Spika Anna Makinda |
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Anna Makinda ametoa rai kwa wanahabari na vyombo vya habari nchini kuacha kutumika kwani watakuwa wakwanza kulaumiwa iwapo nchi itaingia katika machafuko.
Makinda aliyasema hayo wakati akizungumza na wanahabari katika makaribisho ya Spika wa Korea Kusini Kang Chang Hee na ujumbe wake ambao wapo hapa nchini kwa mwaliko wa Bunge la Tanzania.
Alisema wapo wanahabari ambao wanakubali kutumiwa vibaya na wanasiasa wakiamini uandishi ndivyo unataka jambo ambalo amelikemea kwa nguvu zote.
Spika alisema ni vema vyombo vya habari na wanahabari kutumia nafasi yao kukosa Bunge na Serikali pale vinapoenda kinyume na maadili na kushindwa kutumikia wananchi ambao ndio waajiri wao wakubwa.
“Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba wanahabari na vyombo vyenu kukataa kutumiwa na wanasiasa pamoja na ukweli kuwa wapo ambao wanauhusiano na vyama mbalimbali ,” alisema.
Aliwataka kwa wale wanahabari wenye kuhitaji kushiriki siasa ni vyema wajiweke wazi kwani haipo sababu ya kuwa vibaraka wakati fursa ya wao kushiriki ipo wazi.
Aidha alivitaka vyama vya siasa kufanya siasa za haki na kuacha kutumbukiza chuki kwa wananchi kwa kile wanachoamini kuwa ndio njia ya kufikia malengo yao ya kisiasa.
Makinda alisema iwapo vyama vya siasa nchini vitadumisha siasa za ukweli ni dhahiri kuwa wananchi watakuwa na maamuzi sahihi bila kusukumwa na mtu yoyote.
Pia aliwataka wanasiasa kuacha kumchafua kwa kile ambacho wanasema kuwa amekuwa akipendelea hasa kwa wabunge wa chama chake jambo ambalo halina ukweli wowote.