STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, March 20, 2013

Morocco kutua nchini Ijumaa bila Chamack

Kikosi cha timu ya Morocco

Na Boniface Wambura
TIMU ya soka ya Taifa ya Morocco (Lions of the Atlas) inatarajiwa kuwasili nchini keshokutwa Ijumaa kwa ndege ya Emirates tayari kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Tanzania (Taifa Stars) itakayochezwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Msafara wa timu hiyo yenye watu 58 wakiwemo maofisa 19 na waandishi wa habari 12 utawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 8.55 mchana na utafikia hoteli ya Kilimanjaro Hyatt Regency.

Siku hiyo Morocco inatarajia kufanya mazoezi jioni kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, na Jumamosi itafanya mazoezi yake ya mwisho kwenye Uwanja wa Taifa kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa saa 9 kamili alasiri.

Wachezaji walioko kwenye kikosi hicho chini ya Kocha Rachid Taoussi ni Nadir Lamyaghri, Anas Zniti, Yassine Bounou, Younnes Bellakhadar, Abdellatif Noussair, Abderrahim Achchakir, Zoheir Feddal, Younnes Hammal, Zakarya Bergdich na Abdeljalil Jbira.

Issam El Adou, Kamel Chafni, Salaheddine Saidi, Mohamed Ali Bamaamar, Abdelaziz Barrada, Salaheddine Aqqal, Abdessamad El Moubarky, Nordin Amrabat, Chahir Belghazouani, Abdelilah Hafidi, Youssef Kaddioui, Brahim El Bahri, Hamza Abourazzouk na Youssef El Arabi.

Wakati huo huo, tiketi kwa ajili ya mechi hiyo zitaanza kuuzwa keshokutwa katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Uwanja wa Taifa na Dar Live Mbagala.

Milango siku ya mechi kwa ajili ya watazamaji itafunguliwa saa 6 kamili mchana.

Kibwende cha Kazi chatoka


MCHEKESHAJI anayetamba na filamu kadhaa za komedi, Kazi Seleman 'Kazi' ameachia wimbo mpya wa muziki wa kizazi kipya uitwao 'Kibwende' alioimba na wasanii wenzake wa 'Vituko Show', Man Bizzo na Tausi.
Kazi, msanii mwenye umbile dogo alisema wimbo huo ameurekodi mjini Tanga na anatarajia kuanza kuusambaza ili urushwe hewani wakati akijiandaa kurudi tena studio kufyatua mwingine akimshirikisha nyota, Prince Dully Sykes.
Msanii huyo aliutaja wimbo huo anaojiandaa kuurekodi kuwa ni 'Mateso' utakaokuwa katika miondoko mchanganyiko ya Kwaito na Rhumba.
"Nimekamilisha wimbo wangu mpya uitwao 'Kibwende' nilioimba na 'swahiba' yangu Man Bizzo na Tausi, wakati pia najiandaa kurudi studio kurekodi kazi nyingine ambayo nimepanga kuimba na Dully Sykes," alisema Kazi

KR Mullah ana wivu kwa masela



NYOTA wa muziki wa kizazi kipya kutoka kundi la Wanaume Halisi, Rashidi Ziada maarufu kama KR Mullah, amesema anajiandaa kutoa nyimbo zake mbili binafsi ziitwazo 'Wivu' na 'Masela na Machizi'.
Akizungumza na MICHARAZO, KR alisema amemaliza kuzifanyia mazoezi nyimbo hizo na zitarekodiwa baada ya kiongozi wao wa kundi la Wanaume Halisi, Sir Juma Nature, atakapomaliza uzinduzi wa albamu yake binafsi.
KR Mullah ambaye pia ni mwanasoka, alisema ndani ya kundi lao wamewekeana utaratibu wa kila mwanakundi kutoa kazi binafsi na kwa sasa ni zamu ya Nature kisha itafuata yake.
"Natarajia kuvunja ukimya tangu nilipoachia wimbo wa 'Choo cha Kike' kwa kutoa nyimbo mbili za 'Wivu' na 'Masela na Machizi', ambazo zimekamilika mashairi yake isipokuwa nasubiri kuzipeleka studio baada ya Nature kutoka," alisema.
Mkali huyo, mmoja wa waasisi wa kundi la TMK Wanaume Halisi 'Mapanga Shaa' alisema imani yake ni kwamba nyimbo hizo zitarejesha heshima aliyopata kupitia kazi zake za awali ukiwamo wa 'Kamua kwa Uwezo'.
"Kwa wanaonifahamu nadhani wanajua namaanisha nini ninapowaambia wajiandae kupata burudani kutoka kwangu, ila kifupi ni kwamba 'Wivu' na 'Masela na Machizi' zitakuwa zaidi ya burudani," alisema.

BIBI CHEKA SASA ANALIA, KISA...!

Bibi Cheka (kulia) akiwa na Fella

BAADA ya kutambulishwa vyema na nyimbo zake mbili za 'Ni Wewe' alioimba na Mheshimiwa Temba na 'Good Baba Fella' aliomshirikisha rapa Godzilla, msanii mwenye umri mkubwa, Cheka Hijja 'Bibi Cheka' amefyatua wimbo mpya uitwao 'Nalia'.
Akizungumza na MICHARAZO, meneja wa msanii huyo, Said Fella alisema wimbo huo pamoja na video yake imekamilika wiki iliyopita na unatarajiwa kuachiwa rasmi kwa mashabiki leo Jumatano.
Fella alisema Bibi Cheka anayetokea katika kituo chake cha Mkubwa na Wanawe, safari hii ametoa kazi hiyo akiimba yeye peke yake tofauti na 'ngoma' zake za awali ambazo zinaendelea kutamba.
Alisema wimbo huo ni wa tatu kwa msanii huyo anayeshikilia rekodi ya kuwa msanii mzee zaidi kuimba nyimbo za vijana.
Katika hatua nyingine, Fella alisema wimbo wao mpya wa 'Bendera' ulioimbwa na wasanii kadhaa wa Mkubwa na Wanawe, umeshasambazwa na kuanza kusikika hewani wakati wakijiandaa kutoa video yake.
"Tayari tumeshausambaza wimbo wa 'Bendera' na umeanza kusikika hewani. Sasa tunajiandaa kurekodi video yake mara baada ya kumalizika kwa Pasaka," alisema Fella

Simba yainyuka CDA, leo kuikabili Singida Utd


SIMBA ilipata ushindi wa bao 1-0 juzi katika mechi yao ya kirafiki dhidi ya CDA ya Dodoma na leo inatarajia kushuka tena dimbani kwenye uwanja wa Namfua mkoani Singida kuikabili Singida United.
Bao pekee la Simba katika mechi yao dhidi ya CDA kwenye Uwanja wa Jamhuri lilifungwa katika kipindi cha kwanza na winga wao Kigi Makasi.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Pamba, ambaye yuko na timu katika safari yao itakayowafikisha hadi Bukoba mkoani Kagera, aliliambia gazeti hili jana kwamba  wameshatua Singida na wachezaji wote wako katika hali nzuri.
Pamba alisema kwamba bado kikosi hicho kiko chini ya uongozi wa mwenyekiti Ismail Aden Rage, na hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanyika kama ilivyotangazwa na baadhi ya wanachama waliokutana Jumapili na kudai wamewang'oa madarakani viongozi halali waliopo.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wanatumia mechi hizo za kirafiki kuiandaa timu yao kabla ya kukutana na Kagera Sugar katika mechi ya ligi kuu itakayochezwa Machi 27 kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.
Baada ya mechi yao dhidi ya Kagera, Simba itaelekea Mwanza kuivaa Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, mechi itakayochezwa Machi 30.


CHANZO: NIPASHE

Kocha Polisi Tabora achekelea kuiokoa timu


KOCHA wa timu ya soka ya Polisi Tabora, Mwinyimadi Tambaza amesema amefurahishwa kufanikiwa kuiokoa timu yake iliyokuwa katika hali mbaya na kusalia kwenye Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.
Polisi Tabora iliyomaliza duru la kwanza la ligi hiyo ikiwa na pointi tatu tu imenusurika kushuka daraja baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Pamba ya Mwanza katika mechi yao ya kufungia msimu wa ligi hiyo.
Ushindi huo uliifanya timu hiyo kuweza kuokoka kuteremka daraja na kuiacha Morani ikiungana na timu nyingine mbili ikiwamo Moro United na Small Kids kushuka hadi Ligi Daraja la Pili.
Akizungumza na MICHARAZO juzi, Tambaza alisema anashukuru vijana wake kutekeleza kila alichokuwa akiwafundisha na kujituma uwanjani kiasi cha kuiwezesha kuiokoa Polisi kutoshuka daraja kwa hali mbaya iliyokuwa nayo.
Kocha huyo alisema mafanikio aliyoyapata kwa kuweza kuisaidia Polisi kuvuna pointi 15 katika duru la pili ni furaha kwake kwa vile ameweza kutimiza ahadi yake ya kuiokoa timu hiyo isishuke daraja.
"Wakati nikiitwa kuja kuinoa Polisi ilikuwa katika hali mbaya, ila nilijipa moyo nikijiamini kwa uwezo niliokuwa nao kwa kuahidi nitapigana kufa na kupona kuiokoa iishuke daraja na imekuwa kweli ni faraja kwangu," alisema.
Alisema baada ya kuinusuru timu hiyo anafanya utaratibu wa kuwasilisha ripoti na mapendekezo yake kwa mabosi wake ili waanze kujipanga mapema kwa ajili ya msimu ujao akiwa na ndoto na kuipandisha Ligi Kuu Tanzania Bara.

TWIGA STARS FULL DISPLINE CHINI YA KAIJAGE






WACHEZAJI wa timu ya soka ya taifa ya wanawake 'Twiga Stars' wamemgwaya kocha wao mpya, Rogasian Kaijage kwa kuanza kutii masharti yake ikiwemo suala la nidhamu.
Wachezaji hao ambao walikuwa wanakata nywele kwa staili za ajabu na uvaaji wa surulia na pensi kwa staili ya mlegezo wameonekana kubadilika baada ya kuwa na kocha huyo mpya.
Kaijage ambaye amerithi mikoba ya Boniface Mkwasa baada ya kubwaga manyanga mwaka jana alipoita timu hiyo alikaa nao kikao na kuwaeleza kuwa hatapenda kuona wachezaji hao wakivaa staili ambazo zinaleta picha mbaya kwa jamii.
“Niliwaambia mpira unahitaji uwe na adabu ili ufanikiwe hivyo niwaambia wabadilike kuanzia muonekana hadi uwanjani na ndio maana unawaoneka wamesuka vizuri na kubana nywele vizuri na kuvaa nguo sawasawa”, alisema Kaijage
Mashabiki wa soka walishuhudia wachezaji wakiwa nadhifu kuanzia kwenye mavazi hadi kichwani na wakifanya mazoezi kwa ari na kocha anapoita timu kila mtu anakimbia kuwahi kufika siyo kutembea wala utani ambao hauna tija.
Naye meneja wa timu hiyo Furaha Francis amefurahishwa na kitendo cha kocha kuwaeleza ukweli wachezaji kuwa nidhamu inaanzia kwenye muonekano kwa jamii.

Star Boy ajifua kumkabili Yusuf Jibaba



BONDIA Shabani Mhamila 'Star Boy' ameingia kambini kujiandaa 

kumkabili Yusuf Jibaba katika pambano la utangulizi wakati wa
mchezo wa kati ya Francis Cheka na Thomas Mashali.
Pambano hilo la raundi nne linatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa PTA Sabasaba, Dar es Salaam Mei Mosi mwaka huu, linatarajiwa kuwa la vuta nikuvute kutokana na kila mmoja kujigamba kujiandaa vema.
Kocha wa Star Boy, Habibu Kinyogoli 'Master' akisaidiwa na  Rajabu Mhamila 'Super D' wamesema kuwa bondia wao ameingia kambini juzi kujiandaa kumchakaza Jibaba ili
kuendelea kujiwekea sifa nzuri.
"Bondia wangu yuko katika maandalizi ya kutosha kuhakikisha anafanya vizuri katika pambano hilo la utangulizi kati ya Cheka na  Mashali" alisema Super D na kuongeza Star Boy alishawahi kuwa
bingwa wa masumbwi mwaka 1998.
Hata hivuo aliamua kusimama kwa muda kucheza ngumi na kwa sasa amerejea ulingoni ili atoe changamoto za mchezo huo.
Bondia huyo mwenye rekodi ya kucheza mapambano 23 akishinda 14 (5 KO) kupoteza 7 na kupata sare mbili.
Super D, kocha huyo wa kimataifa wa mchezo wa ngumi nchini, alisema kuwa katika mchezo huo kutakuwa na DVD za mafunzo ya mchezo huo zenye mapambano makubwa ya mabondia wa ndani na nje ya nchi. 
DVD hizo zinahusisha mapambano ya Kalama Nyilawila dhidi ya Francis Cheka, Mbwana Matumla na Francis Miyeyusho, Said Mundi na King Class Mawe.