uongozi wa Ismail Aden Rage kwamba ameshindwa kufanya kazi kwa kuitelekeza timu.
Hata hivyo uongozi wa Simba kupitia Katibu Mkuu wake, Ezekiel Kamwaga na manahodha Said Masoud 'Chollo' na Amri Kiemba wamewahakikisha wanasimba kwamba watarekebisha makosa na kuanza kuwapa raha kuanzia mechi hiyo ya kesho dhidi ya Ruvu.