STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, March 7, 2013

Barcelona yawatamani Vermaelen, Daniel Agger


VINARA wa Ligi Kuu ya Hispania, Barcelona imetajwa kuwa katika mbio za kuwanasa nyota wa Ligi Kuu ya England, beki wa kati wa Arsenal Thomas Vermaelen na Daniel Agger wa Liverpool kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake kilichoanza kupwaya.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na the Sun, zinasema kuwa Barca wanamsaka Vermaelen na Agger kwa ajili ya kuziba nafasi ya nahodha wao Carles Puyol ns Eric Abidal ambao umri umeanza kuwatupa mkono ili kuimarisha kikosi chao kushambulia kuanzia nyuma.

Hatua ya Barca kuwafukuzia wakali hao wa EPL imetokana na kukatishwa tamaa na dau kubwa linalotaka mabingwa wa Ujerumani ili kuachia 'kitasa' wao Mats Hummels.

Kwa siku za karibu Barcelona wameonyesha kupoteza ule umahiri wake ambako hivi karibuni katika siku nne walijikuta wakinyanyaswa na wapinzani wao Real Madrid kwa kufungwa jumla ya mabao 5-2 katika mechi mbili.

Walianza kwa kunyukwa mabao 3-1 katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mfalme kabla ya kulala tena 2-1 katika Ligi Kuu.

Klabu hiyo iliwahi kuingia kwenye mbio za kumwania Agger, 28 kabla ya Manchester City kuingia kati na kusitisha mipango yake na inadhani Vermaelen kwa staili ya uchezaji wake itawasaidia na inamkadiria nyota huyo anaweza kuwa na thamani ya Pauni Milioni 15 na watajaribu kuishawishi Arsenal kuwaachia beki huyo.

Msimbazi kumekucha 'vibopa' wajiuzulu

Zakaria Hanspope (mwenye kofia) na Kaburu (kati) waliotangaza kuachia ngazi Simba leo mchana

HALI ndani ya klabu ya Simba si shwari baada ya vibopa wawili muhimu ndani ya timu Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ambaye pia ni Mjumbe wa kamati ya utendaji, Zakaria Hanspope na Makamu Mwenyekiti, Godfrey Nyange 'Kaburu' kubwanga manyanga kwa sababu mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini mchana wa leo zinasema kuwa Hanspop amebwaga manyanga kwa kuuandikia barua uongozi wa juu ukitaka kukaa kando kwa kushindwa kutimiza malengo waliyojiweka kutokana na kuwepo kwa mgawanyiko ndani ya uongozi uliopo sasa.
Tayari barua hiyo imeshatua mikononi mwa viongozi wa klabu hiyom unasubiriwa kuridhia maamuzi hayo au la, ikizngatiwa kuwa Hanspop kwa sasa ndiyo kila kitu katika Simba.
Na hivi punde taarifa zimedokeza kuwa Kaburu, ambaye naye ni mmoja wa mhimili wa Msimbazi ameomba kuachia ngazi ikiwa ni katika mtindo ule ule wa kukerwa na hali ya mambo iliyopo ndani ya Simba.
Micharazo imedokeza kuwa, vibopa hao ni mwanzo tu wa kuparaganyika kwa viongozi wa Simba kutokana na kuelezwa kuwa wajumbe kadhaa wa Simba wapo njiani kuwafuata kama njia ya kuonyesha hali si shwari Msimbazi.
Kujiuzulu kwa viongozi hao kunaweza kuwa mwiba kwa Mwenyekiti Ismail Aden Rage ambaye wiki iliyopita alivumishiwa kutaka kuachia ngazi baada ya Simba kulala kwa Mtibwa Sugar katikma mechi ya ligi kuu kabla ya kuibuka na kukanusha taarifa hizo akidai hajiuzulu ng'o kwa vile siyo anayecheza uwanjani.
Simba imekuwa ikifanya vibaya tangu mwishoni mwa duru la kwanza na katika mechi za duru la pili huku wakiwa wameshaaga michuano ya kiimataifa ilipokuwa ikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kunyukwa jumla ya mabao 5-0 na Recreativo do libolo ya Angola.


Micharazo inaendelea kuwasaka viongozi wa juu ya Simba kupata undani ya hali ilivyo kadhalika kuwajulisha kinachoendelea, ingawa kinachoonekana Msimbazi sasa ni kuelekea kwenye hali tete huku wakikabiliwa na mechi ngumu siku ya Jumapili dhidi ya Coastal Union na mechi nyingine saba kabla ya kumaliza msimu wa 2012-2013 kukiwa na dalili ya kuutema ubingwa wa ligi hiyo.

Golden Bush Veterani yampa shavu Mzee wa Kiminyio, kuivaa Baker Rangers


Kikosi cha Golden Bush Veterani katika picha ya pamoja

WAKALI wa soka la wazee jijini Dar e Salaam, Golden Bush Veterani imefanya mabadiliko katika benchi lake la ufundi ikijiandaa na pambano siku ya Jumamosi dhidi ya Baker Rangers.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa timu hiyo ambaye pia ni mlezi wa klabu hiyo, Onesmo Waziri 'Ticotico' uteuzi huo umefanywa wakijiandaa na mechi za sikukuu ya Pasaka.
Taarifa hiyo ya Ticotico imemtaja nyota wa zamani wa Majimaji, Simba na Taifa Stars, Madaraka Selemen kuwa ndiye kocha mkuu na msaidizi wake ni Herry Morris nyota za zamani wa Yanga.
"Tungependa kuwataarifu kwamba lie timu inayoogopwa sana hapa Dar es salaam imeanza Maandalizi rasmi kabisa ya game ya kumaliza ubishi Siku ya Pasaka na vibonde wetu Wahenga."taarifa ya Ticotico inasomeka hivyo kabla ya kuendelea; 
"Ili kujiweka sawa kabisa, timu yetu imefanya mabadiliko kidogo katika bench la ufundi ambapo kuanzia sasa Kocha Mkuu atakuwa Madaraka Seleman na Msaidizi wake ni Herry Morris ambaye atakuwa kocha mchezaji".
Taarifa hiyo iliongeza kwa kusema kuwa, Nahodha wa timu hiyo anasalia kuwa Yahya Issa akisaidiwa na Wazir Mahadhi na Nico Nyagawa.
Ticotico alidokeza kuwa timu hiyo imeanza mazoezi kabambe kabisa katika fukwe ya bahari na siku ya Jumamosi itashuka dimbani kuumana na Baker Rangers kabla ya timu kuingia kambini.

Juventus, PSG nazo zapenya robo fainali Ulaya



KIkosi cha Juve kilichopenya robo fainali Ligi ya Ulaya
  
MABINGWA wa Italia Juventus jana walifanikiwa kuingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuilaza Celtic mabao 2-0 na kufuzu kwa jumla ya mabao 5-0, huku PSG ya Ufaransa nayo ikipenya hatua hiyo kwa sare ya 1-1.
Juventus iliyokuwa uwanja wake wa nyumbani mjini Turin, ilipata mabao yake katika kila kipindi bao la kwanza likifungwa dakika ya 24 na Alessandro Matri na kufanya hadi mapumziko matokeo yawe 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana, lakini ni Juventus walioendelea kutamba kwa kujipatia bao la pili lilitumbukizwa kimiani na Fabio Quagiarella.
Katika mechi nyingine iliyochezwa jana usiku, PSG ilifanikiwa kuungana na timu za Real Madrid, Borrusia Dotmund na Juventus hatua ya robo fainali baada ya kulazimishwa sare kwenye uwanja wake wa nyumbani na Valencia ya Hispania.
Hadi mapumziko timu hizo mbili zilikuwa nguvu sawa kwa kutofungana licha ya kushambiuliana na kufaya kosa kosa kadhaa.
Kipindi cha pili kilianza kwa Jonas wa Valencia kuipatia wageni bao la kuungoza katika dakika ya 55 na kuwafanya wenyeji kucharuka wakisaka bao.
Juhudi zao zilikuja kufanilkiwa katika dakika ya 66 kupitia nyota wake, Ezequiel Lavezzi na kuifanya timu hiyo iliyomchezesha nyota wa zamani wa England, David Beckham kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya mechi ya awali kumalizika kwa PSG kushinda mabao 2-1 ugenini.