STRAIKA wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Athuman Machuppa 'Smilling Killer' amezitaka klabu za Tanzania kuachana na ulimbukeni wa kuwapapatikia wachezaji wa kigeni na badala yake kutumia vipaji vilivyojazana nchini kuzijenga timu zao.
Machuppa alisema ni kweli wachezaji wa kigeni ni muhimu katika klabu, lakini sio wanaokuja nchini ambao wengi wao huwa ni wazee na walio na viwango vizivyotisha au kupitwa hata na wazawa.
"Nadhani klabu ziwekeze kwenye vipaji vya nyumbani, kuna wachezaji wengi wazuri Tanzania kama watatengenezwa na kuaminiwa, wageni waje lakini wenye viwango kama vya akina Emmanuel Okwi, Kipre Tchetche au wengine siyo kuletwa ilimradi tu na kulipwa fedha nyingi bila sababu," alisema Machuppa.
Mshambuliaji huyo aliyeweka maskani yake nchini Sweden kwa sasa akijiandaa kuwa raia wa nchi hiyo panapo majaliwa Mei mwakani, alisema hata idadi ya mapro katika vikosi vya klabu za Ligi kuu kutoka watano mpaka saba hakukuwa na sababu yoyote ya maana.
"Watano wangetosha tu, watatu wacheze na wawili wakae benchi, saba ni wengi na ninavyojua viongozi wa soka wa Tanzania walivyo na mzuka na wageni watalazimisha wote wacheze kama ruksa ilivyo, je wazawa wataonekana wapi, tutapata timu nzuri ya taifa vipi?"
"Watu wawekeze kwa vijana, Simba ilipata mafanikio ikiwa na wazawa waliojituma na kutumia vyema vipaji vyao, ila tusiwakatae wageni wanongeza chachu kama wakiwa ni wakali," alisema.