Mkurugenzi wa Joyland International School, Fredrick Otieno akihutubia wageni katika hafla iliyofanyika jana shuleni kwao Kigamboni. |
Mkurugenzi wa Joyland International School, Fredrick Otieno akicheza muziki na wanafunzi wake |
Fredrick Otieno (kulia) akionyesha kipajo chake cha kucheza muziki akichuana na mmoja wa walimu wake |
Imeelezwa dawa pekee ya Tanzania kufanya vizuri michezo ya kimataifa ni kuwaandaa wachezaji tangu wangali wadogo wakiwa wamejengwa moyo wa kizalendo na ufahamu wa mchezo husika badala ya kukurupuka.
Mkurugenzi wa Shule ya Kimataifa ya Joyland na nyota wa zamani wa soka wa nchini Kenya, Fredrick Otieno, ndiye aliyefichua hayo wakati wa mahafali ya kwanza ya wanafunzi wa Chekechea shuleni kwao, Kigamboni jijini Dar.
Otieno aliyewahi kuichezea Gor Mahia, alisema ili Tanzania iweze kuja kutamba katika michuano ya kimataifa ni lazima ikubali kuwekeza michezo mashuleni na kuwaandaa vijana na siyo kutegemea miujiza.
Alisema amekuwa akijisikia aibu kila mara timu na wanamichezo wa Tanzania wakichemsha kwenye michuano ya kimataifa licha ya ahadi na mbwembwe nyingi na kuamini siasa zikiondolewa michezoni Tanzania itang'ara kimataifa.
"Hakluna njia ya mkato kuyaendea mafanikio katika michezo zaidi ya kuwekeza na kuwajengea misingi imara wenye vipaji tangu utotoni, na katika kuliunga hilo shule yetu inatarajia kuanzisha mtaala wa kimataifa ambao utahusisha poa masuala ya michezo," alisema Otieno.
Otieno alisema kama kila shule itakuwa na programu za michezo kama moja ya somo la darasani na wanafunzi wenye vipaji wakaanza kupikwa mapema ni wazi miaka michache ijayo Tanzania itakuwa na wanamichezo wenye kutisha.
"Zamani michezo ilipewa kipaumbele na kushuhudia Tanzania ikitoa nyota mbalimbali, siasa zilikuja kuua suala hilo. Sasa ni lazima tuamke na Joyland inataka kuonyesha mfano wa kuja kutoa nyota mbalimbali wa michezo watakaokuja kulisaidia taifa na nawahimiza wengine wafanye hivyo," alisema.
Alisema anajisikia aibu kusikia Tanzania imeenda Scotland na kuambulia patupu katika michezo ya Jumuiya ya Madola na kudai ni wakati wa serikali na wadau wa michezo kwa ujumla kujipanga kuifuta aibu hiyo siku za baadae.