STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, September 13, 2011

Fella akamilisha albamu ya 'Rusha Roho'




MENEJA wa kundi mahiri la muziki wa kizazi kipya nchini la TMK Wanaume Family, Said Fella 'Mkubwa Fella', amekamilisha albamu yake mpya na ya kwanza ya miondoko ya taarab akiipa jina la 'Kunguni' ikiwa na nyimbo sita.
Akizungumza na MIcharazo, Mkubwa Fella, alisema albamu hiyo ambayo nyimbo zake zimewashirikisha wasanii nyota wa muziki huo kama Khadija Kopa, Maua Tego na Isha Mashauzi itaachiwa rasmi mtaani mapema mwezi ujao.
Fella alisema katika kutaka kuitambulisha albamu hiyo ameshafyatua video ya wimbo wa Kusonona, atakayoiachia rasmi Ijumaa wiki hii.
"Nimekamilisha albamu yangu yenye nyimbo sita ambapo mmoja nimeufanyia video na ninatarajiwa kuanza kuusambaza kwenye vituo vya runinga Ijumaa ijayo," alisema.
Alivitaja vibao vya albamu hiyo ni 'Simuachi', 'Midomo Imewashuka', 'Mchakamchaka', 'Sijapopoa Dodo', 'Kimodern Modern' na 'Kusonona'.
Fella alisema ushirikiano aliofanya na wasanii wenye majina makubwa katika muziki huo utasaidia kuibeba albamu hiyo, iliyotangulishwa na kibao cha Midomo Imewashuka kinachoendelea kutamba kwenye vituo kadhaa vya redio nchini.

Mwisho

Extra Bongo 'kujinafasi' Kanda ya Ziwa



BENDI ya muziki wa dansi ya Extra Bongo 'Wazee wa Kujinafasi' inatarajia kuondoka jijini dar es salaam kuelekea mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria ya Mara na Mwanza ili kufanya maonyesho kadhaa ya burudani.
Meneja wa bendi hiyo, Mujibu Hamis alisema kuwa Extra Bongo itaondoka jijini Dar es Salaam kesho Alhamisi ambapo inatarajia kufanya onyesho la kwanza keshokutwa Ijumaa katika ukumbi wa Magereza, mjini Musoma mkoani Mara.
"Kama utakumbuka, ilikuwa tuanze ziara ya mikoa hiyo kabla ya kuanza kwa mfungo wa Ramadhan, lakini bahati mbaya kulitokea mambo ambayo yako juu ya uwezo wetu tukalazimika kuahirisha ziara yetu," alisema Mujibu.
Alisema kuwa kwa sasa kila kitu kiko sana na kwamba wanamuziki wake wako tayari kwenda kuwaburudisha wapenzi wa bendi hiyo wa miji ya Musoma na Mwanza ambako wamekuwa wakisubiriwa kwa hamu.
"Katika ziara hii tutamtambulisha mnenguaji wetu mpya, Aisha Madinda pamoja na nyimbo za albamu ya pili ambazo ni Neema, Mtenda Akitendewa, Watu na Falsafa, Bakutuka, Mama Shuu na Fisadi wa Mapenzi," alisema.
Alisema, kabla ya kuondoka kuelekea mkoani Mara, leo Jumatano watafanya vyao kwa ajili kuwaaga wapenzi wa bendi hiyo kwenye onyesho litakalofanyika katika ukumbi wa Masai uliopo Ilala Bungoni.
Extra Bongo ni bendi inayokuja kwa kasi kwenye angaza za muziki wa dansi ikiwa na albamu ya kwanza ya 'Mjini Mipango' ambayo nyimbo zake 'Wema','Maisha Taiti', 'Laptop', 'First Lady' na 'Safari ya Maisha'.

Hammer Q aibuka Eagle Modern taarab



MUIMBAJI nyota wa muziki wa taarab nchini, Husseni Mohammed 'Hammer Q' ameanzisha kundi jipya la miondoko hilo, liitwalo Eagle Modern Taarab 'Wana Kimanumanu' likiwa limeshaachia nyimbo mbili mpya za kulitambulisha.
Akizungumza na Micharazo, Hammer Q, alisema kundi hilo linaloundwa na wasanii 16, linajiandaa kukamilisha albamu yao ya kwanza itakayokuwa na nyimbo tano, mbili kati ya hizo zimerekodiwa video na zimeshasambazwa ili virushwe hewani.
Hammer Q aliyekuwa Five Star baada ya awali kulitema kundi la Dar Modern Taarab, alizitaja nyimbo zilizorekodiwa audio na video kwa ajili ya kulitambulisha kabla ya kuanza kufanya maonyesho yake ni Tatu Bila na Zangu Dua.
"Baada ya kimya kirefu, nimeibuka nikiwa na kundi jipya la taarab liitwalo 'Eagle Modern Taarab na tayari tumeshakamilisha nyimbo mbili kati ya tano tunazoandaa kwa ajili ya albamu yetu ya kwanza," alisema Hammer Q.
Nyota huyo aliyetamba na vibao kama Pembe la Ng'ombe na Kitu Mapenzi akiwa Dar Modern, alisema kundi lao lina wasanii 16 baadhi yao wakiwa ni wale aliokuwa nao kundi la Dar Modern kama Latifa Salum, Ramadhani Kisolo na Aisha Athuman.
Wengine wanaounda kundi hilo jipya lililokua wiki chache tangu kuanzishwa kwa kundi jingine la Tanzania Moto Taarab ni; Mwanaidi Ramadhani, Asma Ally, Mohammed Mzaka na wengineo waliopo kambini wakijiandaa na kujitambulisha rasmi kwa mashabiki wa miondoko hiyo.
Hammer Q, alisema tayari nyimbo tano za albamu yao zimekamilika na kuzitaja majina yake na waimbaji wake kuwa ni; 'Tatu Bila'-Hammer Q, 'Zangu Dua'-Latifa Salum, 'Kunyamaza Kwangu'- Mwanaidi Ramadhani, 'Siri ya Mungu'-Aisha Athuman na 'Mapenzi ya Dhati'-Asma.