STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, August 24, 2013

Huyu ndiye Muhidin Mwalimu Gurumo 'Mjomba' Muasisi wa Msondo Ngoma, Sikinde Ngoma ya Ukae na Ndekule

Mzee Gurumo akiwa na wanamuziki wenzake wa Msondo Ngoma, Hassain Moshi na Shaaban Dede
JUZI tasnia ya muziki ilipata simanzi kubwa kutokana na maamuzi magumu aliyoyafanya mwanamuziki gwiji nchini, Muhidin Mwalimu Gurumo 'Mjomba' a.k.a Kamanda alipotangaza kung'atuka kwenye muziki baada ya kuutumikia kwa miaka zaidi ya 50.
April mwaka jana (2012) nilikuwa miongoni mwa watu waliomtembea Mzee Gurumo alipokuwa akijiuguza nyumbani na kubahatika kufanya naye mahojiano yaliyozaa makala ndefu kuhusu alipoanzia alipotoka na alipokuwa akielekea.
Kwa ambao hawakubahatika kuisoma makala hiyo labda wajikumbushe kidogo historia ya mwanamuziki huyo mkongwe ambaye alikuwa tayari kugombana na wamiliki wa bendi mradi kuwatetea wanamuziki wenzake ambao aliamini kama siyo wao wamiliki wasingekuwa na chao na kutambulisha bendi zao.

Naiweka makala hiyo kama ilivyotoka gazeti la NIPASHE bila kupunguza wala kuongeza neno jingine ili mradi tu wasomaji wa blogu hiii mumjue Gurumo na kwa amewatia simanzi kwa uamuzi wake wa kujiondoa kwenye muziki wakati bado watu wanamhitaji kuanzia wanamuziki wenzake, mashabiki na hata taifa kwa ujumla.
=========
HUWEZI kuuzungumzia muziki wa Tanzania hasa miondoko ya dansi, bila kulitaja jina la Muhidin Mwalimu Gurumo (sio Maalim kama baadhi walivyozoea kumuita).
Hii ni kwa sababu mwanamuziki huyo mkongwe, maarufu kama 'Kamanda' au 'Mjomba', aliyewahi kutamba na kuziasisi bendi mbalimbali nchini ameutumia zaidi ya nusu ya umri wake katika mambo ya muziki, hivyo kuwa na mchango mkubwa katika fani hiyo.
Gurumo alianza fani ya muziki katika bendi za mitaani miaka ya 1950 akipitia bendi moja baada ya nyingine hadi leo akiwa na Msondo Ngoma, ingawa ameshindwa kupanda nao jukwaani kwa siku za karibuni kutokana na afya yake kutetereka kwa maradhi aliyonayo.
Mbali na mchango wake binafsi kama mwanamuziki, Gurumo mwenye umri wa miaka 71 amekuwa msaada mkubwa kwa wanamuziki waliowahi kuibuliwa naye au kufanya naye kazi kutokana na misimamo yake thabiti ya kulinda na kutetea haki za wanamuziki.
Baadhi ya wanamuziki waliowahi kufanya naye kazi na Gurumo ni Shaaban Dede 'Super Motisha', Bennovilla Anthony, Hassan Rehani ‘Bitchuka’ na wengine kadhaa wakiwemo waliotangulia mbele ya haki kama Suleiman Mbwembwe na Tx Moshi William, wamewahi kukiri jambo hilo.
"Kama viongozi wa bendi wangekuwa kama Gurumo katika kupigania na kutetea haki za wasanii, naamini tungekuwa mbali mno, mjomba (jina jingine la utani la Gurumo) huwa hataki mchezo," aliwahi kusema Dede.
Wakati wa mahojiano maalum na yeye yaliyofanyika hivi karibuni nyumbani kwake Mabibo jijini Dar es Salaam, Gurumo alisema kwamba kilichokuwa kikimsukuma kuwapigania wanamuziki wenzake na yeye mwenyewe ni dhamana ya uongozi na hali ya umaskini aliozaliwa nao.
"Unajua mimi nimezaliwa katika familia ya kimaskini na kimekulia kwenye umaskini, hivyo nafsi yangu huwa ngumu kumkandamiza maskini mwenzangu kwani naamini sio haki na dhambi kubwa kwa Mungu," alisema.
"Japo nilikuwa katika nafasi ya kufanya hila kwa kuegemea upande wa wamiliki wa bendi, ila kule kutambua kuwa uongozi niliopewa na wenzagu umetokana na imani  yao kwangu, ndio maana nilikuwa mkali kama pilipili kuwapigania wenzangu," aliongeza.
Gurumo, alisema hata alipokuwa akishawishiwa na baadhi ya wamiliki wa bendi ili kuwageuka wenzake ilimradi yeye aongezwe dau lolote analotaka, hakukubali kirahisi na  wakati mwingine kufikia kuamua kuhama iwapo dai lake halisikilizwi.
"Karibu bendi zote nilizopitia misimamo yangu ilikuwa hivyo na ikitokea uongozi ukawa mbishi  kukaidi madai ninayowasilisha kwao, huwa radhi kuondoka kama nilivyofanya OSS na kwingine," aliongeza.
Gurumo, alisema kutokana na misimamo hiyo mikali, alijikuta kila bendi aliyojiunga nayo wanamuziki wenzake humchangua kuwa kiongozi hadi sasa akielekea kustaafu fani hiyo kutokana na umri kumtupa mkono na maradhi yanayomsumbua kwa hivi sasa.
Alisema, tabia yake ya kutanguliza masilahi ya wanamuziki wenzake mbele kwa kiasi fulani yamechangia kushindwa kujijenga kimaisha kulinganisha na umaarufu wa jina lake na umri alioutumia katika fani hiyo ya muziki.
Gurumo, alisema katika umri wa zaidi ya miaka 40 aliyotumia katika muziki hana cha  kujivunia zaidi ya kujenga nyumba yenye vyumba 17 eneo la Mabibo, kujenga nyumba nyingine katika shamba lake lililopo kijijini kwao Masaki, Kisarawe, mkoani Pwani.
"Nyumba hii kama unavyoiona ambayo nimewapangisha watu na ninaendelea kuikarabati ndio pekee ya kujivunia, pia nina shamba nililojenga kibanda kingine huko Masaki, lakini kwa hadhi yangu nilipaswa kuwa mbali na hapa au vipi?" alisema Gurumo kwa kuhoji.

Gurumo akiwa nje ya nyumba yake ya Mabibo

Alisema, kwa hadhi yake wala asingekuwa akipigana vikumbo na mashabiki wake kwenye daladala aendapo kwenye shughuli zake na hata kwenye kliniki ya matatizo yake kiafya, lakini hana jinsi kwa vile hana uwezo wa kumiliki hata gari ndogo ya kutembelea.
"Naamini wengine wanaweza wasiamini, lakini ukweli ni kwamba sijawahi na wala sijui ni lini nitakuwa na usafari wangu binafsi, natamani lakini tatizo uwezo wa kifedha ndio tatizo, kama sio kujenga banda hili hapa Mabibo, sijui ingekuwaje," alisema.
Alisema, kinachomfanya awe katika maisha hayo licha ya umaarufu wake kimuziki,  Gurumo alisema mbali na kuthamini na kujali wengine, lakini ukweli ni kwamba enzi  akiutumikia muziki hakukuwa na masilahi ya kutosha kama wapatavyo vijana wa sasa.
"Huwa natamani miaka irudi nyuma na zama zile ziwe hivi sasa, ili nami niweze kunufaika na jasho langu katika muziki," alisema huku tabasamu la uchungu likimtoka usoni mwake.

MJOMBA
Mkongwe huyo aliyejifunza muziki tangu akiwa Shule ya Msingi Sungwi, iliyopo Kisarawe akiimba na kupiga dramu katika bendi ya shule, alisema safari yake ya muziki kwa kiasi kikubwa ilichangiwa na mjomba wake aitwaye Seleman Sultan Wamikole.
Alisema mjomba wake aliyemchukua tangu akiwa mdogo baada ya baba yake mzazi  Mwalimu Mohammed Gurumo, kufariki na kumuacha katika maisha magumu na ndugu zake wakiwa na mama yao Mwazani Sultan aliyefariki mwaka 1981.
Alisema kutokana na hali ilivyokuwa nyumbani kwao, mjomba wake huyo alimchukua na kuja kuishi nae Dar es Salaam maeneo ya Ilala ambapo moja kwa moja alimwandikisha katika madrasa ambako alipata fursa ya kuimba kaswida.
Alisema kuwa baadaye alipata hamu ya muziki hasa kutokana na kuvutiwa na kazi za nyota wa wakati huo, Salum Abdallah 'SAY' na Luambo Luanzo Makiadi 'Franco'.
Alisema mjomba wake huyo akishirikiana na mama yake walitambua kiu kubwa aliyokuwa nayo katika sanaa ya muziki na hivyo wakamruhusu kujiunga jumla ambako alizidi kuiva na baadaye kufuatwa na bendi mbalimbali.
"Kwa kitendo nilichofanyiwa na mjomba kwa kunitunza, kunilea na kunisaidia katika harakati zangu za muziki, ilinifanya nimtungie wimbo maalum nilikuwa OSS miaka ya  1980, wimbo uliitwa 'Shukrani kwa Mjomba'," alisema Gurumo.
Alisema anaamini kama sio mjomba na mama yake ambaye hadi leo anamliza akikumbuka alivyofariki, huenda asingefikia mahala alipo sasa kimuziki.
Mtunzi na muimbaji huyo mahiri nchini, alisema licha ya kipaji cha kuzaliwa, lakini Salum Abdallah na Franco ni watu waliochangia kufika kwake hapo alipo kwani enzi zao walimvutia mno.
"Ni kweli kipaji cha muziki nimezaliwa nacho na kukirithi kutoka kwa mama yangu Mwazani aliyekuwa kiongozi wa kundi la ngoma, ila kuvutiwa na Salum Abdallah na Franco ni sababu ya mimi kufika hapa nilipo, niliwapenda mno wanamuziki hawa," alisema.

SAFARI
Gurumo alisema baada ya kujifunza muziki kwenye makundi mbalimbali ya mitaani,  mwaka 1959 ndipo alipoanza kutambulika rasmi baada ya kuchukuliwa na bendi ya  Kilimanjaro Chacha.
Alisema alijiunga na bendi hiyo kama muimbaji ingawa pia alikuwa anamudu kupiga  dramu chombo alichokuwa akikipiga katika bendi ya shule na ndani ya bendi hiyo ndipo alipotunga kibao chake cha kwamba kilichoitwa 'Wakati Nikiingia Bar'.
Hata hivyo Gurumo alisema hakukaa sana Kilimanjaro Chacha kwani mwaka 1962  alihama na kwenda kujiunga bendi ya Rufiji Jazz alipokutana na wakali kama Salum  Nonde, Mbarouk Khalfan na wengine.
Alisema alijiunga na bendi hiyo kutokana na kushawishiwa na safari ambayo Rufiji Jazz ilikuwa ikitarajia kufanya mkoani Arusha na pia maslahi, hata hivyo miezi michache baadaye aliiacha bendi hiyo na kuhamia Kilwa Jazz B mwaka 1963.
Mzee Gurumo akiwa na baadhi ya tuzo zake wakati huo nilipomtembelea nyumbani
"Masilahi na ujana ndiyo ulionifanya niikache bendi ile na kutua Kilwa Jazz B, ambapo  kutokana na kipaji kikubwa cha uimbaji nilichokuwa nacho, uongozi wa Chama cha Wafanyakazi (NUTA) uliamua  kunichukua na kutua NUTA Jazz mwaka 1964," alisema.
Alisema kuwa alipotua NUTA alitunga kibao kilichokuja kumpa umaarufu cha kilichoitwa 'Mwangele', kikiwa na maana 'Mchumba' kwa lugha ya Kingoni na kisha kufuatiwa na nyimbo nyingine kadhaa.
"Kwa kweli idadi ya nyimbo nilizotunga nikiwa NUTA sizikumbuki kwa wingi wake, ila baadhi ni kama "Nimuokoe Nani', 'Kaka Seleman', 'Amina', Msondo Ngoma Na.1-4 na 'Maneno ya Nyerere'," alisema.
Gurumo alisema baada ya kuipandisha NUTA  iliyokuwa ikifahamika baadaye kwa jina la JUWATA, hasa alipowachukua wanamuziki nyota kama Bitchuka 'Stereo' na Said Mabera aliyekuwa akipuliza 'trumpet' katika bendi moja ya Arusha, Shirika la Teksi (TTTS) lilimfuata ili kuasisi bendi yao.
"TTTS walinifuata na kunieleza nia yao ya kutaka kuanzisha bendi na nikakubaliana nao ambapo walinilipa Sh 50,000, nikaondoka Juwata Jazz mwaka 1978 na kuasisi bendi ya Mlimani Park 'Sikinde' nikiwa na wanamuziki wenzangu wa Juwata na wengine kutoka Dar International," alisema.
Aliwataja baadhi ya waasisi wa bendi hiyo iliyokuja kufahamika kama DDC Mlimani Park kabla ya miaka mitatu iliyopita kurejea jina lake la awali baada ya kutemwa na mwajiri wao,  Shirika la Maendeleo mkoa wa Dar es Salaam, ni Hassani Bitchuka na marehemu Abel Baltazar aliotoka nao Juwata.
Wengine ni Joseph Mulenga 'Spoiler', Salum Machaku, Cosmas Chidumule, Hamis Juma  'Maalim Kinyasi', Ibrahim Mwinchande, Abdallah Gama na George Kessy kabla ya kuongezwa nguvu na akina Michael Enoch 'Teacher', Joseph Benard na Habib Jeff.

‘KASSIM WA KUTUMIA’
Alisema ndani ya Sikinde, kama kawaida aliendelea kutamba na utunzi wa nyimbo zilizotwaa umaarufu mkubwa ukiwemo wa 'Kassim' uliokuwa na sehemu mbili.
Gurumo alisema kibao hicho ni tukio la kweli lililomhusu rafiki yake aitwaye Kassim aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni ya mizigo uwanja wa ndege (DAHACO), ambaye alikuwa akisifika enzi hizo kwa ulevi na kusahau familia yake.
"Huu wimbo nilimtungia rafiki yangu ambaye alikuwa akiendekeza starehe kupita kiasi na kila nilipokuwa nikimsihi apunguze,  alikuwa akinitaka nimuimbe ndipo ataacha ulevi," alisema.
Alisema kuwa baada ya hapo, ndipo alipoamua kutunga 'Kassim namba 1', ambapo mwenyewe (Kassim) alikuwa akijisikia fahari, ingawa hakuacha ulevi hadi alipopatwa matatizo kazini na kuchacha ambapo kidogo aliacha pombe na yeye kumtungia Kassim Na.2'.
Gurumo alipokuwa amelazwa hospitali
Gurumo alisema mpaka sasa hajui kama jamaa yake huyo aliacha pombe na pia hajui kama yu hai au la kwa vile ni miaka mingi imepita bila kuonana naye.
"Sijui kama yu hai au la, ila nyimbo zile zilimhusu yeye katika kumkataza anasa ingawa pia nilikuwa natoa ujumbe kwa jamii," alisema.
Mkali huyo ambaye ni shabiki wa kutupwa wa Simba, akiwa ni mmoja wa wanachama wake tangu mwaka 1972 na pia anayeishabikia Manchester United ya Uingereza, alisema alikaa na Mlimani Park hadi mwaka 1985 alipojiunga na safari Sound (OSS) akiwa na Bitchuka.
Alisema alipotua OSS aliwakuta baadhi ya wanamuziki wake ambao wengi wao walitokea Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) wakilala chini na kuushinikiza kuwanunulia vitanda kama anataka aifanyie kazi bendi hiyo.
Alisema kuwa kwa bahati nzuri, uongozi ulimsikiliza  na kuwanunulia wanamuziki wote vitanda kama alivyotaka na kuanza kufanya kazi ikiwemo kubadili mtindo wa bendi hiyo wa 'Dukuduku Yee' na kuwa 'Ndekule'.
Gurumo alifichua kuwa mitindo yote aliyoasisi katika bendi za NUTA Jazz, Mlimani Park na OSS ya 'Msondo Ngoma', 'Sikinde Ngoma ya Ukae na 'Ndekule' ni ngoma ya asili ya kabila lake la Kizaramo ambazo mama yake alikuwa akiimba na kuzicheza enzi zake.
Alisema jambo hilo la kutumia ngoma za makabila ya kabila lake, ndilo ambalo hata wanamuziki nyota wa nchi za Kongo na mataifa mengine ya Afrika Magharibi wamekuwa wakifanya na kuutangaza muziki wao kimataifa tofauti na ilivyo nchini.
Mzee Gurumo akiwa na Nyoshi El Saadat
"Hata Wakongo na wanamuziki wa kimataifa kutoka nchi kama Senegal, Cameroon, Nigeria na Chad wamekuwa wakibuni muziki wao kwa kutumia ngoma za makabila yao, bahati mbaya vijana wengi wameshindwa kuumiza vichwa nao kubuni kazi zao na kuishia kunakili kazi za wenzao bila kujua wanawasaidia kuwatangazia, kwa kulikwepa hilo ndio maana nilikuwa nakubuni miondoko ya kabila langu la Kizaramo," alisema.
Gurumo, alisema sio jambo baya wanamuziki wa Tanzania kuiga kazi za wenzao, kitu alichodai ni vigumu kukikwepa, lakini alidai ni vema kama wangekuwa wakibuni vionjo vitakavyowatofautisha na wanamuziki hao wanaowaiga.
Alisema kwa muono wake ukiondoa Msondo na Sikinde zinazopiga muziki unaotambulika kama dansi la Tanzania, karibu bendi zote zinapiga muziki kwa kuwaiga wakongo, hata kwa zile bendi ambazo zilikuwa zikiaminika kuwa ni kilelezo rahisi kuitambulisha Tanzania kimataifa.

ULEVI
Gurumo hafichi kitu juu ya ujana wake kwa kueleza mbali na 'ubitozi' aliokuwa nao, pia alikuwa 'gangwe' enzi zake na pia aligeuzwa mtumwa wa pombe kutokana na kuwa mlevi aliyepitiliza.
Alisema, alikuwa anakata kilaji isivyo kawaida jambo ambalo lilikuwa likimfanya akorofishane na mama yake mzazi aliyetishia kumuachia 'laana' kama angeendelea kuendekeza ulevi.
"Kwa wanaonijua sidhani kama hili ni jipya, nilikuwa mlevi haswaa, kiasi mama alishindwa kunivumilia na kutishia kuniachia laana kama nisingesikilia wito wake wa kuachana na pombe," alisema.
Alisema, baada ya kushindana na 'shetani' kwa muda mrefu akikorofishana hata na mkewe, Pili bint Said Kitwana, hatimaye aliachana na ulevi mwaka 1982, miezi michache tangu mama yake mzazi kufariki.
"Ilikuwa ni kazi ngumu kuachana na pombe, lakini kwa heshima ya mama niliacha, pia shinikizo la mke wangu kipenzi ambaye ninampenda na kumsifia kwa uvumilivu wake, niliacha miezi michache baada ya mama kufariki na hadi leo situmii hiyo kitu," alisema.
Gurumo akiwa na wanamuziki wenzake wakongwe walipokuwa wakiandaa nyimbo maalum za Tanzania All Stars
Gurumo, alisema binafsi anajutia masuala ya ulevi akidai ni kati ya mambo yaliyochangia kumkosesha kufanya mambo ya maendeleo pamoja na kuihatarisha ndoa yake, kama mkewe asingekumvumilia kwa miaka 20 tangu walipooana mwaka 1962.
"Naamini ulevi uliopitiliza kwa hakika ni mbaya kama vijana wa sasa mnavyosema kwamba 'ulevi ni noma', nusura ndoa yangu ivunjike kwa ajili ya kuendekeza hii kitu, hata nilipotangaza kuachana na pombe si mke wangu wala marafiki zangu waliokuwa wakiamini hadi walipoona siku zikienda bila kupiga kilaji," alisema Gurumo.
Gurumo alisema hakuna kitu anachofurahia maishani mwake kama siku alipooana na mkewe, aliyezaa nae watoto wanne, Mariam aliyemzaa mwaka 1981,  Mwalimu, 28, Omar na Mwazani pamoja na alipoachana na pombe.
"Hivyo ndivyo vinavyonifurahisha hadi leo, nilipomuoa mke wangu na nilipoacha pombe, ila kwa huzuni ni kifo cha mama yangu, huwezi kuamini hadi leo huwa nikikumbuka natokwa machozi kwa namna mama alivyokuwa anikipenda na tulivyokuwa tunapendana na kuishi kwa upendo na furaha," alisema.
Gurumo, alisema maisha yake yamekuwa mikononi mwa mama yake kutokana na baba yake kufariki mwaka 1948 wakati akiwa na miaka nane tu, ndio maana amekuwa akimkumbuka kila mara marehemu mama yake.

BITCHUKA
Gurumo anayekula vyakula vyote halali na vyenye manufaa kwa afya yake na kunywa juisi na soda, alisema hakuna tukio lisilofutika kichwani mwake kama siku alipoamua kumsimamisha kazi 'swahiba' wake, Hassani Rehani Bitchuka.
Hassain Rehani Bitchuka
Alisema, alifanya uamuzi huo aliouita kuwa mgumu kuwahi kukutana nao maishani kama mwanamuziki mwaka 2005, baada ya Bitchuka kugoma kushiriki kwenye onyesho la pamoja kati ya Msondo Ngoma na African Stars 'Twanga Pepeta'.
"Bitchuka aligoma kushiriki onyesho hilo kwa madai asingeweza kufanya onyesho na watoto, kitu ambacho kiliwaudhi wanamuziki wenzake na wote waliniangalia mimi kama kiongozi wao nitafanya nini kwa kosa alilofanya 'swahiba' wangu ambaye tumekuwa katika 'udugu' tangu nilipomchukua toka Arusha mwaka 1973," alisema.
Alisema, hata hivyo alilazimika kusimama kidete kama kiongozi kwa kuweka kando 'uswahiba' wake kwa Bitchuka, ili kuinusuru Msondo na kuitisha kikao nilichotangaza kumtimua kundini, jambo ambalo anadai hadi leo humpa tabu kubwa kutokana na uhusiano aliokuwa nao na Bitchuka kwa mjda mrefu.
"Kwa kweli jinamizi la tukio lile hadi leo huniwewesesha, lakini tayari nilishazungumza na Bitchuka na kunielewa, pia unajua wakati mwingine ukiwa kiongozi unapaswa kufanya maamuzi magumu bila kutarajiwa," alisema.
Alipoulizwa juu ya msanii gani kwa sasa anayemuona kama ndiye mrithi atakayeendeleza gurudumu la muziki wa dansi nchini, Gurumo bila kificho alimtaja Husseni Jumbe mmiliki wa bendi ya Talent.
"Kwangu namuona Jumbe kama ndiye tumaini pekee la maendeleo ya muziki wa dansi kutokana na kipaji kikubwa alichonacho akitunga, kuimba, kupanga muziki na kujaliwa sauti ya kipekee," alisema.
Kuhusu muziki wa kizazi kipya, alisema upo juu kwa vile unatangazwa mno na vyombo vya habari, ila haoni kama ni muziki wenye nguvu unaoweza kuufunika muziki wa dansi.
"Promo ndio inayoubeba muziki huu, kitu kinachowalemaza wasanii wake kushindwa kuwa wabunifu na kujiona wamefika mbali, wakati wana kazi kubwa hususani ya kujifunza kupiga ala mbalimbali ili wapige muziki wao utakaokubalika kimataifa tofauti na sasa wakitegemea kila kitu kifanywe studio," alisema.
Hata hivyo alikiri wanaoufanya muziki huo na taarabu wamekuwa na mafanikio makubwa kimaisha kwa vile soko limewapokea vema, jambo ambalo hata yeye hupata wivu akifikiria anapowaona vijana wakiendesha magari wakati yeye akitembea kwa miguu licha ya muda mrefu aliotumia kwenye fani hiyo ya muziki.

SWAHIBA WA JK
Gurumo, alisema fani yake ya muziki imemsaidia kufahamiana na wengi wakiwemo viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, huku akimtaja Rais Jakaya Kikwete kwamba ni mmoja wa viongozi 'rafiki' zake.
Alisema, urafiki huo ndio anaoamini ulimfanya Rais Kikwete kuvunja shughuli zake na kumtembelea hospitalini kumjulia hali alipolazwa kwa mara ya kwanza kutokana na maradhi yanayomsumbua.
Gurumo, alisema kitendo cha Rais Kikwete kuacha kazi zake kwendsa kumjulia hali na kumsaidia katika matibabu yake kumemfariji mno, kwa vile katika kulazwa kwake na hata sasa akiendelea kujiuguza nyumbani hakuna kiongozi yeyote wa serikali wakiwemo wa Wizara wa Habari na Utamaduni, kuwahi kwenda kumjulia hali.
Rais Kikwete akimtunukia tuzo Mzee Gurumo wakati wa uzinduzi wa TBC
"Huwezi amini ni yeye na mkewe, Mama Salma ndio waliokuja kunijulia hali hospitalini, akianza mwenyewe kisha mkewe kitu ambacho kinanifariji hadi leo nikiamini Rais Kikwete anatujali na kututhamini wasanii," alisema.
Aliongeza kuwa, ukiondoa kufarijika kwake kutembelewa hospitalini na Rais Kikwete na mkewe, Mama Salma, pia kitendo kilichofanya na Mkurugenzi wa ASET, Asha Baraka cha kuandaa onyesho maalum kwa ajili ya kumchangia ni kitu ambacho kitabaki kichwani mwake na kumpongeza mwanamama huyo maaraufu kama 'Iron Lady'.
"Kwa kweli sikutarajia kama Asha Baraka angeweza kufanya kitendo kile ambacho ni wazi ninaonyesha ni jinsi gani anavyothamini na kujali mchango katika muziki. Nadhani watu wengine wanapaswa kuiga mfano wake, ni mtu ambaye ameonyesha mapenzi kwangu na kujali mchango wangu katika muziki, namshukuru na kumpongeza," alisema.
Gurumo, anayechizishwa na rangi nyekundu na nyeupe na ambaye anapenda kutumia muda wake za ziada kujishughulisha na mambo ya Kilimo kwenye shamba lake lililopo Masaki, alisema katika maisha yake kisanii amewahi kupata tuzo mbili tu zote za mwaka 2008.
Alisema tuzo hizo ni ile ya Kili Music Award kama Mwanamuiki Mkongwe na ile ya Hall of Fame, huku aliyekuwa mdau mkubwa wa muziki nchini aliyekuwa akifanya shughuli zake Umangani, Is'haka Kibene alimtengenezea na kumpa tuzo maalum kumtambua kama 'Kamanda wa Muziki wa Tanzania.
Mzee Gurumo akipokea msaada wa fedha toka kwa Asha Baraka 'Lady Iron' anayetajwa na gwiji huyo kama mwanamke wa mfano Tanzania katika kuuthamini mchango wake kisanii Tanzania
UBUNIFU
Gurumo, aliyeanza kuonekana tena kwenye jukwaa la bendi yake ya  Msondo baada ya kuwa nje kwa wiki kadhaa kutokana na kulazwa hospitalini, alisema muziki wa Tanzania umepiga hatua kubwa kimaendeleo, ingawa alikiri kwamba kukosekana kwa ubunifu miongoni mwa wananamuziki na wasanii wake ni tatizo linaloukwaza usitambe nje.
Alisema, hata muziki wa kizazi kipya (bongofleva) ambao umekuwa ukitajwa kama wenye maendeleo makubwa kwa wasanii wake, alisema unashindwa kutamba kimataifa kwa sababu wasanii hao hawaumizi vichwa kubuni vitu vipya.
Mkongwe huyo alisema tatizo la wasanii kupenda kuiga kazi za wenzao wa nje na kuzifanya zao kwa kuziimba kiswahili, ndilo linalowafanya wasitambe kimataifa na kutaka kuwepo kwa mabadiliko kuanzia sasa.
Alisema suala la kuiga kazi za nje halijaanza sasa, bali kitamboi kirefu akikiri hata wao (wakongwe) walikuwa wakifanya hivyo, ila alisema ubunifu wa ziada ndio uliowafanya waonekane mahiri katika soko la kimataifa.
"Kuiga ni jambo lisilokwepeka, lakini ni wajibu wa wasanii wa sasa kuumiza vichwa na kubuni vitu vipya ambavyo vitawatofautisha na wanaowaiga. Sio Bongofleva wala dansi kote wamelemaa kwa kuiga kazi za wenzao," alisema.
Alisema cha ajabu hata bendi za zamani ukiondoa Msondo Ngoma na Mlimani Park, zote hushindana kupiga muziki wa kikongo bila kujua wanasaidia kuutangaza muziki wa nchi hiyo na kuzidumaza bendi zao tofauti na Msondo na Sikinde.
Aliongeza anahisi bendi hizo zimeamua kuingia kwenye mkumbo huo kutokana na upepo wa soko ulivyo, japo alisema kimezifanya bendi husika zisiwasisimue mashabiki wake kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

KUSTAAFU
Gurumo, alisema hana muda mrefu kabla ya kutangaza kustaafu fani ya muziki kutokana na hali yake ya kiafya na umri mkubwa alionao akitaka kuwapisha wanamuziki wenye damnu changa kuendelea gurudumu la fani hiyo.
Mzee Gurumo alipotangaza kung'atuka kwenye muziki kando yake ni Meneja wa Msondo, Said Kiberiti na Juma Mbizo
Alisema, ingawa hajajua ni lini atafanya hivyo ila hadhani kama utamalizika mwaka huu wa 2012 kabla ya kutimiza azma hiyo na kudai atakapostaafu atajikita kwenye kuwasaidia vijana chipukizi.
Gurumo, alisema mipango yake ni kuanzisha chuo cha muziki anachotaka kukijenga Masaki, Kisarawe iwapo atapata mtu wa kumsaidia kufanikisha hilo kwa lengo la kutaka kuendeleza vipaji na kuudumisha muziki wa Tanzania.
"Sina muda mrefu kabla ya kustaafu rasmi muziki, sitajiweka kando kabisa na ndoto zangu ni kutaka kujenga chuo cha muziki katika shamba langu lililopo Masaki, lakini natatizwa na hali ya kiuchumi, hivyo kama serikali au mtu yeyote mwenye uwezo kifedha akinisaidia nitafurahi kwa vile nataka kuendeleza muziki wetu," alisema.
Alisema, anaamini vijana wanapaswa kujifunza mengi kutoka kwake na kwa wakongwe wengine ili kuufanya muziki wa Tanzania uendelea kudumu hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya kidunia.

FAMILIA
Muhidini Mwalimu Gurumo, alizaliwa mnamo mwaka 1940 katika kijiji cha Masaki, Kisarawe akiwa ni mtoto wa pili kati ya watatu wa mzee Mwalimu Mohammed Gurumo.
Baba yake alifariki wakati Gurumo akiwa na miaka nane tu na hivyo maisha yake ya utotoni kuwa chini ya mama yake mzazi kabla ya kuchukuliwa na mjomba wake aliyemsaidia kuingia kwennye muziki.
Gurumo, alifanikiwa kufunga ndoa na mkewe, Pili bint Said Kitwana na kubahatika kuzaa nae watoto wanne, ambapo ni mmoja tu aitwae Mariam ndiye aliyerithi kipaji chake cha muziki akiimba kundi moja la taarabu lililopo Temeke.
Mkongwe huyo anayemtaja Said Mabera 'Dokta' kama mmoja wa wanamuziki viongozi anayemzimia, alisema katika maisha yake ya ndoa hakuna anachokifurahia kama kudumu kwa ndoa yake na mkewe ambayo imetimiza miaka 50 mwaka huu.
Alisema, kama sio uvumilivu wa mkewe, huenda ndoa hiyo ingevunjika kitambo kutokana na ukweli ukiondoa ulevi na kazi yake ya sanaa, pia ukorofi aliokuwa nao uliochangiwa na ujana ni kati ya mambo yaliyotaka kuivunja ndoa yake.
"Sio siri najivunia kuwa na mke mvumilivu kama huyu, kuna mambo niliyomfanyia kwa muda mrefu ndani ya ndoa yetu, lakini alinivumilia hadi leo tukiingia mwaka wa 50 tangu tuoane mwaka 1962," alisema.
Aliongeza, kuwa anaamini ndoa yao ilikuwa mipango ya Mungu ndio maana wamedumu na kuzeeka pamoja wakiwa ndio kwanza wanapendana kama wameoana jana, jambo ambalo linamfanya kila mara kumshukuru Mungu.

MKEWE
Pili Bint Said Kitwana, alikiri kwamba ndani ya uhusiano wa kimapenzi hadi kuja kuoana na Gurumo alipitia katika misukosuko mingi, lakini anashukuru Mungu alijaliwa uvumilivu na kuidumisha hadi leo.
Mama huyo alisema ugomvi wake mkubwa na mumewe ilikuwa ni tabia yake ya ulevi, hali iliyomfanya mara kwa mara kukwaruzana nae akimsihi aache.
Mzee Gurumo akiwa na mkewe, Pili bint Said
Alisema, kuna wakati mumewe alikuwa akiondoka nyumbani Ijumaa kwenda kwenye maonyesho na asionekane hadi Jumatatu akiletwa na rafiki zake akiwa 'bwii', kitu kilichokuwa kikimuuma.
"Tatizo kubwa baina yangu na Gurumo ilikuwa suala la ulevi, hata alipokuja kuacha sikuamini," alisema.
Aliongeza, jingine ni tabia ya kuwa na 'kuchakachua nje', na kumfanya aumie roho hasa wanawake zake wa nje kumfuata na kumtukana na hata wakati mwingine kutaka kupigana nao hasa anapoamua kuambatana nae kwenye maonyesho.
Alisema, ukiondoa matatizo hayo, Gurumo ni mume bora, mpole, mkarimu  na baba anayejali familia mwenye mapenzi ya dhati, ndio maana aliamua kumvumilia hadi leo na kutoa wito kwa wanandoa wengine kuvumiliana katika ndoa zao ili kuzifanya zidumu kama ilivyo kwao.
Pia, alisema kitu kinachomfurahisha kwa Gurumo ni tabia ya kutochagua chakula cha kula, akidai hula chakula chochote isipokuwa 'kitimoto'.
Mama huyo alisema kwa namna mumewe alivyojitolea ndani ya taifa hili kupitia fani yake ya muziki ni vema serikali ikamkumbuka kwa kumsaidia angali akiwa hai, badala ya kusubiri aje afe ndipo wajitokeze kumwagia sifa lukuki.
"Naiomba serikali imsaidie mzee huyu, huwa naumia roho tunapokuwa tukipelekana klinini jinsi abiria ndani ya daladala wanavyotushangaa, najua ni kutokana na jina kubwa la Gurumo na hali aliyonayo kimaisha," alisema.
Aliongeza, ingelikuwa ni amri yake angependa kuona Gurumo akipumzika masuala ya muziki baada ya kuutumikia kwa zaidi ya miaka 50.

Mwisho

NB:Inawezekana Mzee Gurumo aliuzingatia ushauri huo wa mkewe na kuamua kupumzika muziki majuzi akitarajiwa kuagwa rasmi kwa matamasha ili kumchangia fedha za 'pensheni' yake katika muziki. MICHARAZO inamtakia kila la heri mkongwe huyo na Allah SW ampe siha, afya na umri mrefu zaidi Inshallah.

TFF yawazuia usajili wa wachezaji, kisa....!

Mombeki (kushoto) mmoja wa waliozuiliwa na TFF
Na Boniface Wambura
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imezuia usajili wa wachezaji 37 wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kutokana na usajili wao kuwa na kasoro.

Klabu husika zimetakiwa kurekebisha kasoro hizo kabla ya kuanza kuwatumia wachezaji hao kwenye mechi za VPL ambazo zinaanza leo (Agosti 24 mwaka huu) katika viwanja mbalimbali nchini.

JKT Ruvu Stars inatakiwa kuwafanyia uhamisho (transfer) wachezaji Salum Machaku Salum aliyekuwa Polisi Morogoro na Emmanuel Leonard Swita (Toto Africans). Mgambo Shooting inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Mohamed Hussein Neto (Toto Africans), Kulwa Said Manzi (Polisi Morogoro) na Mohamed Ally Samata (African Lyon).

Pia Salum Aziz Gilla anaonekana bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Coastal Union huku kukiwa hakuna vielelezo vyovyote kutoka kwa mchezaji mwenyewe, Coastal Union au Mgambo Shooting kama ulivunjwa au umenunulia na klabu anayotaka kuchezea msimu huu.

Tanzania Prisons inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji James Mjinja Magafu kutoka Toto Africans na Six Ally Mwasekaga (Majimaji). Nayo Coastal Union inatakiwa kumfanyia uhamisho mchezaji Kenneth Abeid Masumbuko kutoka Polisi Morogoro.


Kagera Sugar inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Suleiman Kibuta Rajab (Toto Africans), Godfrey Innocent Wambura (Abajalo), Eric Mulera Muliro (Toto Africans), Adam Juma Kingwande (African Lyon) na Peter Gideon Mutabuzi (Toto Africans).

Pia Kagera Sugar imepata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya mchezaji Kitagenda Hamis Bukenya, lakini bado hana kibali cha kufanyia kazi nchini (work permit).

Kwa upande wa Ruvu Shooting inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Abdul Juma Seif (African Lyon), Lambele Jerome Reuben (Ashanti United), Juma Seif Dion (African Lyon) na Cosmas Ader Lewis (African Lyon).

Oljoro JKT inatakiwa kumfanyia uhamisho mchezaji Tizzo Charles Chomba kutoka Polisi Morogoro, lakini imekataliwa kumsajili mchezaji Damas Mussa Kugesha wa Mlale JKT kwa kigezo kuwa ni askari na amehamishiwa Arusha kwa ajili ya mafunzo ya kijeshi. Kama Oljoro JKT inamtaka mchezaji huyo ni lazima ifuate taratibu za usajili kwa kumfanyia uhamisho kutoka Mlale JKT.

 Nayo Mtibwa Sugar inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Ally Shomari Sharrif (Polisi Morogoro), Salim Hassan Mbonde (Oljoro JKT U20) na Hassan Salum Mbande iliyemsajili kwenye kikosi chake cha U20 akitokea Oljoro JKT U20.

Ashanti United haiwezi kumtumia Said Maulid Kalikula aliyekuwa akicheza Angola kwa vile hajapata ITC. Nayo Rhino Rangers inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Ally Ahmad Mwanyiro (Mwadui FC), Laban David Kambole (Toto Africans) na Musa Boaz Chibwabwa (Villa Squad).

Klabu ya Simba inatakiwa kumfanyia uhamisho Betram Arcadi Mwombeki kutoka Pamba SC wakati wachezaji Gilbert John Kaze na Amisi Tambwe bado hawajapata ITC kutoka Burundi na hawana vibali vya kufanya kazi nchini. Mchezaji Joseph Owino tayari ITC imepatikana lakini hana kibali cha kufanya kazi nchini. Pia kipa Abel right Dhaila hana kibali cha kufanya kazi nchini.

Vilevile Simba inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji wawili iliyowasajili katika kikosi chake cha U20. Wachezaji hao ni Twaha Shekue Ibrahim kutoka Coastal Union 20 na Adeyun Saleh Seif (Oljoro JKT U20).

Nayo Yanga inatakiwa kumfanyia uhamisho mchezaji Rajabu Zahir Mohamed kutoka Mtibwa Sugar U20 wakati Hussein Omari Javu bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Mtibwa Sugar huku kukiwa hakuna vielelezo vyovyote kutoka kwa mchezaji mwenyewe, Mtibwa Sugar au Yanga kama mkataba huo ulivunjwa au umenunulia na klabu anayotaka kuchezea msimu huu.

Wachezaji waliosajiliwa kutoka nje ambao ITC zimefika na pia wana vibali vya kufanya kazi nchini ni Crispine Odula Wadenya kutoka Bandari ya Kenya na Yayo Wasajja Fred Lutimba kutoka URA ya Uganda waliojiunga na timu ya Coastal Union. Pia Mtanzania Hamis Thabit Nyige aliyejiunga na Yanga kutoka Ureno naye tayari na ITC.
Kwa mujibu wa kanuni, wachezaji wote wa ridhaa (wa madaraja ya chini ikiwemo Daraja la Kwanza) wanatakiwa kufanyiwa uhamisho (transfer) kwa klabu husika kujaza fomu za uhamisho na kulipia ada Chama cha Mpira wa Miguu cha Wilaya, Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa na TFF.
Pia TFF inakumbusha kuwa wachezaji wanaotajwa kuwa wamesajiliwa kama wachezaji huru (free agent) ni lazima waoneshwe kama huko walipokuwa mikataba imekwisha au la.

Yanga, Coastal, Ruvu zaua, Simba, Azam zang'ang'aniwa

Yanga iliyoanza kwa kishindo Dar

Ashanti United waliotunguliwa mabao 5-1

JKT Ruvu walioshinda ugenini jijini Tanga

Simba waliong'ang'aniwa na Rhino Rangers

Kagera Sugar waliotoshana nguvu na Mbeya City

JKT Oljoro walilala mabao 2-0 mbele ya Coastal Union
PAZIA la Ligi Kuu Tanzania Bara limefunguliwa jioni ya leo kwa kushuhudiwa mabingwa watetezi, Yanga kuikaribisha kwa kipigo cha aibu Ashanti Utd, huku watani zao Simba waking'ang'aniwa ugenini na 'wageni' wa ligi hiyo Rhino Rangers mjini Tabora.
Yanga ikiwa kwenye uwanja wa Taifa iliishindilia Ashanti kwa mabao 5-1, wakati Simba iliyokuwa ikiongoza kwa mabao 2-1 ilijikuta wakizembea na kulazimishwa sare ya 2-2 na Rhino.
Mabao ya Yanga katika mechi hiyo yalifungwa na Jerry Tegete aliyefunga mawili, Simon Msuva, Haruna Niyonzima na Nizar Khalfan.
Mjini Tabora kwenye uwanja wa Ali Hassani Mwinyi, Simba ilipata mabao yake kupitia Jonas Mkude, wakati Rhino walipanda daraja walipata mabao yao kupitia Imani Noel na Soud Kipanga.
Katika mechi nyingine Coastal Union ikiwa jijini Arusha ilionyesha ilivyopania msimu huu kwa kuilaza JKT Oljoro kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Abdul Banda kwa shuti la mita 40  na Mkenya Crispian Odulla.
Coastal walioshinda mabao 2-0
Nao Azam wakiwa ugenini Manungu kuumana na Mtibwa Sugar ililazimisha sare ya 1-1 wakisawazisha bao kwa mkwaju wa penati ya Aggrey Morris baada ya kutanguliwa kufungwa na Juma Liziwa.
Maafande wa JKT Ruvu wakiwa ugenini mjini Tanga waliishindilia Mgambo JKT kwa  mabao 2-0, huku Ruvu Shooting wakipata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Prisons Mbeya.
Nao wageni wengine wa ligi hiyo, Mbeya wakiwa nyumbani uwnaja wa Sokoine walilazimisa sare ya bila kufungana dhidi ya Kagera Sugar inayonolewa na Jackson Mayanja.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena siku ya jumatano kwa michezo kadhaa mabapo Simba itasafiri kuifuata Oljoro jijini Arusha, huku Ruvu ikielekea Mbeya kuwakabilia wenyeji wao Mbeya City.