ALIYEPIGWA RISASI NA ASKARI POLISI AKATWA MGUU
Na Antony Sollo - Kishapu.
HALI
si shwari katika mgodi wa mwadui,wananchi wamezidi kuuawa na kujeruhiwa
kwa risasi huku Serikali ikiwa haina majibu kuhusu kashfa zinazotokea
katika mgodi huo jambo ambalo hadio sasa wananchi wana mpango wa kuvamia mgodi huo kwa lengo la kuharibu mali za mgodi huo.
Kufuatia
hali hiyo,wananchi wa vijiji vinavyozunguka eneo la mgodi huo
wanajipanga kufanya vurugu kubwa katika mgodi huo ili kulipiza kisasi
kufuatia kushambuliwa kwa vijana watano ambao waliingia mgodini humo
hivi karibuni kama ilivyoripotiwa na Tanzania daima na hatimaye kupigwa
risasi na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za miili yao huku mmoja wa
vijana hao bwana Geroge Joseph akikatwa mguu.
Hali hii ni mwendelezo wa taarifa nyingi za kuuawa na kujeruhiwa kwa raia lakini
hakuna ufuatiliaji wowote kutoka kwa viongozi wa Serikali hususani
vyombo vya ulinzi na usalama kama jeshi la polisi jambo ambalo kwa siku
chache zijazo kama hali hii haitarekebishwa watanzania tukashuhudia
mapigano makubwa kati ya walinzi wa mgodi na wananchi.
Matukio
haya yamegubikwa na usiri mkubwa huku Viongozi mbalimbali wakiendelea
kutupiana mpira na kushindwa kueleza bayana juu ya ukweli wa matukio
haya na kibaya zaidi majeruhi aliyepata ulemavu huo bwana George Joseph
akiwatuhumu viongozi hao akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kishapu kwa kushindwa
kufika kwa muda muafaka kumuona na kumuombea ruhusa kwa uongozi wa
mgodi ili aende kupata matibabu.
Hali
hii inatokana na kwamba mgonjwa majeruhi huyo alikuwa akishikiliwa na
uongozi wa mgodi huo kwa tuhuma za kuingia mgodini isivyo halali jambo
lililosababisha kumchelewesha kwenda kupata matibabu hivyo kuharibika
kwa mguu wake na hatimaye kukatwa.
Kijana
huyo alilazwa katika hospitali ya mgodi wa mwadui tangu tarehe
9/01/2013 huku akiwa chini ya ulinzi wa askari wa mgodi huo lakini
kukiwa hakuna huduma zilizokuwa zikitolewa jambo lililosababisha aombe
kupewa rufaa bila mafanikio ambapo na hatimaye ndugu walifanikiwa
kumuondoa hospitalini hapo kwa kutumia nguvu na kumpeleka hospitali ya
Rufaa ya Bugando jijini Mwanza ambako amelazwa hadi sasa.
Akilalamikia
viongozi wa Serikali mgonjwa huyo Bwana George Joseph anasema”ndugu
mwandishi,Mkuu wa Wilaya ya Kishapu ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya
ulinzi na usalama ya Wilaya alikuwa ni mtu wa kwanza kumjulisha juu ya
tukio hili na aliahidi kufika hospitalini lakini hakufanya hivyo hadi
sasa nimethirika na kuwa mlemavu kwa kukatwa mguu wangu.
Kuhusu
kauli ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga kuwa hana
taarifa,inashangaza na inasikitisha sana kwani askari waliokuwa wamekuja
hapa kwa ajili ya kufanya operesheni walitoka mkoani Shinyanga.
Askari waliofika kunichukua
maelezo nao pia walitoka ofisi ya upelelezi ya Mkoa wa Shinyanga hata
operesheni hii huandaliwa na Mkoa,je haya madai kwamba hana na taarifa
yana lengo gani kama si kuficha ukweli wa jambo hili? na anafanya hivyo
kwa faida ya nani amehoji bwana George.
Wakiongea
na Tanzania daima wananchi waliozungumzia tukio hili walisema ndugu
mwandishi, kwa kweli kuna idadi kubwa sana ya watu waliouawa na
kujeruhiwa katika mgodi huu lakini hatuoni viongozi wetu wakifuatilia
masuala haya sijui hawana uchungu na wananchi ambao ndiyo rasrimali ya
taifa hili.
Kwa
sasa tukio hili limetupa hofu kubwa na sasa tunaiomba Serikali ijiandae
kuona machafuko makubwa kwa vile tumechoshwa na vitendo hivi katika
maeneo yetu.
tuna
mpango wa kwenda kuvamia mgodi na kuchoma ofisi mbalimbali pamoja na
kufanya uharibifu mkubwaili kuibua na kuweka wazi manyanyaso
tunayofanyiwa na mawekezaji wa mgodi wa Williamson mwadui maana kuna
usiri mkubwa mno kuhusu matukio ya unyanyasaji wa wananchi wa Maganzo na
vitongoji vyake.
Akiongea
na waandishi wa habari waliotembelea Ofisi za SHILEMA zilizopo katika
mji mdogo wa Maganzo, Katibu Msaidizi wa SHILEMA bwana Hamza Yusuph
amesema watu wengi wamepoteza maisha na viungo vyao kwa sababu ya
kuingia mgodini mwadui pasipo na uhalali wa kuingia mgodini humo,wote
tunajua kuwa kuingia mgodini ni kosa la jinai,lakini pia hatua za watendaji wa jeshi la Polisi kujichukulia sheria mkononi zinatokana sheria na mamlaka ipi?
Kwa
nini watu hawa wasikamatwe na kufikishwa mbele ya sheria kuliko kufanya
ukiukwaji huu wa sheria na kusababisha wimbi la vijana walemavu
kuongezeka! Vitendo hivi havikubaliki kabisa alisema bwana Selemani
mkaji wa kitongoji cha majimaji mji mdogo wa Maganzo.
Bwana
Yusuph amewalalamikia pia viongozi wa kisiasa wanaotumia mwavuli wa
kisiasa katika masuala yanayohusu maisha ya watu ili kujijengea umaarufu
katika nyakati za uchaguzi huku akiwalaumu viongozi wa kamati ya
mzunguko wa mwadui kwa kujali masilahi yao binafsi na kusahau kwamba wao ni wawakilishi wa wananchi.
Akizungumzia fedha zinazotolewa mgodini hapo bwana Yusuph amesema haelewi kama fedha hizo zinatolewa kama zawadi au
ni wajibu wa kampuni katika kuihudumia jamii hususani huduma za msingi
kama Elimu,Afya,Miundo mbinu,Maji,Umeme naBarabara kama ilivyo katika
maeneo mengine.
Bwana
Yusuph amelaumu pia Serikali kwa kushindwa kuweka wazi mikataba ya
Makampuni ya uchimbaji wa madini nchini kwa kuwa wananchi hadi sasa
hawaelewi mambo mbalimbali zikiwemo haki zao dhidi ya makampuni ya
uwekezaji katika maeneo yao.
Tanzania
daima ilibisha hodi katika Ofisi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
ya Kishapu Bwana Justine Sheka na kufanya mahojiano naye ambapo alianza
kwa kusema,ndugu mwandishi,sisi kama viongozi wa Serikali Wilayani
Kishapu tunashangazwa na uongozi wa mgodi wa Mwadui kwa kuendesha
shughuli zake kwa ubabe na usiri katika mapato yanayotokana na mgodi
huo.
Hadi
sasa uingiaji ndani ya mgodi huo una urasimu mkubwa kiasi kwamba hata
Mbunge wa Jimbo anapohitaji kuingia na kuangalia utendaji wa shughuli za
mgodi huo zinavyofanyika ni shida,unaingia ukiwa chini ya ulinzi mkali
na mara nyingine yapo madai kuwa ni lazima utoe taarifa mapema kwa
uongozi wa mgodi.
Lakini
pia amesikitishwa na jinsi Serikali ilivyofanya siri kuhusu uwakilishi
wake katika kukagua uzalishaji wa madini na namna ya kupata taarifa
mbalimbali ili kuweza kuona kama kweli mali inayopatikana ndiyo
inayotolewa taarifa kama ilivyo katika maeneo mengine yaliyo na migodi.
Inasemekana
ni muda mrefu mgodi wa Mwadui umekuwa ukiendesha shughuli za uchimbaji
wa madini Wilayani Kishapu bila kuwa na mwakilishi wa Serikali ambaye
anafanya ukaguzi jambo linalohofiwa kuporwa kwa madini na kuisababishia
Hasara Serikali.
Kamanda
wa Polisi Mkoani Shinyanga bwana Evarist Mangala alipotafutwa kujibu
malalamiko juu ya tuhuma zinazotolewa na mgonjwa aliyekatwa mguu bwana
George Joseph alisisitiza kwamba bado hana taarifa lakini akashauri
kwamba mgonjwa aandike barua ya malalamiko juu ya tukio hilo ili aweze
kulifanyia kazi.
CHANZO:Francis Godwin