STRIKA
USILIKOSE
Monday, August 13, 2012
Simba, Azam, Mtibwa zafuzu semi fainali Super8
TIMU za soka za Simba na Azam zinatarajiwa kukumbushia mechi yao ya robo fainali za Kombe la Kagame 2012 zitakapokutana katika nusu fainali ya Super 8 baada ya zote kufuzu hatua hiyo ya michuano hiyo maalum inayodhaminiwa na BancABC.
Simba imetinga hatua hiyo baada ya kuifunga Zimamoto ya Zanzibar mabao 2-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Simba walioingiza kikosi chao cha pili kwenye michuano hiyo, kinachonolewa na Kocha Suleiman Abdallah Matola, ilipata mabao yote yote kupitia kwa kiungo chipukizi anayeinukia vema katika soka ya Tanzania, Christopher Edward kipindi cha pili.
Christopher ambaye hukomazwa pia kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na kikosi cha kwanza cha Simba, alifunga bao la kwanza penalti dakika ya 50, baada ya beki Miraj Adam kuangushwa kwenye eneo la hatari.
Edward ambaye ni kipenzi cha kocha Mserbia wa Simba, Profesa Milovan Cirkovick, alifunga bao la pili dakika ya 55 baada ya kuwapiga chenga mabeki watatu wa Zimamoto kabla ya kumchambua kipa wa timu hiyo ya Zanzibar.
Pamoja na Simba SC kuwania ubingwa wa michuano hiyo, lakini sasa Christopher ameingia kwenye mbio za kiatu cha dhahabu cha michuano hiyo, kwa kufikisha mabao manne, akiwa anaongoza.
Katika michezo mingine ya kuhitimisha hatua ya makundi ya michuano hiyo, Uwanja wa Chamazi, Jamhuri FC iliichapa 4-0 Mtende, zote za Zanzibar mabao ya washindi yakifungwa na Sadik Rajab dakika ya 20, 44, Issa Achimwene aliyejifunga dakika ya 82 na Suleiman Khatib dakika ya 88.
Kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Azam FC ilitoka nyuma kwa bao 1-0 na kuifunga Polisi Moro FC mabao 2-1, mabao yake yakitiwa kimiani na beki Said Mourad dakika ya 20 na Abdi Kassim ‘Babbi’ dakika ya 70, wakati la Maafande wa Morogoro lilitiwa kimiani na Mokili Rambo dakika ya kwanza. Polisi ilimpoteza mchezaji wake, Abdallah Rajab dakika ya 88 aliyetolewa nje kwa kadi nyekundu.
Uwanja wa Amaan, Zanzibar, Kocha Mecky Mexime ataiongoza Mtibwa Sugar katika mchezo wa mwisho wa makundi dhidi ya wenyeji Super Falcon FC.
Katika Kundi A, Simba SC inaongoza kwa pointi zake nne, baada ya kutoa sare moja na kushinda moja, ikifuatiwa na Zimamoto na Mtende zinazofungana kwa pointi tatu kila moja, wakati Jamhuri inashika mkia kwa pointi yake moja.
Kundi B, Mtibwa inaongoza kwa pointi zake sita ikifuatiwa na Azam FC na Polisi Moro, zenye pointi tatu kila moja, wakati Falcon inashika mkia, ikiwa haina pointi hata moja.
Kwa kufuzu hatua hiyo, Simba inatarajiwa kuvaana na Azam, ambao katika mechi yao ya Kagame waliishindilia 'Mnyama' mabao 3-1 yote yakiwekwa kimiani na John Bocco aliyepo Afrika kwa sasa kifanya majaribio katika klabu ya Super Sports.
Mechi nyingine itakayochezwa mapema saa 8 siku hiyo ya Jumamosi itazikutanisha Mtibwa Sugar dhidi ya jamhuri ya Pemba.
Mechi zote za Nusu fainali na fainali zote zitachezwa Dar es Salaam. Mdhamini wa michuano hiyo, Banc ABC anagharamia usafiri wa ndege kwa timu zote kutoka kituo kimoja hadi kingine, malazi na jezi.
Kanuni za mashindano haya ni kushirikisha timu zilizoshika nafasi tatu za juu katika Ligi Kuu za Bara na visiwani na mbili zilioongoza katika kupanda Ligi Kuu zote mbili, lakini kwa Bara, Yanga waliokuwa washindi wa tatu msimu uliopita, walijitokea na nafasi yao ikachukuliwa na Mtibwa Sugar ambayo ilishika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu.
Bingwa wa michuano hiyo mipya itakayokuwa ikifanyika kila mwaka, ataondoka na Sh. Milioni 40, mshindi wa pili Sh. Milioni 20, wa tatu Sh. Milioni 15 sawa na wa nne, wakati washiriki wengine wataondoka na Sh. Milioni 5 kila moja.
NUSU FAINALI
Agosti 15, 2012
Mtibwa Sugar Vs Jamhuri (Saa 8:00 mchana)
Simba SC Vs Azam FC (Saa 10:00 jioni)
(Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam)
Subscribe to:
Posts (Atom)