STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, May 17, 2012

MASKINI PATRICK MUTESA MAFISANGO!

KIFO kina usiri mkubwa na hakuna ajuae ila Mwenyezi Mungu! Ndio kauli inayoweza kuanza nayo kutokana na ukweli ni saa chache tu, tangu kiungo mahiri wa Simba, Patrick Mafisango kuitwa kwa mara ya kwanza baada ya kitambo kirefu kuwa nje ya kikosi cha timu ya taifa ya Rwanda 'Amavubi'. Mafisango aliyefariki alfajiri ya leo kwa ajali ya gari, alikuwa miongoni mwa wachezaji 32 walioitwa na kocha wa timu ya taifa ya Rwanda, Milutin 'Micho' Sredojovic kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya kuwania Fainali za Afrika za 2013 na Kombe la Dunia za 2014. Kitambo kirefu marehemu Mafisango alikuwa hajajumuishwa katika timu hiyo kutokana na tatizo la utovu wa nidhamu, lakini kwa kiwango alichokionyesha kwa siku za karibuni akiwa na klabu ya Simba, Micho alishawishika kumuita katika timu hiyo. Hata hivyo, wakati akiwa anajiandaa kwenda Rwanda kujiunga na kambi ya timu hiyo kwa ajili ya michezo yao miwili ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu za Libya na Tunisia ambazo zimepangwa kucheza Mei 25 na 26. Wengine walioitwa katika kikosi hicho ni nahodha wa zamani, Hamad Ndikumana, aliyekuwa ametemwa muda mrefu, Hamdan Bariyanga, Olivier Kwizera na Francois Hakizimana na Haruna Niyonzima anayeichezea Yanga. Kwa hakika ni pigo kwa Amavubi, Simba na familia nzima ya mchezaji huyo ambaye alikuwa miongoni mwa wafungaji walioisaidia Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kufika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho. Marehemu Patrick Mutesa Mafisango alizaliwa Machi 09, 1980
Innalillah Wainailahi Rajiun!

Azam itafanya maajabu Afrika-Nahodha

NAHODHA wa klabu ya soka ya Azam, Aggrey Morris, amesema ana imani timu yao itafanya maajabu katika ushiriki wao wa michuano ya kimataifa. Morris, alisema japo Azam wataiwakilisha nchi kwa mara ya kwanza, bado anaamini kwa namna uongozi wao ulivyojizatiti na kujipanga tangu ilipopanda daraja, timu yao itafika kule iliposhindwa wawakilishi wengine Beki huyo wa kati anayezichezea pia timu za taifa za Zanzibar na Taifa Stars, alisema aina ya wachezaji waliopo Azam na benchi la ufundi chini ya kocha Stewart John Hall, linampa jeuri ya kuamini timu yake itatisha Afrika. "Awali ya yote tunashukuru kwa kuweza kupata nafasi hiyo ya kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa mwakani, lakini pia nataka kuwatia moyo wadau wa soka kwamba Azam haitawaangusha Afrika," alisema. Alisema, japo wachezaji karibu wote wa Azam kwa sasa wapo mapumzikoni, lakini akili zao zipo katika michuano hiyo ya Afrika. Kwa kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam imepata fursa ya kuiwakilisha Tanznaia katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa ni mara yao ya kwanza tangu timu hiyo ianzishwe mwaka 2004.

Cheka ajipanga kumtoa nishai Mzambia

BINGWA mpya wa IBF Afrika, Francis Cheka 'SMG' ametamba kwamba hatawangusha Watanzania katika pambano lake la kutetea taji hilo dhidi ya Mzambia, Stephen Chungu atayepigana nae Julai mwaka huu. Cheka, alisema kwa kutambua umuhimu wa pambano hilo anatarajia kuingia kambini mapema zaidi ili kujiweka fiti kabla ya kuvaana na Chungu katika pambano la uzani wa Super Middle la raundi 12. Awali Cheka alikuwa apambane na Mohammed Akpong wa Ghana, lakini kutokana na masharti aliyoyatoa bondia huyo, imemfanya waratibu wa IBF kumbadilishia Mzambia huyo mwenye rekodi ya kucheza michezo 16. "SItaki kuwaangusha Watanzania na hivyo nitaanza mapema kambi yangu ili kumkabili nikiwa fiti na kuhakikisha napata ushindi hiyo Julai," alisema. Cheka anayeshikilia pia mataji ya Kamisheni ya Ngumi Dunia, WBC, ICB na UBO, alisema ushindi wake dhidi ya Mada Maugo uliomfanya atwae taji hilo la IBF Afrika imekuwa kama chachu ya kuzidi kusaka mafanikio kimataifa. "Akili yangu kwa sasa ni kusaka mafanikio zaidi duniani, ndio maana sitaki kufanya uzembe wa aina yoyote katika pambano langu lijalo na mengine ya kimataifa ambayo ndiyo yenye ulaji mkubwa," alisema. Cheka alitwaa taji hilo kwa kumshinda Mada Maugo aliyekacha ulingo wakati wakijiandaa kwa raundi ya saba kwa kile alichodai alikuwa akiona 'kiza' na kumfanya bingwa huo wa IBF kushinda pambano la 11 mfululizo tangu 2008. Mwisho

Messi wa Simba achekelewa kuitwa Taifa Stars

MSHAMBULIAJI nyota kinda la klabu ya Simba, Ramadhani Singano 'Messi' amesema hakuamini kirahisi alipolisikia jina lake likitajwa na kocha mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Kim Poulsen kujiunga na kikosi cha timu hiyo. Akizungumza na MICHARAZO nyumbani kwao, Keko Machungwa jijini Dar es Salaam, Messi, alisema mara alipojithibitisha kwamba ni kweli ni miongoni mwa wachezaji wa timu hiyo aliporomoka hadi chini kumsujudia Mola wake. Mchezaji huyo aliyetamba na timu za Ubatan na Bombom kabla ya kuonwa na Simba, alisema kifupi ni kwamba amefurahia uteuzi huo akiamini kocha Poulsen amekiona kipaji chake na wajibu wake kutomuangusha. "Kwa kweli sikuamini kama ni mimi niliyetajwa katika kikosi hicho, ila ndugu zangu waliponithibitishia cha kwanza nilichofanya ni kusujudu kumshukuru Mungu kwani nimefurahi kupata fursa hii na sitamuangusha kocha," alisema. Alisema mbali na kujitahidi kwa uwezo wake wote kuonyesha fadhila kwa kocha Kim, pia asingependa kuwaangusha Watanzania ambao wamekuwa na matumaini makubwa na timu yao licha ya kushindwa kuwapa raha. "Ninachoomba nipate nafasi ya kuonyesha uwezo wangu kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu ili kuweza kuisaidia timu ifanye vema na kusuuza roho za watanzania wenye wazimu wa soka," alisema Messi. Messi, aliyepandishwa kikosi cha kwanza cha Simba kitokea timu B ya klabu hiyo hiyo ni mara yake ya kwanza kuitwa Stars, ingawa tangu mwaka 2009 amekuwa akizichezea timu za taifa za vijana U17 na U20. Mchezaji huyo ni kati ya wachezaji 25 walioteuliwa na kocha Poulsen kwa ajili ya kujiandaa na mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia na zile za Afrika zitakazofanyika kati ya mwaka kesho na 2014.
KIPA nyota wa zamani wa timu za Simba na Yanga, Doyo Moke, amesema umefika wakati wa wadau wa soka nchini kuwapa nafasi wachezaji wa zamani kuziongoza klabu za soka badala ya kuwaachia 'wavamizi' wanaziyumbisha. Moke, aliyewahi kung'ara pia na timu za Majimaji-Songea, Rayon Sports ya Rwanda na Vital'O ya Burundi, alisema watu wasio na uchungu waliovamia mchezo huo ndio wanaolifanya soka la Tanzania kushindwa kusonga mbele. Alisema, dhana kwamba lazima kiongozi wa soka awe na elimu ya Chuo Kikuu, imechangia kudumaza soka la Bongo kwa vile wengi wa wasomi hao wamekuwa akizitumia klabu wa masilahi yao ikiwemo kupata umaarufu. "Lazima watanzania wabadilike kwa kutoa nafasi kwa wachezaji wa zamani kuweza kuongoza soka la Tanzania, mataifa mengine yamefanya hivyo na kufanikiwa, kwa kuwa wachezaji huwa na uchungu wa kweli na soka," alisema. "Wengi wanaojitokeza sasa kuongoza klabu ni wavamizi wasiokuwa na uchungu na mchezo huo zaidi ya kujitafutia umaarufu ili waende kugombea nafasi za uongozi wa kisiasa na kujinufaisha kimasilahi wenyewe," aliongeza. Alisema, ingawa elimu ni kitu cha muhimu katika uongozi, lakini basi nafasi hizo wapewe wachezaji wenye elimu za kutosha kuweza kuongoza gurudumu la soka kama ilivyotokea kwa akina Leodger Tenga, Mtemi Ramadhani na wengineo ambao wameonyesha uwezo mkubwa na ufanisi wa hali ya juu. Kuhusu kinachoendelea kwenye klabu yake ya zamani ya Yanga, Moke mwenye asili ya Jamhuri wa KIdemokrasia ya Kongo, alisema ni lazima pande zinazolumbana zikae chini na kumaliza tofauti zao ili kuinusuru klabu yao. "Kulumbana hakuwezi kukusaidia wakati wana kibarua kigumu katika utetezi wao wa Kombe la Kagame, wakizembea hata taji hilo litapotea hivihivi," alisema. Tangu wafungwe mabao 5-0 na watani zao Simba na kulipoteza taji la Ligi Kuu Tanzania Bara, hali ndani ya klabu ya Yanga imekuwa si shwari ambapo wanachama na wazee wakilumbana na uongozi wao chini ya Mwenyekiti Llyod Nchunga. Mwisho

Patrick Mutesa Mafisango afariki kwa ajali ya gari

KIUNGO mahiri wa klabu ya soka ya Simba, Patrick Mutesa Mafisango "petit' amefariki dunia alfajiri ya leo baada ya kupata ajali ya gari jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa taarifa ambazo MICHARAZO imezipata na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo ya Simba, Ismail Aden Rage, Mafisango aliyekuwa mmoja wa wachezaji tegemeo wa klabu hiyo katika ushiriki wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya Kombe la Shirikisho alifariki majira ya saa 10 akitokea klabu kujirusha. Imeelezwa kwamba, mchezaji huyo kutokla Rwanda, ingawa asili yake ni Jamhuri ya KIdeomkrasia ya Watu wa Kongo, alifariki wakati akitoka kujirusha klabu usiku na alipatwa na ajali hiyo maeneo ya TAZARA wakati akijaribu kumkwepa mwendesha Bodaboda na kujikuta wakiporomokea mtaroni na gari lake ambalo lilikuwa na watu wengine wawili. Watu hao wametajwa kuwa ni rafiki ya kiungo huyo mshambuliaji na mdogo wake ambao hata hivyo majina yake hayakuweza kupatikana mara moja. Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage, alisema yeye alipata taarifa na wakati akizungumza na blog hii alikuwa akiendelea kufanya mchakato wa msiba wa mchezaji wake huyo ambaye walimchukua kutoka Azam Fc. Kabla ya kutua Azam na kuonyesha uwezo mkubwa, Mafisango aliyezaliwa Machi 09, 1980 alikuwa akikipiga katika klabu ya ya nchini kwake APR ya Rwanda. Mafisango anakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika klabu hiyo akiifungia jumla ya mabao 11 katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ambapo Simba imetwaa taji ikiwapoka watani zao Yanga. Pia alikuwa mmoja wa wafungaji walioisaidia Simba kufika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho kabla ya kutolewa na Al Ahly Shandy ya Sudan,ambapo alikosa mkwaju wake wa penati uliosababisha Simba kung'olewa kwa jumla ya mabao 12-11. Mungu aipumzishe kwa amani roho ya marehemu Patrick Mutesa mafisango Amin!

Super Nywamwela sasa aibuka na Ndungwe

DANSA kiongozi wa bendi ya Extra Bongo, Hassani Mussa 'Super Nyamwela' amefyatua kibao kipya kiitwacho 'Ndungwe'akiwa katika maandalizi ya kukamilisha albamu yake ya tatu. Akizungumza na MICHARAZO, Nyamwela alisema kibao hicho kilichopo katika miondoko ya Bongofleva, amekifyatulia katika studio za AM Records chini ya prodyuza 'Maneke. Nyamwela alisema huo ni wimbo wa pili kuurekodi kwa mwaka huu baada ya awali kupakua Tumechete, alichowashirikisha 'bosi' wake, Ally Choki, Banza Stone na Athanas Montanabe. "Nimeachia wimbo mpya wa Ndungwe, nilioimba pekee yangu katika kuwaonmyesha mashabiki wangu kwamba naweza miondoko yote, kwani wimbi huu nimeutoa katika miondoko ya Bongofleva," alisema. Nyamwela alisema, kwa sasa anafanya mipango ya kurekodi video ya wimbo huo, ili mashabiki wake wapate burudani, huku akiendelea kumalizia nyimbo nyingine za kukamilisha albamu yake ya tatu binafsi. Albamu mbili za awali za bingwa huyo wa zamani wa Bolingo mkoa wa Dar es Salaam ni 'Master of the Tample' na 'Afrika Kilomondo'.
Super Nyamwela akionjesha manjonjo yake katika mazoezi ya bendi yake ya Extra Bongo