MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu, Simba jana waliendelea kutakata kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuitandika Prisons ya Mbeya mabao 2-0 na kurejea kileleni wakiiondosha Azam Fc iliyowaengua kwa saa kadhaa.
Bao la kwanza la Mrisho Ngassa kwa timu hiyo ndilo lililoipa Simba ushindi iliyomaliza mechi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa wachezaji tisa uwanjani.
Kwa ushindi huo, Simba imeendelea kuwa timu pekee yenye matokeo ya asilimia 100 baada ya raundi nne, ikiwa na pointi 12, mbili juu ya Azam, katika pambano lililohudhuriwa na watazamaji wachache kuliko kawaida ya mechi za mabingwa watetezi hao.
Coastal Union ni ya tatu ikiwa na pointi nane, tatu juu ya Prisons ambayo imeshuka kwa nafasi moja mpaka kuwa timu ya tano nyuma ya JKT Oljoro kwa uwiano wa mabao, zote zikiwa na pointi tano baada ya michezo minne.
Siku iliisha vibaya kwa Simba baaada ya beki wake Amiri Maftaha kuonyeshwa kadi nyekundu na muamuzi Paul Soleji dakika mbili kabla ya filimbi ya miwsho, baada ya kumchezea rafu mbaya Khalid Fupi.
Siku ilianza vibaya pia kwa Simba baada ya Lugano Mwangama kuipatia Prisons bao la kuongoza katika dakika ya saba tu ya mchezo kwa shuti kali ambalo lilimbabatiza beki Juma Nyoso wa Simba kabla ya kutinga wavuni, kwenye Uwanja wa Taifa.
Iliichukua Simba kipindi kizima cha kwanza kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Felix Sunzu katika dakika ya 45 akiunganisha krosi ya Mwinyi Kazimoto.
Kama alivyomalizia ngwe ya kwanza, Sunzu angeweza kuongeza idadi ya mabao ya Simba dakika tatu tangu kuanza kwa kipindi cha pili lakini shuti lake kutokana na pasi ya Mrisho Ngassa lilipaa juu.
Ndipo Ngassa alipochukua jukumu la kusahihisha kosa hilo mwenyewe dakika saba baadaye kwa shuti lililomshinda David Abdallah kuzuia katika lango la Prisons, akiunganisha krosi ya Said Nassoro.
Simba iliwatoa Amri Kiemba na nafasi yake kuchukuliwa na Salim Kinje, Ramadhani Chombo aliyempisha Jonas Mkude na Edward Christopher kwa Daniel Akuffor baada ya goli la Ngassa ikiwa ni jitihada za kutawala zaidi mechi hiyo, lakini hapakuwa na goli la ziada.
Kocha wa Simba Milovan Circovic alisema timu yake ilipata ushindi kutokana na kucheza vizuri, na akasikitikia athari za kadi nyekundu ya Maftah ingawa alisema kuna wachezaji wa kuziba pengo lake.
Timu zilikuwa:
SIMBA: Juma Kaseja, Nassoro Masoud, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Juma Nyoso, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba (Salim Kinje dk.74), Ramadhani Chombo (Jonas Mkude dk.67), Edward Christopher (Daniel Akuffor dk.76), Felix Sunzu, Mrisho Ngassa.
PRISONS: David Abdallah, Aziz Sibo, Laurian Mpalile, Lugano Mwangama, David Mwantika, Khalid Fupi, Misango Magai, Fred Chudu, Elias Maguri, Peter Michael (Sino Agustino dk.67), John Matei.
Wachezaji wa Simba wakishangilia bao la kwanza lililofungwa na Felix Sunzu (kulia)
Mashabiki wa Simba wakishangilia
Mshambuliaji wa Simba, mrisho Ngasa akichuana na nahodha wa Tanzania Prisons, Lugano Mwangama
Golikipa wa Prisons, David Abdallah akiokoa hatari langoni mwake
Wachezahi wa Prisons ya Mbeya wakiongozwa na kipa wao kuomba dua wakati wa mapumziko