STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, January 8, 2017

SIMBA NA YANGA HAKUNA JINSI TENA

Simba wakishangilia katika mechi zao za hivi karibuni









Picha zikionyesha kabla ya pambanio la Simba na Jang'ombe Boys lililochezwa jioni ya leo kwenye Uwanja wa Amaan.
USIYEMPENDA kaja. Simba imepata ushindi wa mabao 2-0 na kuifuata Yanga kwenye pambano la nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi katika mechi itakayopigwa usiku wa Jumanne.
Mabao mawili ya kila kipindi kutoka kwa Laudit Mavugo yametosha kuzikutanisha timu hiyo ambazo zina upinzani wa jadi katika soka la Tanzania.
Mavugo alifunga bao la kuongoza dakika ya 11 kabla ya kuongeza jingine tamu katika kipindi cha pili dakika ya 54 na kuifanya Simba kubaki kileleni mwa msimamo wa Kundi A ikiwa na pointi 10, pointi ambazo haziwezi kufikiwa na klabu yoyote nyingine iliyopo kwenye kundi hilo.
Watetezi URA ya Uganda usiku itavaana na Taifa Jang'ombe ili kuunga na Simba katika nusu fainali ambapo itakayofuzu itavaana na vinara wa Kundi B, Azam iliyoikandika usiku wa jana Yanga kwa mabao 4-0.
Katika pambano hilo lililoisha hivi punde, Simba iliwazidi ujanja wapinzani wao, licha ya Boys kujitutumua kutaka kuizuia Simba isisonge mbele.
Simba na Yanga zinakutana kwenye pambano la Kombe la Mapinduzi kwa mara ya kwanza tangu walipovaana kwenye fainali ya mwaka 2011 ambapo Yanga ilikandamizwa mabao 2-0.

Lakini hilo litakuwa pambano la nne la watani hao wa jadi kukutana visiwani Zanzibar tangu mwaka 1975 walipokutana kwa mara ya kwanza kwenye Kombe la Kagame na Yanga kushinda na kuvaana tena 1992 na Simba kushinda kwa penalti.
Washindi wa mechi za nusu fainali hizo mbili zitakazochezwa Jumanne zitavaana Ijumaa ijayo kwenye pambano la fainali ya michuano hiyo ya 11 tangu mfumo wa sasa uanze kutumika mwaka 2007 na Yanga kuwa bingwa wa awali.
Simba ndio timu iliyotwaa taji la michuano hiyo mara nyingi, ikifanya hivyo mara tatu na kufuatiwa na Azam iliyobeba mara mbili, huku Yanga, Mtibwa Sugar, Miembeni, KCCA na URA zote za Uganda zikitwaa mara moja moja.

West Bromwich Albion yamkomalia straika wa Napoli

KLABU ya West Brom ipo kwenye mazungumzo ya kutaka kumnyakua straika wa Napoli, Manolo Gabbiadini.
Kwa mujibu wa duru za kimichezo nchini Uingereza zinasema kuwa Albion inazungumza na klabu ya Napioli inayoshiriki Ligi Kuu ya Italia, Serie A ili kumsajili Gabbiadini.
Straika huyo mwenye miaka 25 pia ananyatiwa na klabu za Wolfsburg, Southampton, huku Everton na Stoke City nazi zikitajwa kwenye mbio hizo.
Wolfsburg walikaribia kumnasa Gabbiadini kwa mkono kwa kiasi cha Puni 15 milioni usajili uliopita na Albioni walijaribu kumnasa Agosti mwaka uliopita na sasa inakula sahani moja kumnasa jumla kwenye usajili huu wa Januari.
Gabbiadini aliifungia timu yake bao dhidi ya Sampdoria na kuisaidia kutoka nyuma na kushinda mabao 2-1.

Mavugo atupia jingine kuipeleka Simba nusu fainali

MRUNDI Laudit Mavugo ameendelea kuwafunga mdomo waliokuwa wakimponda baada ya kutupia tena bao la pili dakika ya 54 na kuifanya timu yake ya Simba kuwa mbele kwa mabao 2-0 dhidi ya  Jang'ombe Boys.
Kama matokeo yatabaki kama yalivyo kwa Simba kushinda mchezo huo haitakuwa na kingine ila kuvaana na Yanga walioshika nafasi ya pili katika kundi B la michuano ya Kombe la Mapinduzi 2017.

Kibarua cha Bilic West Ham shakani

KAZI anayo. Kibarua cha Meneja wa West Ham United, Slaven Bilic kipo hatarini, ikielezwa ana mechi mbili tu kabla ya kufutwa kazi.
Kwa mujibu wa The Sun, limefichua kuwa kibarua cha Bilic kipo kwenye hatihati kama atashindwa kufanya vema kwenye mechi zijazo za timu hiyo.
Mechi hizo zinahusisha pambano dhidi ya Crystal Palace na Middlesbrough hii ikiwa ni baada ya kupokea kichapo cha aibu cha mabao 5-0 juzi Ijumaa kutoka kwa Manchester City katika pambano la Kombe la FA.
Ushindi wa mechi tatu katika mwezi uliopita, West Ham ilijikwamua toka janga la kushuka daraja, lakini bado imekuwa na muelekeo mbaya kitu kinachowatisha mabosi wa klabu hiyo.

Simba v Jang'ombe Boys sasa ni mapumziko

PAMBANO la Simba na Jang'ombe Boys kwa sasa ni mapumziko kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, huku Wekundu hao wa Msimbazi wakiwa mbele kwa bao 1-0.
Bao lililofungwa na Laudit Mavugo na kuifanya Simba iwe kwenye nafasi kubwa ya kuvaana na Yanga katika mechi ya nusu fainali kama matokeo yatabaki yalivyo, kwani Mnyama atamaliza nafasi ya kwanza na pointi 10.

Mavugo atupia kambani baada ya miezi miwili

SEMENI tena! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya straika wa Simba, Laudit Mavugo kufunga bao lake la kwanza tangu alipofanya hivyo mara ya mwisho Oktoba mwaka jana katika mechi ya Ligi Kuu Bara.
Mavugo amefunga bao hilo dakika 11 ya pambano lao la Kundi A ya michuano ya Kombe la Mapinduzi unaoendelea kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar dhidi ya Jang'ombe Boys kuwania tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano hiyo.
Kwa sasa pambano linakaribia kwenda mapumziko na Simba inaongoza bao 1-0. MICHARAZO itakuwa inakuletea dondoo kadri mechi inavyoendelea visiwani humo.

Obi Mikel kasepa zake Uchina kiroho safi

HABARI ndio hiyo bwana! Nyota wa Chelsea John Obi Mikel ametangaza kupitia posti kwenye mitandao ya Kijamii kuwa anaihama klabu hiyo na kujiunga na klabu ya Ligi Kuu ya China, Tianjin TEDA.
Mnigeria huyo mwenye miaka 29, alijiunga na Chelsea akiwa na kinda la miaka 19 akitokea klabu ya Lyn  ya Norway mwaka 2006 na kucheza Mechi 374.
Katika msimu huu wa Ligi Kuu ya England, chini ya Kocha Antonio Conte, Mikel hajacheza hata mechi moja na inaelezwa hiyo ni sababu ya kuchukua maamuzi ya kwenda China ambayo imekuwa ikimwaga fedha lukuki kwa mastaa ili kushawishi kutua kwenye ligi yao.
Akiwa na Chelsea, Mikel alitwaa mataji 11 yakiwemo mawili ya Ligi Kuu England na moja la L:igi ya Mabingwa Ulaya.
Akiaga, Mikel alitoa shukran kwa Mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich pamoja na mashabiki wa Klabu hiyo, huku bilionea huyo akimtakia kila la heri.

Yanga yakumbana na dhahama mbele ya Azam

Sure Boy aliyekuwa mpishi katika maangamizi ya Yanga jana mjini Zanzibar
Na Rahma White, Z'Bar
BADO hawaamini. Yanga na kikosi chake bora. Ikiwa na Kocha Mzambia George Lwandamina usiku wa jana wamepigwa mabao 4-0 na Azam katika mechi ya kufungia dimba ya Kundi B kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2017.
Sio makocha tu, bali hata mashabiki wa klabu hiyo mpaka sasa hawaamini kile kilichowakuta kwa sababu waliamini Azam walikuwa wepesi kwao.
Hata hivyo kwa kuwa soka ni mchezo wenye matokeo ya kikatili, Yanga imelala bao 4-0 na kuweka rekodi ya kupokea kipigo kikubwa tangu mwaka 2012 walipotunguliwa na watani zao wa Simba katika mechi ya Ligi Kuu 2011-2012.
Katika pambano hilo Yanga ilikandikwa mabao 5-0, lakini Azam jana usiku ilisamehe moja na kufunga mabao hayo ikiwa ni mengi kuwahi kuifunga timu kongwe nchini Simba na Yanga na kumaliza kama kinara wa kundi lao.
Mabao ya John Bocco 'Adebayor' lililokuwa la 14 kwake kuitungua Yanga, na mengine ya Waghana Yahya Mohammed na Enoch Agyei-Atta na lile la Joseph Mahundi yalityosha kuinyoosha Yanga iliyocheza ovyo eneo lake la ulinzi.
Mabadiliko ya kutolewa kwa Haji Mwinyi na kuingizwa Geofrey Mwashiuya yaliigharimu Yanga ambayo sasa inasubiri kujua itaumana na Simba au klabu gani katika mechi ya nusu fainali Jumanne ijayo.
Simba itakabiliana na Jang'ombe Boys katika mechi ya kukamilisha ratiba, huku URA na Taifa Jang'ombe zikipapetuana kusaka tiketi za kucheza nusu fainali. Mechi hizo zinapigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Amaan.
Baadhi ya wachezaji wa Yanga wamesema hawajui mpaka sasa kilichoikuta timu yao kwani walijiandaa kuvaana na Azam, ingawa wamekiri kucheza mfululizo bila mapumziko ni tatizo la kupoteza umakini usiku wa jana.