STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, October 3, 2013

Athuman Machuppa ampongeza na kumuonya Amisi Tambwe

Athuman Idd Machuppa akishangilia moja yha mabao yake alipokuwa akiichezae Vasalund ya Sweden

MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa klabu ya Simba na timu ya taifa, Taifa Stars, Athuman Machuppa amempongeza mfungaji mpya wa klabu hiyo Amisi Tambwe huku akimuonya ajipange zaidi ili asiye 'akafulia'.
Machuppa aliliambia MICHARAZO akiwa nchini Sweden kwamba japo hajamuona Tambwe akiwajibika uwanjani, lakini kwa sifa anazozisikia kuhusu mshambuliaji huyo Mrundi bila ya shaka ni 'bonge la Strika'.
Alisema kuanza kufumania nyavu mfululizo ni mwanzo mzuri kwa nyota huyo na kudai huenda anaisaidia Simba kurejesha heshima yake iwapo kama ataendelea kufunga.
Hata hivyo alisema kwa anavyoitambua Ligi ya Tanzania ni vyema mkali huyo akajipanga ili asije akaishia njiani kakma ilivyomtokea Mrundi mwenzake anayeichezea Yanga, Didier Kavumbagu.
"Kwa jinsi ninavyosikia simulizi zake ni wazi ni mmaliziaji mzuri na ataisaidia sana Simba na kwa kuanza kwake vyema na kuizoea mapema ligi ya Tanzania nampongeza na kumtaka aendeleze moto huo huo," alisema.
Machuppa aliongeza hata hivyo Tambwe hapaswi kulewa sifa  anazopewa na badala yake aongeze kasi ili aendelea kutamba na kuwapa raha wana Msimbazi sambamba na kutimiza ndoto zake za kuwa Mfungaji Bora.
"Unajua soka la Bongo halitabiriki, hata Kavumbagu alianza kwa kasi hiyo hiyo lakini mwisho wake umekuwaje, hivyo namsihi Tambwe asilewe sifa badala yake alinde kiwango chake kwa vile ligi ni ngumu," alisema.
Machuppa aliyemaliza mkataba wake wa kuichezea Vasby Utd inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ya Sweden akitokea Vasalund pia ya nchini humo, alisema hata mashabiki wa Simba wanapaswa kumsaidia Tambwe.
Juu ya kitendo cha Tambwe kufunga mabao manne katika mechi moja, Machuppa alisifu ni jambo zuri linalovutia, ila hapaswi kupambwa kama ni kitu cha ajabu sana, wakati wapo wabongo waliowahi kufanya hivyo na pia kuna vijana wenye makali zaidi yake ila hawaaminiwi na makocha wao.
Kadhalika Machuppa alidokeza kusudio lake la kutaka kubadilisha uraia ili awe raia wa Sweden, akidai kwa sasa anasikilizia maombi yake aliyoomba Idara ya Uhamiaji wa nchi hiyo akitaka kufuata nyayo za Shekhan Rashid nyota mwingine wa Tanzania aliyewahi kutamba Simba na Taifa Stars.

Maskini Niyonzima! Umeme wamtia hasara kwa kuunguliwa na vitu nyumbani kwake Magomeni Kondoa

Baadhi ya vitu vilivyoungua ndani ya nyumba ya Haruna Niyonzima wa klabu ya Yanga.
Hii ndiyo nyumba ya kiungo mahiri wa Yanga, Haruna Niyonzima iliyoshika moto baada ya hitilafu ya umeme.
Nyumba anayoishi Haruna Niyonzima ambayo ilipatwa hitilafu ya umeme na kuuguza baadhi ya vitu kabla moto huo kuzimwa usilete madhara zaidi. Tukio hilo limetokea leo asubuhi jijini Dar.
Baadhi ya samani za nyota huyo wa Kinyarwanda vilivyoungua kutokana na moto huo uliozuka asubuhi na kuwahiwa.

Haruna Niyonzima akiwa nje ya nyumba yake hiyo.
Kiungo Haruna Niyonzima akiwa nje ya nyumba yake iliyonusurika kuteketea kwa moto uliozuka ghafla majira ya asubuhi ya leo.
NYOTA wa klabu ya Yanga, Haruna Niyonzima asubuhoi ya leo ameunguliwa nyumba yake iliyopo Magomeni Kondoa kwa kile kilichoelezwa hitilafu ya umeme ambapo baadhi ya mali zake ziliungua kabla ya kuokolewa.
Inaelezwa kuwa moto huo ulizuka wakati wakiwa wamelala na kwa bahati mfanyakazi wake wa ndani alikuwa ameshamka na kuona tukio kabla ya kutoa taarifa na kufanyika juhudi za kuuzima moto huo ulioungua masofa na samani nyingine za mwanandinga huyo.
Hata hivyo ni heri hakukuwa na madhara yoyote kwa wakazi wa nyuma hiyo zaidi ya mali zilizoungua ambazo hata hivyo bado hazijafahamika thamani yake.

Mamlaka ya viwanja vya ndege (TAA) yajitosa bonanza la nyota wa Simba na Yanga Kisarawe


MAMLAKA ya viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imejitosa kudhamini Bonanza la Soka litakalowahusisha nyota wa zamani wa klabu za Simba na Yanga litakalofanyika kesho (jumamosi) wilayani Kisarawe Pwani.
Bonanza hilo lililoandaliwa na klabu ya Kisarawe Veterani, linatarajiwa kufanyika Oktoba 5 kwenbye uwanja wa Bomani likishirikisha klabu 10 toka mkoa wa Dar na Pwani.
Mratibu wa bonanza hilo kutoka kampuni ya Mdau Entertainment, Mohammed Masenga alisema mamlaka hiyo imekubali kuwadhamini ili kufanikisha michezo hiyo ambayo itawakutanisha wachezaji waliowahi kutamba katika soka nchini.
Masenga, alisema kujitokeza kwa mamlaka hiyo ni faraja kwao kwa vile ni nadra kuziona taasisi za serikali zikijitokeza kusaidia michezo kama hiyo ya maveterani.
Aliongeza kuwa wanaishukuru mamlaka hiyo na kutaka taasisi nyingine za kiserikali kuiga mfano huo.
Kuhusu bonanza hilo, Masenga alisema maandaliai yake yanaendelea vyema na kwamba kivumbi kitatimka jumamosi kwa kuwashuhudia nyota hao wa zamani wa Simba na Yanga wanazozichezea timu shiriki za veterani.
Masenga alisema timu shiriki zitakazochuana katika bonanza hilo ni pamoja na Majohe Veterani, Pugu Veterani, Kigogo Veterani, Ukonga, Segerea ya akina Spear Mbwebwe na Willy Martin 'Gari Kubwa', Mbagala ya akina Yusuph Macho 'Musso', Kinyerezi Veterani, Bandari ya akina Kennedy Mwaisabula na Yobo.
Nyingine ni Vituka, New Ukonga na wenyeji Kisarawe Veterani na mshindi wa kwanza atanyakua seti nzima ya jezi, huku wa pili ataambulia 'bips' na wa tatu kubeba mpira mmoja.

Beki Simba achekelea ushindani wa namba Msimbazi

Adeyum Saleh Ahmed
BEKI mpya wa klabu ya Simba Adeyum Saleh amekiri kuna ushindani mkubwa wa namba katika kikosi cha vinara hao wa Ligi Kuu ya Vodacom, lakini akidai anafurahia hali hiyo akiamini itasaidia kuinua kiwango chake na cha timu nzima.
Aidha beki huyo aliyesajiliwa Simba akitokea Miembeni ya Zanzibar, anasema Ligi Kuu ya Tanzania Bara ni ngumu na yenye ushindani huku wachezaji wake wakicheza kwa malengo kuliko ilivyo Ligi Kuu ya visiwani Zanzibar alitokea.
Akizungumza na MICHARAZO kwenye mahojiano maalum, Adeyum aliyewahi kuzichezea Malindi, Mafunzo na Oljoro JKT, alisema ndani ya Simba hakuna mchezaji wenye uhakika wa namba mpaka sasa kutokana na ushindani uliopo kitu kinachowafanya wachezaji wote kujifua vilivyo ili kuwavutia makocha.
"Hivi ndivyo inavyotakiwa kwa timu yoyote, kadri ushindani unapokuwa mkubwa ndivyo wachezaji wanaimarisha viwango vyao, naamini hata mimi kiwango changu kitapanda zaidi na kutimiza ndoto nilizojiwekea," alisema.
Beki huyo wa kushoto alisema moja ya ndoto zake ni kucheza soka la kulipwa nje ya nchi pamoja na kutamani aje kuitwa kuichezea timu ya taifa (Taifa Stars) kwani hajaridhika na kuichezea Zanzibar Heroes tu.
Pia mkali huyo aliyewavutia makocha na mashabiki mara alipojitokeza kwenye majaribio ya timu hiyo alisema Ligi ya Tanzania Bara ni tofauti kiushindani na ile ya visiwani Zanzibar.
Alisema Ligi ya Bara ni ngumu na wachezaji wanacheza kwa malengo kitu ambacho anatamani nyota wa visiwani wangepata fursa ya kuja kuicheza ligi hiyo ili kukuza viwango vyao na kuisaidia timu ya taifa ya visiwa hivyo.
Adeyum anayeisaidia timu ya taifa ya Zanzibar, kunyakua nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Chalenji ya mwaka jana, alisema ugumu wa ligi hiyo unafanya awe mgumu kutabiri itakavyokuwa mbeleni japo anatamani kuibebesha Simba taji la ligi la Vodacom.

Warundi kuwachezesha Twiga Stars, Msumbiji


SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Burundi kuchezesha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kwa wanawake chini ya miaka 20 Kanda ya Afrika kati ya Tanzania na Msumbiji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, Waamuzi hao watakaochezesha mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Oktoba 26 na 27 mwaka huu wataongozwa na Ines Niyonsara.
Niyonsara atasaidiwa na Jacqueline Ndimurukundo na Axelle Shikana, huku Irene Namiburu kutoka Uganda ndiye atakayekuwa mwamuzi wa mezani wakati Kamishna wa mechi hiyo ni Evelyn Awuor wa Kenya.
Wambura alisema mechi ya marudiano itachezwa jijini Maputo kati ya Novemba 9 na 10 mwaka huu, na itachezeshwa na waamuzi kutoka Madagascar.
Fainali hizo za Kombe la Dunia zitafanyika mwakani nchini Canada, ambapo Tanzania inashiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo ya Kombe la Dunia kwa wasichana.
Timu ya Tanzania tayari imepiga kambi mkoani Pwani ikiwa chini ya Kocha wake Rogasian Kaijage.
Wachezaji walioko kambini ni Amina Ally, Amina Ramadhan, Amisa Athuman, Anastazia Anthony, Anna Hebron, Belina Julius, Donisia Daniel, Esther Mayala, Fatuma Issa, Gerwa Lugomba, Happiness Lazoni, Harriet Edward, Hellen Maduka, Irene Ndibalema, Jane Cloud, Khadija Hiza na Latifa Salum.
Wengine ni Maimuna Hamis, Mwanaidi Khamis, Najiati Abbas, Neema Paul, Niwael Khalfan, Rehema Abdul, Sabahi Hashim, Sada Ramadhan, Shamimo Hamis, Shelder Boniface, Stumai Abdallah, Tatu Idd, Therese Yona, Violet Nicholas, Vumilia Maarifa, Yulitha Kimbuya na Zena Said.

MPAMBANO WA MASUMBWI KUFANYIKA PANANDI PANANDI OKT 26

MPAMBANO mwingine wa masumbwi kufanyika katika ukumbi wa panandi panandi Oktoba
26 mpambano huo wa mchezo wa masumbwi utakaokuwa chini ya uratibu wa Kinyogoli Fondition utawakutanisha mabondia mbalimbali wenye majina na wanaotamba kwa sasa katika anga za masumbwi nchini

Akizungumzia mchezo huo kocha wa Kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini kutoka kambi ya ilala Rajabu Mhamila 'Super D' amesema kuwa mpambano huo utawakutanisha bondia Yakubu Maganga atakae zichapa na Ubwa Salumu katika uzito wa kilo 75 huku Seif Ali akipambana na Hassani Labanda

pamoja na mipambano mengine ya masumbwi itakayo wakutanisha mabondia mbalimbali

Siku hiyo kutakuwa pia na huzwaji wa DVD kali za ngumi wakiwemo mabondia wakali wanaotamba Duniani na hapa nchini kama.Manny Paquaio, Saul 'canelo' alverez ,Floyd Mayweathar,Mike Tyson,Mohamed Ali,Ferex Trinidad,Miguel Cotto na wengine wengi
 
DVD hizo za ngumi kali zitakuwa zikiuzwa na kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D'
 
Pamoja na kutambua sheria na taratibu za mchezo huo siku hiyo pia kuta kuwa na vifaa vya mchezo huo wa masumbwi vitakavyotolewa  zawadi kwa mabondia na Kocha Super D  ambaye ame haidi kutoa, Gum Shit ,Clip Bandeji,DVD za Mafunzo kwa mabondia, Bukta,Protector na vifaa mbalimbali kwa mabondia watakao onesha uwezo wa ali ya juu wa kutupiana masumbwi

Liunda, Nkongo kushiriki kozi ya Futuro Addis Ababa

Liunda
Nkongo anayekimbia mbele

Na Boniface Wambura
MWAMUZI wa kimataifa wa zamani wa FIFA, Leslie Liunda na waamuzi Abdi Spud na Israel Nkongo ni miongoni mwa washiriki 30 walioteuliwa kuhudhuria kozi ya wakufunzi ya waamuzi ya FUTURO III itakayofanyika Addis Ababa, Ethiopia kuanzia Oktoba 5-10 mwaka huu.

Leslie Leonard Liunda, Abdi Soud Mohamed na Israel Nkongo Mujuni ndiyo watakaoshiriki katika kozi hiyo itakayoendeshwa na wakufunzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Kozi hiyo pia itakuwa na washiriki kutoka nchi nyingine tisa za Afrika. Nchi hizo ni Gambia, Ghana, Kenya, Liberia, Nigeria, Seychelles, Sierra Leone, Somalia na Uganda.