|
Deo Lyatto, alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF |
HAPO chini ni Maelezo ya Shurani ya Mwenyekiti Aliyemaliza muda wake wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Deo Lyatto kwa wadau wa soka nchini.
1. Kama
wote tunavyofahamu jana uongozi wangu wa Kamati ya Uchaguzi ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ulifikia tamati kama
mlivyotangaziwa na Rais wa TFF. Kwa heshima kubwa naomba kutumia fursa
hii kuwashukuru viongozi na wadau wa soka kwa ushirikiano mkubwa
nilioupata kutoka kwao wakati nikitekeleza majukumu mbalimbali ya TFF.
2. Kwa
kushirikiana na viongozi wa mpira wa miguu katika TFF na mikoa yote
Tanzania Bara, pamoja na wadau wa soka, nimepata fursa kulitumikia soka
la nchi yetu kwa nafasi mbalimbali. Kwa pamoja tumetekeleza majukumu ya
ujenzi wa misingi ya uongozi bora katika TFF na wanachama wake.
3. Naishukuru Kamati ya Utendaji ya TFF:
(i)kwa
kuniteua kuwa mjumbe wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, (Jan 2005 - Jan
2007). Nawashukuru pia wajumbe wa Kamati hiyo chini ya Mhe. Said
El-Maamry kwa kunichagua kuwa Katibu wa Kamati hiyo. Ushirikiano
mlionipatia ulioniwezesha kulitumikia taifa katika soka na kwa pamoja
kurejesha nidhamu kwa kiwango kikubwa.
(ii)kwa
kuniteua kuwa mjumbe wa Kamati Maalumu, iliyochunguza mkasa wa timu
yetu ya Taifa ya wachezaji wa umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys)
mwezi Juni 2005. Nawashukuru wajumbe wa kamati hiyo
chini ya Dr. Hamad Ndee Mkuu wa Idara ya Michezo ya Chuo kikuu cha Dar
es salaam, kwa kunichagua kuwa Katibu wa kamati hiyo iliyoandaa taratibu
za mashindano ya vijana ambazo ni msingi wa mashindano ya vijana wa umri chini ya miaka 17 hapa nchini.
(iii)kwa
kuniteua kuwa Mjumbe wa Kamati Maalumu iliyotayarisha Programu ya
kuendeleza Timu ya Taifa kwa kipindi cha miezi 15 (April 2006 hadi Juni
2007). Progamu iliyochangia Tanzania kiinua kiwango cha ubora wa soka
kutoka nafasi ya 165 duniani mwezi Februari 2006 hadi nafasi ya 89 mwezi
Desemba 2007.
(iv)kwa
kunipa fursa ya kuwa mjumbe wa Kamati Maalumu ya kuboresha mapato ya
TFF mwaka 2009. Nikiwa mjumbe na Katibu wa Kamati hiyo nilipata
ushurikiano mkubwa kutoka kwa wadau wa soka nchini na nje ya nchi. Nina
imani kuwa TFF itakamilisha utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati na ya
wadau wa soka ikiwa ni pamoja na kuanza kutumia tiketi za elektroniki.
(v)kwa kuniteua kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa vipindi
viwili; Februari 2009 - Machi 2011 na kuniteua tena kuiongoza Kamati
hiyo kwa kipindi cha pili Machi 2011 hadi jana tarehe 18 Julai 2013.
Naishukuru Kamati ya Utendaji ya TFF kwa imani kubwa iliyoonyesha kwangu
na wanakamati wenzangu.
4. Nawashukuru
wajumbe wote wa wa Mkutano Mkuu wa TFF, kwa ushirikiano mkubwa mliotoa
kwangu na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kushiriki kwa amani na utulivu
na kuzingatia Katiba za vyama vyenu, Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi
na hivyo kufanikisha zoezi la chaguzi za viongozi katika wilaya zote na
Mikoa yote ya Tanzania Bara na hivyo kuwezesha kuwa na wajumbe wa
Mkutano Mkuu, ambao katika kikao chake cha kwanza baada ya chaguzi hizo kimefanya jambo la kihistoria kuweka nguzo za Mwenendo, Maadili na Miiko ya uongozi wa soka la nchi yetu. Nilifarijika kuwa sehemu ya Mkutano Mkuu huo nikiwa mwalikwa.
5. Nawashukuru
viongozi na wafanyakazi wote wa Sekretarieti ya TFF, wajumbe wa Kamati
zote za TFF, Wajumbe wa Kamati zote za Uchaguzi za wanachama wa TFF na
wanachama wao, kwa ushirikiano mkubwa na wa dhati uliowezesha
kuwatumikia wadau wa soka kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
6. Nawashukuru
sana wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa ushirikiano niliopata
kutoka kwao kwa muda tuliofanya kazi pamoja. Si jambo rahisi kusimamia
chaguzi za mikoa yote na klabu zenye wanachama za Ligi Kuu, hata hivyo
kwa kushirikiana na wadau mbalimali wa soka ambao nachukua fursa hii
kuwashukuru, kwa pamoja tumeweza kutimiza jukumu hilo kikamilifu.
7. Nawashukuru
sana Waandishi na Wahariri wa habari za michezo na pia Wahariri
Watendaji wa vyombo vya habari, kwa ushirikiano mzuri nanyi, ushirikiano
na uhusiano wa uwazi ambao haukuwa na mikwaruzo ya aina yoyote kwa
kipindi chote (Jan 2005-Jul 2013) tulichoshirikiana kwa pamoja
kulitumikia soka la nchi yetu.
8. Namshukuru sana Rais wa TFF Ndg. Leodegar Tenga
kwa imani kubwa aliyonayo kwangu na kwa wanakamati niliokuwa nao katika
kutekeleza majukumu ya umma. Miaka ishirini na tisa (29) iliyopita
nilipata fursa ya kufanya kazi ya mpira miguu kwa mara ya kwanza na Ndg.
Tenga, nikiwa nahodha wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Chuo kikuu cha Dar
es salaam, Desemba 1984, wakati Ndg. Tenga alipojitolea kuifundisha timu
ya Chuo Kikuu cha DSM. Tangu wakati huo hadi sasa imani na ushirikiano
katika utekelezaji wa majukumu ya umma niliopata kutoka kwa Ndg. Tenga
haujawai kutetereka hata kwa siku moja. Ni faraja kubwa kwangu kufanya
kazi hizi za umma chini ya kiongozi anayeheshimika na kuaminika na wadau
wa soka hapa nchini, Afrika Mashariki na Kati, Afrika na familia ya
soka Duniani kwa ujumla.
9. Mwisho, kwa viongozi na wadau wote wa mpira wa miguu, nawashukuru na nawatakia kheri, baraka na mafanikio katika Uchaguzi Mkuu wa TFF na ujenzi wa soka la nchi yetu..
Asanteni.
Deogratias J. Lyatto
19 Julai 2013, Dar es salaam, Tanzania.