STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, July 29, 2013

Ajali nyingine yachukua roho za watu

View of the bus that crashed on July 28, 2013 on the road between Monteforte Irpino and Baiano, southern Italy.
basi lililopata ajali nchini Italia (Picha:AFP)
WATU wapatao 38 wamepoteza maisha yao huku wengine wakikimbizwa hospitali kwa matibabu kutokana na ajali ya basi iliyotokea nchini Italia.
Waokoaji wa Kusini kwa nchini hiyo wamesema watu hao walikuwa katika basi hilo walilokuwa wakisafiria lililotumbukia ndani ya mtaro wenye urefu wa mita 30.
Baadhi ya abiria waliokimbizwa hospitalini kwa matibabu hali zao zinaelezwa kuwa mbaya kwa majeraha waliyoyapata katika ajali hiyo.
Inaelezwa kuwa basi hilo lilikuwa limebeba abiria waliokuwa wakirudi mjini Napoli kutoka jimbo la kusini la Campania. Haijabainika chanzo cha ajali hiyo iliyohusisha pia magari kadhaa na kwamba basi hilo lililokuwa limebeba abiria 50 wakiwamo watoto waliokuwa wanatoka Naples baada ya kufanya hija.
Basi hilo liligonga magari kadhaa kabla ya kuanguka ndani ya mtaro mjini Avellino.
Picha zilionyesha miili ya watu iliyokuwa imetapakaa kando ya barabara pamoja na magari yaliyokuwa yameharibiwa kwenye ajali hiyo.
Dereva wa basi hilo ni miongoni mwa wale waliofariki.
Waathiriwa kadhaa hata hivyo hawakuweza kutambulika , kwa mujibu wa msemaji wa polisi akisema kuwa wangali wanatoa miili katika magari yaliyoharibiwa. 
Ajali hiyo ya Italia imekuja siku chache baada ya watu wengine zaidi ya 70 kufa katika ajali mbaya ya Treni ya kwenda kasi iliyokea Kaskazini Magharib ya Hispania wiki iliyopita.
 
BBC

Serikali lawamani, kisa Mwigulu kufanya kazi zisizomhusu

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Slaa

 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi

MDHAHARO wa kujadili mstakabali wa amani ya taifa ulioandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA), umeibua mambo mazito ambapo washiriki wameinyooshea kidole serikali wakidai ndiye mchawi wa wananchi. 

Mdahalo huo ambao kauli mbiu yake ilikuwa ni Mustakabali wa Amani na Usalama wa Wananchi wa Taifa Letu kwa Miaka 50 Ijayo, ulifanyika jana katika Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwashirikisha wanazuoni, wanasiasa, viongozi wa vyombo mbalimbali vya ulinzi na serikali.

 Wachokoza mada walikuwa ni mhadhiri wa sheria wa chuo hicho, Dk. Onesmo Kyauke aliyegusia mfumo wa utendaji wa Jeshi la Polisi katika kusimamia amani ya nchi, Profesa Benadetha Kiliani, mtaalam wa sayansi ya siasa na utawala kwa umma na mwanahabari nguli na mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari, Dk. Ayoub Rioba.

 Katika mada yake, Dk. Kyauke aliliponda jeshi la polisi linavyokiuka sheria katika kutekeleza majukumu yake kiasi cha kuruhusu kuingiliwa na wanasiasa na kuelekezwa jambo la kufanya. 

Bila kuuma maneno, mhadhiri huyo alimtaja wazi wazi Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Tanzania Bara), Mwigulu Nchemba, akidai kwa sasa analiendesha jeshi hilo kwa kuingilia majukumu ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mwendesha Mashataka Mkuu (DPP). 

Alisema kuwa mwanasiasa huyo ambaye ni mbunge wa Iramba Magharibi, amekuwa akiwatuhumu wanasiasa wa vyama vya upinzani kuwa ni magaidi na polisi wamekuwa wakiwakamata na kuwafungulia mashtaka hayohayo anayosema kada huyo bila hata kuwa na ushahidi. 

Dk. Kyauke alitolea mfano wa matukio ambayo Nchemba amekuwa akiyafanya kuwa ni pamoja na lile la kuonyesha ushiriki wa kupanga tukio la ugaidi la Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), Wilfred Lwakatare. 

Tukio lingine alisema ni wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani jijini Arusha, ambapo kiongozi huyo aliwataka wananchi wa jiji hilo kutochagua madiwani wa CHADEMA kwa kuwa ni chama cha ugaidi kwa madai kwamba ndio waliohusika kummwagia tindikali kijana wa CCM kule Igunga. 

Kutokana na matamshi hayo, mhadhiri huyo alisema baadhi ya wanachama wa CHADEMA waliweza kukamatwa kama njia mojawapo ya kuisaidia polisi; jambo linalowafanya kama wasomi kujiuliza kuwa Mwigulu siku hizi kawa DCI au DDP? 

Kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi, alisema ndilo limekuwa chanzo kikubwa cha uvunjifu wa amani kwa kupoka haki ya Kikatiba ya wananchi kuandamana na kufanya mikutano huku akitolea mfano wa mauaji yaliyofanywa na jeshi hilo ya mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi, kijijini Nyororo, mkoani Iringa, wakati wa kuzindua matawi ya CHADEMA. 

Katika mauaji hayo, alisema ushahidi wa wazi umeonyesha namna gani polisi walivyoshiriki na tume zote zilizoundwa zikamuelekezea kidole Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa na Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa hadi leo zaidi ya polisi mwenye cheo kidogo akitolewa kafara huku mkubwa wake akiendelea kupandishwa cheo. 

Pia alisema kumekuwepo na upendeleo wa jeshi hilo kwa kutetea chama tawala ikiwemo enzi za IGP Omar Mahita kudai kuwashikilia wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) na majambia ingawa hadi leo wamekosa uthibitisho lakini kutokana na uongo huo wameshindwa kumchukulia hatua kiongozi huyo. 

Katika mapendekezo yake, Kyauke aliitaka polisi kubadili mfumo wake wa kufanya kazi, na kuhoji kwa nini Tanzania ni dhambi kuandamana huku akimtaka Waziri Mkuu kufuta kauli yake ya kutaka wananchi kupigwa tu na jeshi hilo wanapokaidi amri. 

Prof. Kilian kwa upande wake, alisema mpaka sasa bado kiini cha uvunjifu wa amani hakijagundulika na badala yake pande zote zimekuwa zikirushiana mpira ikiwemo serikali, wananchi na wanasiasa. 

Alizitaja sababu zinazochangia matukio hayo kuwa ni pamoja na hali ya upinzani kuja juu hivyo chama tawala kinajihami kutokana na mabadiliko hayo, kuongezeka kwa kiwango cha umaskini na mfumo wa kiliberali ambao umechangia matabaka na uhuru wa kutoa maoni tofauti na enzi za ujamaa. 

Naye Dk. Rioba alisema suala la amani sio la kuombewa kanisani au msikitini bali ni la kisayansi zaidi na kudai kwamba wanasiasa wamekuwa wakijidanganya pale wanapowahimiza watu kuliombea taifa liwe na amani. 

Pia Rioba alikanusha vyombo vya habari kuwa vimekuwa vikichangia kuharibu amani na badala yake alivifananisha vyombo hivyo na bunduki ambapo kama isipotumiwa kamwe haiwezi kuharibu amani. 

Akifafanua hili alisema vyombo vya habari vitaharibu amani endapo tu wanasiasa watavitumia na kuitaka jamii ielewe kwamba vyombo hivyo vina dhima kubwa kama mlinzi wa taifa na ndio maana wakati mwingine vinapendekezwa kuwa NGO’s ili viweze kufanya kazi kwa uhuru zaidi. 

Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk. Willibrod Slaa alisema mchawi wa hayo yote ni serikali, huku akinukuu ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyomtuhumu aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, na Msajili wa Vyama vya Siasa. 

Akisema amani sio suala la kuhubiriwa au kujadiliwa bali ni matokeo ya utekelezaji wa haki mbalimbali. 

Slaa pia alilalamikia vitendo vya ukatili vilivyofanywa Mtwara na vyombo vya dola dhidi ya wananchi, huku akimnyooshea kidole Brigedia Elia Athanas aliyekuwa amemwakilisha Mkuu wa Majeshi. 

“Jeshi letu lilikuwa linaheshimika sana, lakini siku za hivi karibuni linaelekea kupoteza heshima yake kwa jamii, tukirejea mfano katika uchaguzi mkuu uliopita ambapo mnadhimu wa jeshi, Abdulrahman Shimbo, alivyotoa kauli yenye utata, jeshi linaingiaje kwenye siasa wakati suala la uchaguzi ni suala la kiraia?” alihoji. 

Hoja ya Dk. Slaa kuhusu utendaji wa jeshi la wananchi mkoani Mtwara ilipingwa kwa haraka na Brigedia Athanas akisema: “Naomba kuweka wazi kuwa jeshi letu liko Mtwara, lina adabu na vitendo ambavyo vimekuwa vikiripotiwa ni vya propaganda tu kama alivyosema Dk. Slaa. 

Licha ya kiongozi huyo kujitetea, mchangiaji aliyefuata, Julius Mtatiro ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Tanzania Bara), alithibitisha kuwa wanajeshi wanabaka na walitenda vitendo vya kikatili dhidi ya raia na viongozi wa chama hicho akiwemo mkurugenzi wao, Shaweji Mketo. 

Mwakilishi wa NCCR Mageuzi, Faustine Sungura, alisema chama hicho hakiko tayari kufanya maandamano bali kinapambana kwa nguvu ya hoja na kwamba wataendelea kutumia nguvu ya hoja. 

Akihitimisha kongamano hilo, Wazri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema kuwa kati ya mambo ambayo yanampa changamoto ni amani ya nchi hii. 

“Tulirithi nchi ikiwa na amani, hivyo tuna deni la kurithisha nchi hii ikiwa ya amani katika kizazi kijacho. 

Dk. Nchimbi alikemea suala la udini, akiwatahadharisha Watanzania kuwa wasiingie katika vurugu na wasikubali kugawanywa kwa sababu ya dini zao. 

“Tukiingia katika vurugu za dini hatutapona, Wakristo na Waislam wote tukatae kugawanywa kwa kutumia misingi ya udini kwa manufaa ya Tanzania ya sasa na kizazi kijacho. 

Waziri Nchimbi huku akimtambua Dk. Slaa, alisema wanasiasa wote wana wajibu wa kuwatumikia wananchi, “Suala la amani sio suala la Chama cha Mapinduzi peke yake, ni suala la wanasiasa wote wa chama tawala na wapinzani kutambua kuwa wao ni watumishi wa umma, na kuvumiliana kisiasa ndiko kunaleta amani.

Taifa Stars watua kinyonge kupitia KIA

Wachezaji wa Stars wamekiwa wamepozi kusubiri safari ya kuja Dar wakitokea Kilimanjaro walipotua
Kocha Kim Poulsen na tabasamu la uchungu
Makocha Stars
Mfungaji wa bao pekee la Stars dhidi ya Uganda, Amri Kiemba na wenzake katika pozi.

Ngassa akiwa mbele ya wenzake


Wakipanda gari toka uwanjani
We mbona hupigi debe? Kama wanataniana wachezaji wa Stars (picha kwa hisani na Michuzi Blog)
Mwili haujengwi kwa mawe au matofali bali msosi kama hivi!


King Majuto, Mboto watikisa tena, After Death ya Kanumba kesho


MCHEKESHAJI mkongwe nchini, Amri Athuman 'King Majuto' ameibuka tena na filamu iitwayo 'Tikisa' ambayo inaendelea kutikisa katika soko la filamu Tanzania.
Katika filamu hiyo iliyoandaliwa na Salma Jabu 'Nisha' na kuandikwa na kuongozwa na Leah Richard 'Lamata', King Majuto kama kawaida yake anavunja mbavu mwanzo mwisho akishirikiana na Haji Salum 'Mboto' na wakali wengine walioigiza pamoja.
Kwa mujibu wa Lamata, mbali na  Majuto na Mboto, filamu hiyo imewashirikisha pia Hemed Suleiman 'PHD', Chuchu Hans, Jacklyne Wolper na wengine.
"Ni bonge la filamu ambalo karibu waigizaji wote wametikisa kama lilivyo jina la filamu yenyewe, ni moja ya kazi nzuri nilizowahi kuziandika na kuziongoza baada ya kutoka na 'Poor Minds' na 'Pain Killer'," alisema Lamata.
Katika hatua nyingine Lamata alisema kuwa filamu maalum ya kumuenzi marehemu Steven Kanumba 'The Great Pioneer' itaachiwa rasmi mtaani kesho Jumanne na kuwataka mashabiki wa nyota huyo wa zamani aliyefariki mwaka mwaka kukaa mkao wa kula kuipata filamu hiyo.
Lamata alisema filamu hiyo iliyowashirikisha nyota lukuki waliowahi kuigiza kazi mbalimbali na Kanumba enzi za uhai wake, imetungwa na na kuandaliwa na Jacklyne Wolper Massawe na kuongozwa na yeye na kwamba baadhi ya washiriki hao ni watoto Patrick na Jennifer walioibuliwa na Kanumba kupitia filamu kama Uncle JJ, Thisi is It na nyingine.
Pia wapo akina Patcho Mwamba, Wolper mwenyewe, Ben Blanco, Stanley Msungu, Irene Paul, Shamsa Ford, Mwanaidi Suka 'Mainda', Salama Salimin 'Sandra' na wakali wengine huku mhusika mkuu akiwa ni Philemon Lutwazi 'Uncle D' ambaye ameshabihiana na marehemu Kanumba.
'Shangazi mtu' Wolper akiwa na Jennifa na Patrick

Golden Bush Fc yatinga 10 Bora ligi ya Kinondoni


Kikosi cha Golden Bush Fc wakiwa na  makocha wao (wa kwanza kushoto waliosimama)  ni Waziri Mahadh 'Mandieta' na wa nane toka kushoto waliosimama) ni Madaraka Seleman 'Mzee wa Kiminyio'
TIMU ya soka ya Golden Bush Fc ya Sinza imekuwa klabu ya kwanza kufuzu hatua ya 10 Bora ya Ligi ya TFF Wilaya ya Kinondoni kuwania kupanda Daraja la Tatu baada ya kuikwanyua Spallows ya Kijitonyama kwa mabao 2-0.
Katika pambano hilo lililochezwa jana kwenye uwanja wa Mwananyamala, jijini Dar Es Salaam Golden Bush inayonolewa na nyota wa zamani wa Tanzania Shija Katina, Madaraka Seleman na Waziri Mahadh, ilipata mabao yote kupitia Zola.
Ushindi huo umeifanya timu hiyo kufikisha jumla ya pointi 21 na kuongoza katika kundi lake na hivyo kufuzu moja kwa moja kwenye 10 Bora kusubiri timu nyingine zitakaoungana nazo kusaka nafasi tatu za kupanda daraja la tatu.
Katika mechi zake 8 ilizocheza timu hiyo mpya kabisa, imeshinda mechi saba na kupoteza moja dhidi ya Kijitonyama ambapo ilifungwa bao 1-0 na kutibua rekodi yao ya kushinda mechi mfululizo tangu kuanza kwa ligi hiyo.
Mlezi wa klabu hiyo, Onesmo Waziri 'Ticotico' amewapongeza vijana wake pamoja na benchi nzima la ufundi kwa kazi nzuri waliofanya na kuwataka wasibweteke kwa vile hatua waliyotinga ni ngumu zaidi hivyo wagang'amale ili kuweza kutimiza malengo yao ya kuja kucheza Ligi Kuu misimu michache ijayo.

Polisi Dar wachimba mkwara mzito kuelekea sikukuu ya Eid

http://www.ippmedia.com/media/picture/large/Kova1(3)(2)(3).jpg
Kamanda Kova
JESHI la Polisi Kanda Maalum Mkoa wa Dar es Salaam imewatahadharisha na kuwaonya wakazi wa jiji hilo kuhusiana na vitendo vya uhalifu wakati wa kuelekea sikukuu ya Idd el Fitri ikiwataka kuwafichua wahalifu wanaoishi nao kabla kuingia matatani wahalifu hao watakapokamatwa.
Aidha jeshi hilo limesema limejipanga vyema katika kukabiliana na vitendo vyovyote vya uhalifu kwa kupeana mbinu mpya na kuwataka wakazi wa jiji hilo la Dar es Salaam kutokuwa na hofu yoyote na kuwahimisha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu bila mchecheto.
Kamanda wa Polisi kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema jeshi lao limejipanga vyema kukabiliana na vitendo vyote vya uhalifu kuelekea katika sikukuu na wakati wa sikukuu yenyewe, lakini akasema wanawategemea ushirikiano wa wananchi kwa kuwafichua wahalifu hao mahali walipo.
Kamanda Kova, alisema kwa vile wahalifu wanaishi katika nyumba za wakazi hao, ni wajibu wao kuwafichua wahalifu au watu wanaowatilia shaka ili Polisi lifanye kazi zake na ikitokea wahalifu hao wakaachwa hadi waje wakamatwe basi wahusika wa nyumba au eneo hilo wataingizwa matatani.
"Kama wananchi wanajua mahali walipo wahalifu au wanaishi nao na kushindwa kuwafichua siku tukiwatia mikononi watambue wenye nyumba hiyo nayo wataunganishwa pamoja na wahalifu hao, hivyo tunawatahadharisha na kuwaomba raia wema wasifumbie macho uhalifu," alisema Kova.
Aliongeza, Polisi wamejipanga kukabiliana na vitendo vyote vya uhalifu na hasa uvamizi wa kwenye maeneo ya biashara katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye sikukuu, lakini pia wanajitaji msaada na ushirikiano mkubwa toka kwa raia wema kudhibiti vitendo hivyo.
Kadhalika aliwatoa hofu wafanyabiashara na wateja wao kuwa wafanye shughuli zao kwa amani na utulivu kwa vile Polisi wamejipanga na kutawanya vijana wao kila mahali kuhakikisha jiji la Dar es Salaam na raia wake wanakuwa katika hali ya utulivu na salama.
Kamanda Kova alisema jeshi la Polisi linajisikia vibaya kuona raia wake wakiishi kwa wasiwasi mkubwa wa matendo ya uhalifu na hasa mtindo mpya wa kihalifu uliozuka hivi  karibuni wa kutumia pikipiki na kwamba wamehamasishana na kupeana mbinu mpya kukabili vitendo hivyo.
Kova aliyasema hayo mapema leo asubuhi wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Kumepambazuka cha Radio One Stereo.