YANGA YAZINDUA KALENDA YAKE KWA MBWEMBWE
YANGA walitumia burudani ya muziki na wanenguaji kujaza watu kwenye makao makuu ya klabu yao jijini Dar es Salaam wakati wakizindua Kalenda yao ya mwaka 2013.
Mabingwa hao wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) wameingia ubia wa mwaka mmoja na kampuni ya ‘Pecha Media & Health Promotion’ kutengeneza kalenda za klabu yao.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Nasib Limira alisema kuwa kampuni yake imeamua kutengeneza kalenda za Yanga ili kuisaidia klabu hiyo kukuza uchumi wake.
Alisema klabu hiyo inayojiandaa kwenda Uturuki kuweka kambi kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu, ina vyanzo vingi vya mapato, lakini inakosa fedha nyingi kutokana na kuwapo kwa ‘wajanja’ wanaotengenezaa bidhaa kwa jina la klabu hiyo na kuziuza kwa faida yao binafsi.
“Yanga ni klabu kubwa, lakini inakosa pesa nyingi kutokana na kuwapo kwa watu ambao wanajinufaisha kwa kutengeneza kalenda na bidhaa nyingine wakitumia jina la klabu hii. Tumeamua kuwasaidia kutengeneza kalenda hizi ikiwa ni sehemu ya mchango wetu katika kuwasaidia kuinua kipato chao,” alisema Limira.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema kuwa kutengenewa kwa kalenda hizo ni mwanzo mzuri kuonesha kwamba wamedhamiria kuinua kipato cha klabu hiyo na kudhibiti mianya ya watu kutengeneza bidhaa kwa jina la klabu hiyo huku pesa za mauzo zikiishia kwenye mifuko yao bila klabu hiyo kunufaika chochote.
“Huu ni mwanzo tu, tunataka kuwadhihirishia wapenzi wa Yanga kwamba tuko makini na mali za klabu. Tumeanza na Kalenda, zitafuata bidhaa nyingine kama jezi maana watu wengui wamekuwa wakituhujumu katika hili,” alisema Mwalusako.
Alisema kalenda hizo zinauzwa kwa Sh. 5,000 na katika kila kalenda Yanga itapata Sh.1,500 na kwamba kampuni hiyo imeanza kwa kuitengeneza nakala 100,000.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa Yanga, ambao wamemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo wakiwa katika nafasi ya kwanza, kutengeneza kalenda maalum za klabu yao tangu ianzishe mwaka 1935.