STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, May 16, 2014

Du! Luis Suarez azidi kuvuna tuzo England

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Liverpool Luis Suarez amezidi kuongeza tuzo katika kabati lake la kuhifadhia tuzo zake, baada ya kuteuliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza msimu wa 2013-2014.
Nyota huyo aliyefunga mabao 31 na kutoa pasi 12 za mabao katika mechi 33 za ligi alizocheza, huku timu yake Liverpool ikizidiwa kidogo na Manchester City katika mbio za ubingwa, poia ndiye mfungaji bora wa ligi hiyo. 
Suarez, ambaye pia ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Wachezaji wa PFA na Mchezaji Bora wa Waandishi wa habari za Soka msimu huu, ameshinda tuzo ya nne msimu huu pamoja na ile ya kiatu cha dhahabu. 
Tuzo hiyo Suarez imekuja ikiwa ni saa chache baada ya meneja wa Liverpool Brandan Rodgers naye kutunukiwa tuzo ya kocha bora wa mwaka na Chama cha Makocha wa Ligi nchini humo. 
Rodgers amekuwa na msimu mzuri akiiongoza timu hiyo ya Merseyside kumaliza nafasi ya pili kwenye ligi. 
Kocha wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson ndiye alimkabidhi tuzo hiyo kocha huyo mwenye umri wa miaka 41, ambayo hutokana na kura zinazopigwa na makocha kutoka timu za madaraja yote manne.
Kabla ya hapo mshambuliaji huyo alikuwa na wakati mgumu kutokana na matukio ya utovu wa nidhamu yaliyomsababisha kufungiwa kucheza mechi kadhaa na kutoza faini kwa kumbagua Patrick Evra na kung'ata beki wa Chelsea.

HUYU NDIYE AMINA NGALUMA 'JAPANESE'


MIEZI miwili iliyopita nilifanya mahojiano na Amina Ngaluma kuhusu shughuli zake za muziki akiwa ughaibuni, Mashariki ya Mbali nchini Thailand ambapo alieleza mambo mengi kuhusu safari yake na ndoto zake katika tasnia ya muziki aliyoianza tangu akiwa kinda.
Mwanamuziki huyo aliyefariki jana nchini Thailand, atakumbukwa kwa kiu yake ya kufika mbali kisanii.
MICHARAZO inakuweka makala ya mwanamuziki huyo kama alivyozungumza na blogu hii na iliyotumika pia kwenye gazeti la NIPASHE, kujua historia yake kama njia ya kumuenzi mwanamuziki huyo aliyekuwa mcheshi wa kila mtu.
ISOME:

MASHABIKI wa muziki wanamfahamu kwa jina la Japanese, ingawa majina yake halisi ni Amina Kassim Ngaluma, mmoja wa waimbaji mahiri wa kike wa muziki wa dansi nchini anayefanya kazi ughaibuni.
Japanese, aliyewahi kuziimbia bendi mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa sasa anafanya shughuli zake za muziki akiwa na bendi ya Jambo Survivors iliyopo Thailand, Mashariki ya Mbali barani Asia.
Mwanadada huyo anakiri licha ya kipaji cha muziki cha kuzaliwa, lakini alijikuta akipenda kuwa mwanamuziki kwa kuvutiwa na muimbaji nyota wa zamani wa Kongo, Mbilia Bell.
Anasema sauti na uimbaji wa Mbilia ulikuwa ukimkuna na kutamani kuwa kama muimbaji huyo, hivyo kuja kuangukia mikononi mwa nyota wa taarab nchini, Bi. Shakila Said, aliyemnoa kwenye uimbaji.
"Siyo siri nilimzimia mno Mbilia Bell, nikatamani kuwa kama yeye na kwa bahati nikaangukia mikononi mwa Bi Shakila aliyeninoa na kuwa hivi nilivyo kupitia kundi la JKT Taarab," anasema.
Anasema hata hivyo alipata wakati mgumu kwa vile mama yake hakupenda awe mwanamuziki badala yake kutaka afanye kazi za ofisi, tofauti na baba yake aliyemuunga mkono hadi leo ukubwani.
Japanese anasema baada ya kuiva kwa Bi Shakila pale JKT Taarab alihamia katika muziki wa dansi akianzia Less Mwenge-Arusha kisha   kukimbilia Kenya alipojijengea jina akizipigia bendi mbalimbali.
"Niliizipigia bendi za Sayari iliyokuwa chini na Badi Bakule 'Mkandarasi', Sky Sound iliyoongozwa na Mwinjuma Muumin, kisha Mangelepa ya Evanee kabla ya kurejea Tanzania," anasema.
Anasema aliporejea nchini alijiunga na African Revolution 'Tamtam' iliyomjengea jina kabla ya kwenda Double M Sound kisha TOT-Plus kabla ya kuhamia Jambo Survivors alionao mpaka sasa.
Japanese anaitaja bendi ya African Revolution kama ilimtambulisha katika ulimwengu wa muziki, ila bendi ya mafanikio na maendeleo kwake ni Jambo Survivors iliyomuinua kiuchumi toka alipokuwapo.

MKALI
Japanese aliyekuwa mahiri kwa mchezo wa Netiboli alioucheza kwa mafanikio kabla ya kutumbukia kwenye muziki, pia ni mahiri kwa utunzi wa nyimbo baadhi ya tungo zake ziliwahi kutikisa muziki wa Tanzania.
Baadhi ya nyimbo alizotunga mwanadada huyo mwenye ndoto za kuja kumiliki bendi binafsi akishirikiana na mumewe ambaye pia ni mwanamuziki Rashid Sumuni ni; 'Mapendo', 'Manyanyaso Kazini', 'Ukewenza', 'Wajane' na Mwana Mnyonge'.
Pia alishawahi kupakua albamu binafsi iitwayo 'Jitulize' aliyoizindua mkoani Morogoro ikiwa na nyimbo sita baadhi ni 'Jitulize', 'Uombalo Hutopata', 'Pete ya Uchumba', 'Mapenzi ya Kweli' na 'Tulia Wangu'.
Japanese anayefurahia tukio la kufunga ndoa na mumewe Rashid Sumuni na kulizwa na kifo cha kaka yake, Mashaka Ngaluma aliyeuwawa na majambazi kwa kupigwa risasi akiwa kazini kwake.
"Kwa kweli matukio haya ndiyo yasiyofutika kichwani mwangu, nilipofunga ndoa na mume wangu kipenzi, Rashid Sumuni na siku kaka yangu alipouwawa kwa risasi akiwa kazini," anasema.

MAFANIKIO
Japanese asiyefuatilia soka aliota kuja kuwa Daktari ila muziki ukaja kumbeba jumla, ingawa hajutii kwa namna fani hiyo ilivyomsaidia kwa mambo mengi ya kujivunia.
Anasema mbali na kupata rafiki wengi, kutembea nchi mbalimbali duniani na kujifunza tamaduni tofauti, pia muziki umemwezesha yeye na mumewe kumiliki miradi kadhaa ya kiuchumi, nyumba na magari.
Hata hivyo anasema bado hajaridhika hadi atakapoanzisha bendi yao ya Skwensa hapa nchini itakayokuwa ikipiga mahotelini na kurekodi kazi zake katika studio yao binafsi.
Pia angependa kuwasaidia waimbaji wa kike ili kusaidia kuongeza idadi yao katika muziki wa dansi alikodai imekuwa ikizidi kupungua kwa sababu wengi wao hawapendi tabu wala kujifunza muziki.
"Waimbaji wa kike hawapendi dansi kwa ugumu wake hivyo huona bora wajikite kwenye muziki wa kizazi kipya, ila kujifunza muziki wa dansi hasa upigaji ala husaidia kujitangaza kimataifa," anasema.

JUMBE
Japanese alizaliwa Nov 29, mjini Morogoro akiwa ni mtoto wa tatu kati ya tisa wa Baba Kassim Ngaluma na Mama Khadija Abdallah, watatu kati yao wakiwa wameshatangulia mbele ya haki ya kubakia sita tu.
Mkali huyo yupo Jambo Survivors inayopiga muziki wake katika hoteli iitwayo Banthai Beach Resort & SPA akiwa na Hassan Shaw, Eshter Lazaro, Ramadhani Kinguti, Yuda Almasi na mwana BSS Edson Teri.
Mwanadada huyo anasema kwa hapa nchini anawazimia wanamuziki  Hussein Jumbe na Nyota Waziri.
"Hawa ndiyo wanaonikosha na umahiri wao katika muziki," anasema.
Japanese anayewataka wanamuziki wenzake kuwa wabunifu ili kwenda na mabadiliko ya dunia na kuiomba serikali kuutupia macho muziki wa dansi anamshukuru Mungu kwa kumsaidia kufika alipo.
Pia anawashukuru wazazi wake kwa sapoti kubwa anayompa, mumewe Rashid Sumuni pamoja na mwalimu wake Shakila Said bila kuwasahau wote walio bega kwa bega katika fani yake kwa ujumla.

Zimbambwe usiku wa leo, Samatta waja kuibeba Stars

Samata (kati) na Ulimwengu (kulia) wakiwa na Kiemba . Nyota hao watatua keshjo kuisaidia Stars kuiangamiza Zimbabwe
TIMU ya soka ya taifa ya Zimbabwe inawasili usiku wa kuamkia Jumamosi (Mei 17 mwaka huu) ikiwa na msafara wa watu 27 kwa ajili ya mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa Afrika mwaka 2015 nchini Morocco Jumapili, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Timu hiyo itatua saa 7.30 usiku kwa ndege ya Ethiopian Airlines na itafikia hoteli ya Sapphire Court iliyopo Mtaa wa Lindi, Dar es Salaam.

Zimbabwe itafanya mazoezi siku hiyo jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam tayari kwa mechi hiyo itakayochezwa Jumapili saa 10:00 jioni kwenye uwanja huo huo.
Wakati huo huo: Wachezaji wa kimataifa wa Tanzania wanaochezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanatarajiwa kuwasili Jumamosi mchana (Mei 17 mwaka huu) kujiunga na Taifa Stars kwa ajili ya mechi dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors).
Washambuliaji hao watatokea moja kwa moja Sudan ambapo kesho (Mei 16 mwaka huu) TP Mazembe itacheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya timu ya huko.
Ujio wa washambuliaji hao utafanya wachezaji wote kutoka nje walioitwa na Kocha Mart Nooij kuwa wamepatikana kwa ajili ya mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Afrika ambalo fainali zake zitachezwa mwakani nchini Morocco. Mchezaji mwingine wa nje ambaye tayari ameripoti Stars ni Mwinyi Kazimoto anayecheza nchini Qatar.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linamshukuru Mmliki wa TP Mazembe ambaye pia ni Gavana wa Jimbo la Katanga, Moise Katumbi kwa kuwaruhusu wachezaji hao kujiunga na Taifa Stars kwa vile mechi dhidi ya Zimbabwe ipo nje ya kalenda ya FIFA.
Naye Kocha Nooij atakuwa na mkutano na Waandishi wa habari kesho (Mei 16 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye kambi ya Taifa Stars iliyopo katika hoteli ya Accomondia.

Simanzi! Amina Ngaluma Japanese afariki ughaibuni

Amina Ngaluma Japanese enzi za uhai wake
TASNIA ya muziki wa dansi imezidi kupata pigo baada ya nyota wa zamani wa bendi za African Revolution 'Tamtam', TOT-Plus na Double M Sound, Amina Ngaluma 'Japanese kufariki dunia.
Mtunzi na muimbaji huyo aliyekuwa akiitumikia bendi ya Jambo Survivors amefariki dunia mchana wa jana akiwa ughaibuni nchini Thailand alipokuwa akifanya shughuli zake za muziki na bendi hiyo.
Taarifa ambazo MICHARAZO ilizipata mapema, zilisema kuwa marehemu alikumbwa na mauti baada ya kuugua ghafla kichwa na kubainika alikuwa na uvimbe uliopasuka na damu kuchanganyika na ubongo.
Baadhi ya wasanii waliowahi kufanya nao kazi, walisema kuwa walipewa taarifa na mume wa marehemu, Rashid Sumuni ambaye ni mcharaza gitaa kuwa mkewe amefariki ughaibuni.
Kifo cha Ngaluma kimetokea wakati wadau wa muziki wa dansi wakiwa hata hawajasahau msiba mzito uliowapata baada ya gwiji Muhidini Mwalimu Gurumo 'Kamanda' kufariki mwezi uliopita.
Mungu ailaze mahali Pema Peponi Roho ya Amina Ngaluma 'Japaness' ambaye alifanyiwa mahojiano na blogu hii miezi michache iliyopita akieleza mipango yake ya kuja kuanzisha bendi na mumewe.
Kwa hakika kila nafsi itaonja mauti, na siku zote kifo hutenganisha wapendanao na kukatisha ndoto za waja, ila kwa kuwa ni kazi ya Mola tunabidi kumshukuru Maanani kwani yeye alimpenda zaidi.