STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, June 1, 2012

Costa, Jabu, Kago watupiwa virago Simba, wanne wajaza nafasi zao

NYOTA watano wa kikosi cha Simba ambao kwa kiasi kikubwa waliisaidia timu hiyo kung'ara msimu huu wamedaiwa kutupiwa virago, huku nafasi zao zikichukuliwa na wakali wanne waliosajiliwa mpaka sasa ndani ya kikosi hicho. Habari za kuaminika ambazo zimenaswa jijini ni kwamba wachezaji walitupiwa virago ni nyota wa kimataifa toka Jamhuri wa Kati, Gervais Kago, mabeki wa kati Victor Costa na Juma Nyosso, Juma Jabu na Ulimboka Mwakingwe aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu. Aidha kuna taarifa nyingine kwamba naye Uhuru Seleman yupo katika mchakato pia wa kutemwa katika kikosi hicho iwapo atafanikiwa kupata timu, ikidaiwa ananyemelewa na Yanga. Kwa mujibu wa chanzo cha habari toka ndani ya Simba, ni kwamba Costa, Jabu na Kago wametemwa kwa kushuka viwango, huku Nyosso anaysakwa na Yanga pia, ametemwa kutokana na utovu wa nidhamu wa mara kwa mara anaoufanya dimbani na kuigharimu timu, huku Mwakingwe kwa umri na kuwa majeruhi wa muda mrefu. Nafasi za wachezaji hao mpaka sasa zimechukuliwa na wakali wanne walionaswa Msimbazi ambao ni Juma Abdallah, Mussa Mudde Mbongo aliyekuwa akicheza SOFAPAKA, Patrick Nkanu toka Congo na Ibrahim Rajab 'Jebba'. Viongozi wa Simba walinukuliwa jana kwamba, zoezi zima la usajili wa timu yao utaanikwa baada ya kamati zao za ufundi na mashindano kuendesha zoezi hilo kwa maelekezo ya kocha wao, Cirkovic Milovan. Zoezi la usajili nchini kwa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2012-2013 umefunguliwa rasmi leo Juni Mosi na unatarajiwa kumalizika mwanzoni mwa Julai kabla ya Ligi kuanza Agosti ambapo miongoni mwa timu zitakazoshiriki ni Polisi Moro, Mgambo Shooting ya Tanga na Prisons ya Mbeya zilizopanda daraja toka la Kwanza.

Wema Sepetu afafanua pete aliyovishwa Maisha Club

MSANII nyota wa filamu nchini, Wema Sepetu amefafanua uvumi ulioenea jijini Dar kwamba ameangukia kwenye penzi na mwanamuziki wa bendi ya Machozi, Mwinyi kiasi cha kuvishwa pete ya uchumba kama alivyofanyiwa na aliyekuwa boifrend wake, Naseeb Abdul 'Diamond' kabla ya kumwagana hivi karibuni. Wema alisema pete aliyovishwa mwishoni mwa mwezi uliopita ilikuwa ni igizo la filamu aliyokuwa akiishoot iitwayo 'Super Star' kazi binafsi anayokuja nayo ambayo sehemu kubwa inahusu maisha yake halisi. Mrembo huyo alisema wengi walishindwa kuelewa walipomuona akivishwa pete na Mwinyi na kukumbatiwa huku wakipigana mabusu kwa kuwa kamera zilizokuwa zikitumika kutengenezea filamu hiyo zilikuwa juu na hivyo hazikuonwa na watu. "Sio kweli kama nimechumbiwa na Mwinyi wa Machozi, ila tulikuwa tukiigiza filamu yangu ya kwanza binafsi iitwayo 'SUPER STAR' ambayo ni kama inazungumzia maisha yangu," alisema. Mwinyi amecheza kama Diamond katika filamu hiyo ambapo aliwahi kumvisha pete na kutamka maneno ya kusisimua kabla ya kuja kugeukana. Wema alisema filamu hiyo anatarajia kuizindua Juni 23 baada ya kukamilika na imemgharimu karibu Sh Milioni 30 mpaka sasa. Miss Tanzania huyo wa 2006 amesema filamu hiyo imewashirikisha wasanii kadhaa nyota, na anatarajia itakuwa filamu ya kusisimua kutokana na kuigiza sehemu kubwa katika uhalisi wa maisha yake kama WEMA SEPETU.

YANGA MPO? RATIBA YA UCHAGUZI WENU HII HAPA

Stars yafika salama Abidjan, kuwavaa Tembo wa Ivory Coast kesho

Kikosi cha Taifa Stars kimewasili salama mjini Abidjan mchana wa jana huku Kocha Mkuu wa timu hiyo Kim Poulsen akisema mechi dhidi ya Ivory Coast itakuwa ngumu. Kwa mujibu wa ofisa habari wa TFF Boniface WAmbura ambaye ameambatana na timu, Stars yenye wachezaji 21 ilikuwa iwasili hapa asubuhi, lakini ndege iliyobadilisha Nairobi ilichelewa kuondoka kwa saa tatu. Mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Taifa Stars na wenyeji Ivory Coast (Tembo) itachezwa Juni 2 mwaka huu Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny kuanzia saa 11 kamili jioni ambapo Tanzania itakuwa saa 2 kamili usiku. Licha ya kwanza, Stars ililazimika kuacha wachezaji wawili dakika za mwisho (Haruna Moshi na Nassoro Cholo), Kim amesema kikosi chake ambacho kimefikia hoteli ya Ibis bado kimejipanga vizuri kwa ajili ya mechi hiyo. “Tunaiheshimu Ivory Coast kwa vile ni timu ambayo inaundwa na baadhi ya wachezaji nyota wa dunia kama akina Drogba (Didier) na Yaya (Toure), lakini wajiandaa kupata wakati mgumu kutoka kwetu,” amesema Kim ambayo kikosi chake baada ya kuwasili hapa kilipata fursa ya kufanya mazoezi jioni. Kikosi cha Stars kinaongozwa na nahodha wake Juma Kaseja akisaidiwa na Aggrey Morris. Wachezaji wengine waliopo hapa na kikosi hicho ni Mwadini Ally, Deogratius Munishi, Amir Maftah, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Waziri Salum, Shomari Kapombe na Juma Nyoso. Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Salum Abubakar, Shabani Nditi, Edward Christopher, Mrisho Ngasa, Frank Domayo, Mbwana Samata, Ramadhan Singano, Simon Msuva na John Bocco. Mbali ya Kim, Benchi la Ufundi lina Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Mukebezi (Meneja wa timu), Juma Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank Mhonda (Physiotherapist) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
Msafara wa Stars hapa unaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Crescentius Magori lakini pia yupo Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi ambaye amekuja kushuhudia mechi hiyo.

Kipa Lyon akiri udhaifu, ajipanga

MLINDA mlango wa kutumainiwa wa timu ya African Lyon, Noel Lucas, amekiri kuwa msimu uliopita timu yao haikuwa katika ubora wake, huku mwenyewe akishuka kiwango jambo lililosababisha timu yao kunusurika kushuka daraja. Hata hivyo, alisema yeye binafsi amekuwa akitumia muda wake wa mapumziko kwao Kigoma kujifua ili kurejesha kiwango chake na akiamini pia usukwaji upya wa kikosi chao unaweza kutoa ushindani mkubwa katika msimu ujao. Akizungumza na MICHARAZO
kwa njia ya simu kutoka Kigoma, Lucas alisema Lyon kwa msimu uliopita ilicheza chini ya kiwango na kusababisha kuwa na wakati mgumu kabla ya kunusurika kushuka daraja dakika za mwisho. Kipa huyo aliyepoteza namba kwa kipa mwenzake Abdul Seif, alisema hata hivyo anashukuru timu yao kupona kurudi Ligi Daraja la Kwanza, akiamini msimu ujao itakuwa timu tishio huku mwenyewe akidai anajipanga upya. "Najipanga kurejesha makali yangu, sio siri msimu uliopita sikuwa katika kiwango kabisa na ndio maana nilipoteza namba," alisema Lucas. Kipa huyo ambaye kabla ya kutua Lyon alitamba timu za Small Boys ya Singida, FC Congo ya Kigoma na Toto Afrika ya Mwanza na mwaka jana kuipa Kombe la Taifa mkoa wa Singida 'Kindai Shooting' kwa mara ya kwanza mkoa huo kufanya hivyo.

Coastal yamng'ang'ania Nsa Job

UONGOZI wa klabu ya Coastal Union ya Tanga, umesisitiza kuwa umeshamalizana na mshambuliaji wa Villa Squad, Nsa Job, aliyedai bado hajasaini kwao. Aidha, uongozi huo umetangaza kuwanasa nyota wengine wawili, Selemain Kassim 'Selembi' aliyekuwa akiichezea African Lyon kwa mkopo akitokea Azam na Mohammed Soud wa Toto Afrika ya Mwanza. Afisa Habari wa Coastal Union, Eddo Kumwembe, aliiambia MICHARAZO kuwa, Nsa aliyenukuliwa hajasaini kokote, ameshamwaga wino kwao tangu wiki iliyopita hivyo ni mali yao kwa ajili ya msimu ujao. Kumwembe alisema, Nsa ni mmoja kati ya wachezaji watatu ambao wameshamalizana nao mpaka sasa kwa ajili ya kusuka kikosi chao kwa msimu ujao, wengine wakiwa ni Selembi. "Nsa ni mmoja wa wachezaji wetu wapya ameshasaini fomu za usajili tangu karibu wiki sasa, tunashangaa akituruka, ila huenda hakupenda watu wajue mapema, lakini ukweli ndio huo msimu ujao ni wetu," alisema. Msemaji huyo aliongeza kuwa mbali na wachezaji hao watatu, pia wanakaribia kumnasa kinda wa timu ya taifa, (Taifa Stars), Simon Msuva aliyekuwa katika timu iliyoshuka daraja ya Moro United akitokea kikosi cha U-20. "Kwa sasa tunamfukuzia Msuva ambapo tunakaribia kumnasa," alisema Kumwembe. Coastal Union iliyorejea Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu na kumaliza katika nafasi ya tano, tayari imetangaza kuwatema wachezaji wake tisa akiwemo Ally Ahmed Shiboli aliyemwaga wino Polisi Moro iliyopanda daraja msimu huu. Wengine waliotemwa sambamba na Shiboli ni Ramadhani Wasso, Ben Mwalala, Samuel Temi, Enock John, Laurent Mugia, Bakari Mohamed, Daudi Changula na Francis Busungu.

Malipo kiduchu yamkimbiza bondia ulingoni

BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Saleh Mkalekwa, amesema malipo madogo wanayolipwa mabondia wengi akiwemo yeye yamefanya wengi wao kufa maskini, jambo linalomfanya afikirie kuachana na mchezo huo kabla ya kutimiza ndoto zake. Akizungumza na MICHARAZO
, Mkalekwa mwenye rekodi ya kucheza mara saba, akishinda sita na kupoteza moja, alisema alipotumbukia katika ngumi alikuwa na ndoto nyingi ikiwemo kutamba kimataifa, ila amekatishwa tamaa na malipo kiduchu anayolipwa. Alisema hali ya kulipwa kidogo haipo kwake tu, bali karibu mabondia wote ambao licha ya kuhatarisha maisha yao wamekuwa hawathaminiwi zaidi ya kuwanufaisha wasimamizi wa mchezo huo wakiwemo mapromota. Mkalekwa alisema kutokana na hali hiyo anafikiria kuachana na mchezo huo kwani haoni faida anayopata zaidi ya kuhatarisha maisha yake na kuwanufaisha waandaaji ambao wamekuwa wakiweka mbele masilahi yao kuliko ya mabondia na ngumi kwa ujumla. "Kwa kweli nilitamani mno kufika mbali kama walivyofika wakali wengine, lakini kwa jinsi tunavyonyonywa na kutumiwa kuwaneemesha wengine, ngumi zimenitumbukia nyongo," alisema. Alisema tangu alipoanza kupanda ulingoni mwaka 2008 hajawahi kulipwa pigano lolote malipo yanayozidi Sh 100,000, licha ya gharama kubwa za kuajiandaa na michezo hiyo kitu ambacho akihoji anaambiwa acheze kwanza ili akuze jina lake. "Wenzetu katika soka, hata kama ni chipukizi, wanalipwa fedha ambazo zinawatia nguvu kuendelea kuufurahia mchezo huo sio sisi, ndio maana unaona nimejiweka kando nikijifanyia mazoezi mwenyewe nikishughulisha na biashara ya spea za magari," alisema. Hata hivyo bondia huyo alisema iwapo atafanikiwa kupata mtu wa kumsaidia kumtafutia michezo yenye malipo ya kuridhisha na hasa ile ya kimataifa atakuwa tayari kuendelea na ngumi.

Hili Dude la Kitale videoni

VIDEO ya wimbo mpya wa mchekeshaji maarufu nchini, Mussa Yusuf 'Kitale' uitwao 'Hili Dude' inatarajiwa kuanza kurekodiwa wiki hii. Kitale, alisema atarekodi video hiyo baada ya kuona wapenzi wa muziki wameupokea vizuri wimbo wake huo ulioanza kushika chati katika vituo mbalimbali vya redio. Wakati msanii huyo akimalizia wimbo wa mwisho kuhitimisha albamu yake ya kwanza, alisema, wakati akianza kurekodi video hiyo, pia anajipanga kumalizia wimbo wa mwisho kwa ajili ya albamu yake itakayokuwa na jumla ya nyimbo nane. "Najiandaa kurekodi video ya wimbo wangu mpya wa 'Hili Dude' wakati pia nikijipanga kumalizia wimbo wa mwisho kwa ajili ya albamu yangu ya kwanza," alisema. Alisema mpaka sasa amekamilikisha nyimbo saba alizoshirikiana na wasanii mbalimbali akiwemo Sir Juma Nature na kuzitaja baadhi yake kuwa ni 'Chuma cha Reli', 'Kama Vipi Tulianzishe', 'Anajifanya Msela', 'Kinaunau' na 'Hili Dude'. Kitale, alisema amepanga hadi Julai awe ameikamilisha albamu yake itakayofahamika kwa jina la 'Kama Vipi Tulianzishe' sambamba na video ya nyimbo zote za albamu hiyo.

Loveness apika nyingine mpya

MSANII na mtayarishaji wa filamu anayekuja juu nchini, Loveness Watson 'Love' yupo jikoni akipika kazi nyingine mpya baada ya filamu yake ya 'Impossible Promise' kufanya vema sokoni. Akizungumza na MICHARAZO, Loveness alisema kama ilivyokuwa kwa kazi ya awali ya 'Impossible Promise, filamu hiyo nyingine ameitunga kuiandika na atatayarisha yeye mwenyewe. Loveness alisema, kazi hiyo mpya itakuwa na simulizi la mapenzi ambapo atashirikiana na wakali kadhaa nchini kuicheza filamu hiyo. "Baada ya kuitoa filamu yangu ya 'Impossible Promise' inayofanya vema sokoni kwa sasa nipo jikoni napika kazi hiyo ambayo natarajia kuiachia kabla ya Agosti," alisema. Aidha msanii huyo alisema pia yupo katika maandalizi ya kutumbukia kwenye muziki, akidai fani hiyo aliifanya siku za nyuma kabla ya kuingia kwenye uigizaji wa filamu kwa ushawishi wa kaka yake aliyemtaja kwa jina la Yokania Watson. Alisema tofauti na wasanii wenzake kuimba miondoko mchanganyiko, yeye atajikita zaidi katika mirindimo ya R&B.

Miss Tabata kufanyika leo, Mashauzi na Mashujaa Band kunogesha uhondo

Shindano la kusaka Miss Tabata 2012 linafanyika leo (Ijumaa) katika ukumbi wa Da’ West Park, Tabata. Mratibu wa shindano hilo Joseph Kapinga alisema jana kuwa bendi za Mashauzi Classic na Mashujaa zitawasindikiza warembo 19 watakaopanda jukwaani kuwania taji hilo. Mratibu wa shindano hilo lililoandaliwa na Bob Entertainment na Keen Arts alisema kuwa mshindi wa kwanza atazawadiwa Sh 500,000/- na king’amuzi ambayo imelipia miezi sita yenye thamani ya sh 800,000 iliyotolewa na Multichoice. Mshindi wa pili atapata sh 500,000, mshindi wa tatu sh 350,000 wakati washindi wa nne na watano kila moja atapata sh 200,000. Kapinga alisema warembo watano watawakilisha Tabata kwenye shindano la Miss Ilala. Warembo wengine watakaoingia 10 bora kila moja atapata sh 100,000 wakati waliyosalia watapata Sh 50,000 kila moja. Kapinga alisema shindano hilo pia litatumika kwa ajili ya kusherehekea miaka 10 tangu kuasisiwa kwa shindano la Miss Tabata. “Shindano la mwaka huu sio la kukosa kwani litakuwa ni la aina yake ukizingatia kuwa litatumika kusherekea miaka 10 tangua kuanza kuandaa Miss Tabata,” alisema Kapinga. Alisema warembo waliyowahi kushinda mataji mbalimbali ya shindano hilo, pia wamealikwa kusherehekea miaka 10 ya Miss Tabata. Shindano hili limedhaminiwa na Dodoma Wine, Redds, Integrated Communications, Fredito Entertainment, Multichoice Tanzania, Screen Masters, Kitwe General Traders, Step In Electronics, Brake Point, Atriums Hotel na Lady Pepeta. Mrembo anayeshikilia taji la Tabata kwa sasa ni Faiza Ally. Warembo wa Tabata wamekuwa wakifanya vizuri katika mashindano ya Miss Tanzania ambapo mwaka juzi Consolata Lukosi alishinda nafasi ya tatu kabla ya kutangazwa kuwa balozi wa kinywaji cha Redds. Katika shindano la mwaka juzi Juliet William pia alishinda nafasi ya tatu katika ngazi hiyo ya taifa. Juliet ndiye anayeshikilia taji la dunia la Miss Progressive International.
Washiriki wa Miss Tabata