Ruvu Shooting |
RPC wa Morogoro-Leonard Paul |
Msemaji wa Ruvu Masau Bwire |
Kikosi cha Polisi Morogoro |
Msemaji wa Ruvu, Masau Bwire ametamba kuwa kipigo walichowapa Ndanda Fc wakiwa nyumbani kwao Mtwara ndicho ambacho wataipa Polisi katika mchezo wao wa kesho akidai kuwa wapo kamili kuendeleza wimbi la ushindi wakiwa nyumbani baada ya kufanya vibaya katika mechi zao tatu za awali.
Bwire alisema wameona ni vema amtahadharishe mapema RPC Leonard kwa kumtaka awe mvumilivu wakati vijana wake watakapokuwa wakiadhibiwa na Ruvu kwani vijana wa Oloba wamesharekebisha makosa yaliyowafanya washindwe kupata ushindi katika mechi tatu za awali kabla ya kuzinduka kwa kuicharaza Ndanda mabao 3-1.
"Kwa kifupi pambano la kesho tumeshalimaliza na akili zetu zipo kwa mechi ijayo dhidi ya Coastal Union, ila tungependa kumtahadharisha RPC wa Morogoro, Kamanda Leonard Paul awe mpole na mvumilivu wakati vijana wake wakiadhibiwa na Ruvu, asije akaudhika kama walivyoudhika watu wa Mtwara wakati tukiwanyuka Ndanda mabao 3-1," alisema Bwire.
Msemaji huyo alisema kikosi chao chote kipo kamili bila ya kuwa na majeruhi hata mmoja, kitu ambacho kocha wao ameahidi ni nafasi nzuri ya kuendeleza maangamizi kwa wapinzani kabla ya kuwafuata Coastal Union nyumbani kwao Mkwakwani Tanga.
Ruvu waliomaliza nafasi ya sita msimu uliopita wakilingana pointi na timu za Simba na Kagera Sugar waliokuwa juu yao, ina pointi nne mpaka sasa baada ya mechi nne ikishinda mchezo mmoja, kutoka sare moja na kufungwa mbili na inabanana na timu za JKT Ruvu, Simba na Prisons zote zikiwa na pointi nne na zikifuata kwenye msimamo wa Ligi inayoongozwa na Azam na Mtibwa zenye pointi 10. kila mmoja.