Mario Balotelli 'Super Mario' |
MSHAMBULIAJI wa Italia, Mario Balotelli 'Super Mario' ameendelea kuonyesha makali yake ya kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu ya Seria A baada ya jioni hii kuifungia timu yake ya Ac Milan magoli mawili wakiizima Palermo 2-0 katika mfululizo wa ligi hiyo.
Balotelli aliyetua Milan akitokea Manchester City ya Uingereza, alifunga mabao hayo katika kila kipindi bao la kwanza akilipachika kwa njia ya mkwaju wa penati dakika ya nane tu ya pambano hilo lililochezwa kwenye dimba la San Siro mjini Milan.
Kuonyesha kuwa kwa sasa yeye ni nguzo ya Milan iliyotolewa kimaajabu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa ya Ulaya na Barcelona waliowafunga mabao 4-0 katika mechi ya marudiano na kuzima ndoto zao za kutinga robo fainali baada ya awali kushinda magoli 2-0, Balotelli aliongeza bao la pili dakika ya 66.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo inayoongozwa na vinara Juventus, Siena ikiwa nyumbani ilibanwa mbavu na Cagliari kwa kulazimishwa suluhu ya kutofunga, Napoli waliendelea kuwafukuzia mabingwa watetezi Juve kwa kupata ushindi wa magoli 3-2 nyumbani dhidi ya Atalanta, huku Chievo Verona wakiwa ugenini waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 mbele ya wenyeji wa Pescara na Fiorentina iliichapa Genoa magoli 3-2.