|
Hamad Juma akichuana na Ramadhani Singano 'Messi' wa Simba katika picha tofauti |
KABLA ya kuwatungua Simba katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara lililochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki iliyopita, jina la Hamad Juma halikuwa maarufu masikioni mwa mashabiki wa soka.
Hata hivyo, mkwaju aliyomtungua kipa mkongwe na mzoefu nchini, Ivo Mapunda na kuipa ushindi timu yake ya Coastal Union, umelifanya jina la beki huyo wa pembeni kuwa gumzo midomoni mwa watu.
Hamad alifunga bao hilo pekee dakika moja kabla ya mapumziko baada ya kuuwahi mpira uliozembewa kuokolewa na Omar Salum, kisha kufumua shuti lililotinga likimuacha Ivo akigaragara mavumbini.
Mbali na kufunga bao hilo pekee, Hamad na wenzake pia walikuwa mwiba mkali kwa nyota wa Simba walioongozwa na Jonas Mkude, Ramadhani Singano 'Messi', Amisi Tambwe na Haruna Chanongo.
Beki huyo na wenzake walicheza 'jihad' wakianua kila aina ya hatari langoni mwao, huku kipa wao Fikirini Seleman akionyesha manjonjo yake na kuisaidia kuipa Coastal ushindi muhimu mbele ya Simba.
Ingawa beki huyo hakumaliza pambano hilo baada ya kutolewa katika dakika ya 60 kutokana na kuumia, lakini bao lake lilidumu hadi mwisho na kuifanya Simba ipoteze mchezo wake wa nne kwa msimu huu.
Hamad miongoni mwa wachezaji chipukizi waliopandishwa na Coastal msimu huu kutoka kikosi cha vijana, anasema anajisikia furaha kubwa kwa kufunga bao hilo pekee katika pambano hilo kali.
"Najisikia faraja kubwa kuweza kuifunga Simba, kwa sababu ni bao langu la kwanza, pia Simba ni timu kubwa iliyosheheni wachezaji nyota wa ndani na nje ya nchi. Ni furaha kubwa kwangu," anasema.
Beki huyo anasema hakutarajia kama angefunga bao hilo, licha ya maamuzi aliyoyafanya ya kufumua shuti baada ya kuuotea mpira langoni mwa wapinzani wao.
"Mpaka sasa siamini kama ni mimi niliyewatungua Simba," anasema.
NDOTO
Hamad kama wachezaji wengine wa rika lake anasema kiu yake ni kuja kucheza soka la kulipwa nje hasa barani Ulaya, pia kupata nafasi ya kuitumikia timu ya Taifa (Taifa Stars).
"Bado nina safari ndefu katika maisha yangu ya soka, lakini nitafurahi kama nitatimiza ndoto hizo na kufika mbali kisoka," anasema.
Mchezaji huyo anayependa kula ugali kwa samaki na kunywa juisi halisi, anasema anaamini kipaji cha soka na umri alionao utatimiza ndoto hizo za kucheza Ulaya na kuichezea Taifa Stars.
Hamad anayeishabikia timu ya Taifa ya Brazil, aliyekuwa akimzimia kisoka marehemu Patrick Mafisango aliyeichezea Simba, anasema soka la Tanzania linasonga mbele baada ya vijana kupewa nafasi.
Hata hivyo, anataka juhudi zaidi ziongezwe kwa vipaji vinavyoibuliwa kwenye michuano mbalimbali ya vijana kutunzwa na kuendelezwa ili vije kulisaidia taifa hasa kwa michuano ya kimataifa.
"Vipaji visiachwe vipotee, vitunzwe na kuendelezwa kwani ni hazina itakayolisaidia taifa baadaye," anasema.
FURAHA
Beki huyo anayewashukuru wazazi wake na wote waliomsaidia kufika alipo, anasema hakuna tukio la furaha kwake kama siku alipopewa nafasi ya kucheza pambano lake la kwanza la Ligi Kuu.
"Pambano hilo lilikuwa ni kati ya Oljoro JKT na Coastal jijini Arusha likiwa la fungua dimba na kwa bahati nzuri tuliibuka na ushindi wa mabao 2-0 ugenini," anasema.
Juu ya huzuni mchezaji huyo anayewataka wachezaji wenzake kuzingatia nidhamu ndani na nje ya uwanja, kupenda mazoezi na kuwasilikiza makocha wao, anasema ni lile la kumpoteza baba yake.
"Kumpoteza baba kabla hajaanza kula matunda ya mafanikio yangu kisoka kunaniuma, huzuni hiyo ni sawa na nilipoumia na kukaa nje ya dimba kwa muda kabla ya kupona," anasema.
Hamad anayependa kutumia muda wake wa ziada kusikiliza muziki akimzimia Sir Juma Nature, anasema kama siyo soka huenda angekuwa imamu wa msikiti kutokana na kupenda mambo ya ibada.
CHIMBUKO
Hamad Juma Hamis, alizaliwa Februari 25, 1994 mjini Tanga na alianza kucheza soka tangu akiwa kinda wakati akisoma Shule ya Msingi Darajani na kuendelea Sekondari ya Jumuiya zote za mjini Tanga.
Beki huyo anasema timu yake ya kwanza kuichezea ni Tanga Middle Age kabla ya kuonwa na Coastal iliyomchukua ili kuichezea timu ya vijana hadi msimu huu alipopandishwa timu ya wakubwa.
Kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa, Hamad aliisaidia Coastal Union kufika fainali ya Kombe la Uhai na kushika nafasi ya pili kabla ya msimu huu kikosi hicho kutwaa taji kwa kuilaza Yanga.
Hamas anasema hakuna mchezaji anayemuogopa uwanjani kwa kuwa anajiamini kwa kipaji alichojaliwa na Mungu na kukiri mpaka leo bado anamkumbuka marehemu Mafisango kutokana na kumzimia mno.
Anasema Mafisango alikuwa mkali na mwenye kipaji kikubwa cha soka kabla ya kipaji hicho kukatishwa na ajali ya gari iliyotokea Mei mwaka juzi.
"Yule jamaa achana naye, alikuwa anajua soka na alikuwa kivutio kwangu, Mungu amlaze pema," anasema Hamad.
Hamad anawashukuru makocha wake wote waliomnoa tangu shuleni mpaka kufika alipo, kadhalika anaushukuru uongozi wa klabu yake na wachezaji wenzake kwa ushirikiano wanaompa.