STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, December 30, 2011

PICHA KALI YA MWAKA 2011


UTAJAZA MWENYEWE!

NENO LA KUUAGA MWAKA 2011




MUNGU AMETUWEZESHA KUVUKA MILIMA NA MABONDE YA MWAKA 2011 NA HUENDA AKATUJALIA KUMALIZA KILICHOBAKIA NDANI YA MWAKA HUU NA KUKARIBISHA MWAKA MPYA WA 2012. KITU CHA MUHIMU NI KUJIULIZA KIPI TUNACHOWEZA KUMLIPA MUNGU KWA WEMA NA UKARIMU ALIOTUFANYIA KIPINDI CHOTE CHA MAISHA YETU. NADHANI KIKUBWA TUNACHOPASWA KUFANYA NI KUMSHUKURU NA KUZIDI KUMTII NA KUMNYENYEKEA KUSUDI AZIDI KUTUPA MEMA ZAIDI. MICHARAZO MITUPU INAWATAKIA KILA LA HERI KATIKA KUUAGA MWAKA 2011 NA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA WA 2012.

Fella aahidi makubwa 2012



MENEJA wa kundi la TMK Wanaume Family, Said Fella amesema mwaka 2011 kwake umekuwa wa mafanikio, ikiwemo kuwakusanya vijana chipukizi 37 aliwatoa mmoja baada ya mwingine katika anga la muziki Tanzania.
Pia, alisema kumiliki studio binafsi na kuliendeleza kundi la TMK Wanaume Family linalokaribia umri wa miaka 10 tangu kuanzishwa kwake na kufyatua albamu katika miondoko ya taarabu ni vitu vingine vinavyomfanya atembee kifua mbele.
Akizungumza na MICHARAZO, Fella alisema kama kuna mwaka uliokuwa wa neema kwake na kujivunia ni huu unaomalizika leo usiku, kutokana na kufanya mambo makubwa yanayomfanya aufurahie.
Alisema kuunda kundi lenye vijana 37 wenye vipaji mbalimbali na kuwasaidia kuwatoa mmoja baada ya mwingine kama alivyofanya kwa Aslay Is'haka 'Dogo Asley', Mugogo anayetamba na kibao cha 'Jicho Chongo' na wengineo.
"Nadhani kwa mwaka 2012 kwa uwezo wa Allah, nitaendelea kuwatoa vijana chipukizi kama nilivyoweza kufanya ndani ya mwaka huu," alisema.
Fella, alisema pamoja na kuendelea kuwatoa chipukizi, mipango yake ni kuona TMK linatamba nchini, huku akifyatua vitu vikali zaidi kupitia studio yake ya Poteza Records na kuupeleka mbele muziki wa kizazi kipya na sanaa kwa ujumla.
"Kuna mengi niliyoyapanga kuyafanya mwaka ujao, lakini cha muhimu ni Mungu kuniwezesha na kunipa afya njema kuyafanikisha, ila lazima nishukuru kwamba 2011 ulikuwa ni mwaka mzuri kwangu," alisema Fella.
Mwisho

Msondo kuuona mwaka Dar



WAKATI wapinzani wao wa jadi wakilikimbia jiji na kwenda kuukaribisha mwaka mpya jijini Mwanza, bendi ya Msondo Ngoma, yenyewe imejichimbia Dar ikiendelea kutambulisha nyimbo mpya zinazoandaliwa kwa albamu ijayo.
Msemaji wa Msondo Ngoma, Rajabu Mhamila 'Super D', alisema bendi yao imeamua kuwapa burudani mashabiki wa Dar kwa kufanya maonyesho yao ya mwishoni mwa wiki katika kumbi zao zilizozoeleka.
Alisema leo bendi yao itafanya mambo yake kwenye ukumbi wa Leaders Club, kabla ya kesho kutambulisha vibao vyao na kuukaribisha mwaka 2012 na mashabiki wao ukumbi wa TCC-Chang'ombe, wilayani Temeke.
"Sie tumeamua kukomaa Dar ambapo kama kawaida leo Ijumaa tupo Leaders Club wilayani Kinondoni, Jumamosi tutakuwa TCC- Chang'ombe kwa mashabiki wa wilaya ya Temeke na Jumapili tunamalizia hasira zetu kwa watu wa Ilala pale DDC Kariakoo," alisema.
Alisema katika maonyesho yote, Msondo watapiga nyimbo zao zote zilizowasambaratisha wapinzani wao, Sikinde katika mpambano wao usio rasmi uliofanyika siku ya Krismasi.
"Tutatumia silaha zetu zote zilizowasambaratisha wapinzani wetu wiki iliyopita, kuanzia Suluhu, Dawa ya Deni, Baba Kibene, Nadhiri ya Mapenzi, hadi nyimbo za albamu zetu za zamani kuanzia enzi za NUTA, JUWATA na OTTU," alisema Super D.

Jinamizi la Talaka lipo Mwanza



BENDI kongwe ya muziki wa dansi ya Mlimani Park 'Sikinde' wanatarajia kuvitambulisha vibao vyao vipya kikiwemo 'Jinamizi la Talaka' kwa mashabiki wao wa jijini Mwanza.
Bendi hiyo iliyoondoka jana jijini Dar es Salaam ikiwa na kikosi chake kamili imeenda kuuaga mwaka 2011 na kuukaribisha mwaka mpya jijini Mwanza kwa kufanya maonyesho mawili.
Katibu Mipango wa bendi hiyo, Hamis Milambo alisema onyesho la kwanza litafanyika kesho kwenye ukumbi wa Villa Park, kabla ya kumalizia burudani yao keshokutwa kwa onyesho jingine ambalo litafanyika CCM Kirumba.
Milambo, alisema katika maonyesho yote watatambulisha nyimbo zao zinazoandaliwa kwa ajili ya albamu yao mpya iliyoanza kurekodiwa itakayokuwa na nyimbo sita.
"Tunaelekea Mwanza kufanya maonyesho mawili kwa ajili ya kuuaga na kuukaribisha mwaka 2012 na mashabiki wetu wa jijini humo, ambapo tutafanya onyesho la kwanza Villa Park na kumalizia CCM Kirumba," alisema Milambo.
Milambo alisema hata hivyo hakuwa na hakika ya onyesho la CCm Kirumba, akidai huenda wakafanya onyesho ukumbi wa ndani ambao watapangiwa na wenyeji wao waliowaalika jijini humo.
Katibu huyo alivitaja vibao vipya vitakavyotambulishwa ni Jinamizi la Talaka, 'Kilio cha Kazi', 'Kinyonga', 'Bundi', 'Samahani' na 'Deni Nitalipa'.
"Hivyo ni baadhi tu, lakini pia tutakumbushia nyimbo zetu za zamani zilizoifanya Sikinde kuwa Mabingwa wa Dansi Tanzania," alisema Milambo.

Big Daddy yafunga mwaka wa Kanumba



MSANII nyota wa fani ya filamu nchini, Steven Kanumba 'The Great', amedai filamu yake mpya ya 'Big Daddy' ndiyo ya kufungua mwaka.
Hata hivyo, Kanumba alisema tayari ameshaandaa kazi nyingine mpya kwa ajili ya kufungua mwaka mpya wa 2012 unaoatarajiwa kusherehekewa keshokutwa.
Kanumba, alisema kama ilivyokuwa filamu za 'This is It', 'Uncle JJ', filamu ya Big Daddy imejaa vunja mbavu, sambamba na kuibua wasanii chipukizi aliowatabiria kutamba baadaye.
"Niliuanza mwaka kwa kutoka na Deception na ninaufunga na Big Daddy, ni moja ya kazi iliyojaa vichekesho na iliyowaibua wasanii chipukizi kama nilivyofanya kazi zangu za nyuma," alisema.
Aliwataja baadhi ya wasanii walioibuliwa ndani ya filamu hiyo ni Jamila Jaylawi na Jalilah Jaylawi, mbali na Cathy Rupia, Abdul Ahmed, Patchou Mwamba na yeye walioishiriki kazi hiyo.
Kanumba alisema, kazi yake mpya inatarajiwa kufahamika mara baada ya mwaka 2012 kuingia, ila alitamba kuwa ni kama kazi zake nyingine ambazo huwafanya mashabiki wa fani hiyo kuumwa wazikosapo kwa namna zinavyoambiliwa.

Villa Squad yajitapa haishuki daraja ng'o!

UONGOZI wa klabu ya soka ya Villa Squad, umesema utajitahidi kadri ya uwezo wao kuhakikisha timu yao haishuki daraja kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Villa iliyorejea ligi kuu msimu huu tangu iliposhuka msimu wa 2008, ndiyo inayoburuza mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo ikizibeba timu nyingine 13 na ni moja ya klabu iliyo na hali mbaya kiuchumi kiasi cha kutishia ushiriki wao wa ligi hiyo.
Hata hivyo Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ramadhani Uledi, alisema licha ya kumaliza duru la kwanza wakiwa hoi, uongozi wao umejipanga kuhakikisha timu hiyo haishuki daraja.
Uledi, alisema kitu cha kwanza walichofanya kuhakikisha Villa haiteremki daraja ni kukipangua kikosi chao cha awali kwa kusajili wachezaji wapya kulingana na mapendekezo ya kocha wao, Habib Kondo na wasaidizi wake.
"Cha pili tunachopanga kwa sasa ni kuhakikisha timu inaandaliwa mapema nma kucheza mechi nyingi za kujipima nguvu, ili kutoa fursa kwa wachezaji kupata uzoefu na kumpa nafasi mwalimu kuona na kurekebisha makosa mapema," alisema.
Uledi alisema kwa namna hiyo wanaamini ni vigumu kwa Villa kuendelea kuwa 'mdebwedo' katika duru la pili la ligi hiyo itakayoanza Januari 21.
"Tunawaahidi wanachama na wadau wa soka wa Kinondoni kwamba Villa Squad haitashuka daraja na tunaomba tuungwe mkono kwa kuisaidia kwa hali na mali, viongozi tupo makini na tumerekebisha mambo yote yaliyotukwaza duru lililopita," alisema.
Timu hiyo yenye maskani yake Magomeni Mapipa, imesajili wachezaji wapya 11 wakiwemo sita waliopata kwa mkopo toka Azam Fc na kuwaondosha kikosi baadhi ya wachezaji walioonekana hawastahiki kuichezea timu hiyo.

Snake Jr apania kulinda rekodi, heshima ya baba yake



BONDIA chipukizi 'asiyepigika', Mohammed Matumla 'Snake Boy Jr', amesema amepania kumsambaratisha mpinzani wake, Cosmas Cheka atakayepigana nae kesho mjini Morogoro ili kulinda heshima ya baba yake, Rashid Matumla 'Snake Man.
Matumla na Cheka wanatarajiwa kuzichapa kesho kwenye uwanja wa Jamhuri, katika pambano lisilo la ubingwa la kumaliza ubishi baina yao, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Akizungumza na MICHARAZO, Matumla alisema kwa namna alivyojiandaa ni wazi atamsambaratisha mpinzani wao licha ya kucheza uwanja wa nyumbani, lengo likiwa ni kulinda hadhi ya baba yake, Rashid Matumla mbele ya ukoo wa akina Cheka.
Matumla, alisema mbali na kutaka kulinda heshima ya baba yake aliyewahi kupigwa na kumpiga Francis Cheka katika mipambano yao, pia anataka kulinda rekodi yake ya kutopigwa na bondia yeyote nchini.
"Naenda Morogoro kuhakikisha namchakaza Cheka ili kulinda heshima ya mdingi (baba), na kulinda rekodi yangu ya kutopigwa katika michezo 10 niliyokwishacheza hadi sasa," alisema Matumla.
Hata hivyo wakati Matumla akijiapiza hivyo, mpinzani wake amenukuliwa na vyombo vya habari kwamba hana hofu dhidi ya pambano hilo kwa kuamini ataibuka na ushindi kuendeleza ubabe wa ukoo wao mbele ya ukoo wa akina Matumla.
Kwa mujibu wa rekodi zilizopo baina ya mabondia hao wawili ni kwamba Matumla ambaye ni mtoto wa bingwa wa zamani wa WBU, amecheza michezo 10 na kushinda saba, huku Cosmas Cheka mdogo wa Francis Cheka amecheza mechi saba na kushinda manne, akipoteza moja na kupata sare mbili.
Kwa mujibu wa waratibu wa pambano hilo, kabla ya Cheka na Matumla kupanda ulingoni mabondia wa kike wenye upinzani wa jadi, Salma Kiogwa wa Morogoro na Asha Ngedere wa Dar watapigana sambamba na mapambano mengine ya utangulizi.

Mwisho

Super D ajivunia mafanikio mwaka 2011



NYOTA wa zamani wa ngumi za kulipwa nchini ambaye kwa sasa ni kocha wa klabu ya mchezo huo ya Ashanti na timu ya mkoa wa Ilala, Rajabu Mhamila 'Super D' amesema anajivunia mafanikio makubwa aliyoyapata ndani ya mwaka 2011.
Akizungumza na MICHARAZO, Super D, ambaye pia ni Msemaji wa bendi kongwe ya Msondo Ngoma, alisema moja ya mafanikio anayojivunia ni kuwaandaa vijana wengi wanaochipukia katika mchezo sambamba na kuwaelimisha wengine kwa njia ya DVD.
Super D, alisema mbali na hilo pia ameweza kushirikiana vema na wadau wa ngumi
pamoja na mapromota mbalimbali wanaoandaa mapambano makubwa kwa kutoa
mchango wake wa vifaa vya ngumi kufanikisha mapambano hayo ndani ya 2011.
"Nashukuru mwaka 2011 umekuwa ni mwaka wa mafanikio kwangu kwa kuridhika namna nilivyojitahidi kuusaidia mchezo wa ngumi kwa kuwaibua vijana wengi sambamba na kuwasaidia wengine kupitia njia ya DVD ninazoandaa," alisema.
DVD hizo zenye mafunzo ya ngumi pamoja na michezo mikubwa iliyowahi kuchezwa na magwiji wa mchezo huo duniani zimekuwa zikiuzwa na kocha huyo kama njia ya kufika kwa haraka mafunzo ya ngumi kwa wadau wengi.
Ndani ya DVD hizo zinawajumuisha wakali kama Floyd Mayweather, Manny Paquaio, Amir Khan, Muhammed Ali, Mike 'Iron' Tyson, David Haye na wengine ikiwemo na matukio ya mazoezi yao kabla ya mapambano waliyocheza.
Super D, alisema kwa mwaka 2012 panapo majaliwa amepania kuendeleza aliyoyafanya mwaka huu katika kuwainua na kuwaendeleza chipukizi aliowaibua kama akina Shomar Mirundi, Ibrahim Class na Salum Ubwa ili watambe kimataifa.
Chipukizi hao wa klabu ya Ashanti wamekuwa wakifanya vema katika michezo yao, ikiwemo wiki iliyopita Ubwa kumtwanga kwa pointi 60-57 Mustapha Dotto katika pambano lililosindikiza mpambano wa Maneno Oswald na Rashid Matumla.

Mwisho

Kazimoto atajwa mrithi wa Gagarino





KIUNGO mahiri wa klabu ya soka ya Simba, Mwinyi Kazimoto ametajwa kuwa ndiye mrithi wa kiungo nyota wa zamani aliyewahi kutamba nchini na timu za Simba na Yanga, Hamis Gaga 'Gagarino' kwa namna ya uchezaji wake.
Beki wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Willy Martin 'Gari Kubwa', ndiye aliyemtawaza Kazimoto kurithi mikoba ya Gagarino ambaye kwa sasa ni marehemu.
Martin, alisema kwa namna ya uchezaji wake kuanzia umiliki wa mipira, kugawa vyumba na kuburudisha uwanjani, Kazimoto ndiye haswa anayeonekana kufuata nyayo za Gagarino.
Hata hivyo Martin, aliyewaji kuzichezea timu za Simba, Yanga na Taifa Stars, alisema Kazimoto, amekuwa akishindwa kuonyesha makali yake kutokana na kuwa majeruhi mara kwa mara.
"Ukitaka nikuambie ni mchezaji gani ambaye anafuata nyayo za nyota wa zamani ambao walikuwa wakiwatendea haki watazamaji uwanjani, basi ni Mwinyi Kazimto kwani kwa uchezaji wake hana tofauti kabisa na Gagarino," alisema Martin.
Beki huyo aliyewahi kuzichezea pia timu za Majimaji-Songea na Bandari-Mtwara, alisema kwa yeyote anayependa burudani na ufundi dimbani basi kwa Kazimoto kila kitu kipo kama alivyokuwa marehemu Gagarino kiungo mahiri kuwahi kutokea nchini.
Martin, alisema anaamini Kazimoto asingekuwa akisumbuliwa na majeraha huenda angeibeba Tanzania katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars na klabu anazochezea.
Mwinyi Kazimoto alitua Simba msimu huu akitokea JKT Ruvu, ambapo amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa viungo bora kwa namna ya 'ufundi' aliokuwa nao na amewahi kuitwa Stars mara kadhaa kabla ya kuenguliwa kutokana na kuwa majeruhi.

Mwisho

Moro Utd waanza kujifua, kuanza kambi Jan 10

WAKATI uongozi wa Moro United ulitangaza kuwa, kambi rasmi ya timu hiyo kujiandaa na duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara itaanza rasmi Janauri 10, jumla ya wachezaji 20 wa timu hiyo wakijitokeza siku ya kwanza ya mazoezi ya klabu hiyo.
Mazoezi hayo ya Moro United yalianza jana asubuhi eneo la Tabata Segerea, jijini Dar es Salaam, tayari kwa maandalizi hayo ya ligi kuu itakayoendelea tena Januari 21.
Katika mazoezi hayo ni wachezaji sita tu ndio waliokosekana kutokana na sababu mbalimbali na kuufanya uongozi wa klabu hiyo kufurahia mahudhurio ya nyota wake hao waliojitoeza kuanza kujifua hiyo jana.
Katibu Mkuu wa Moro United, Hamza Abdallah 'Mido' aliiambia MICHARAZO kuwa, kujitokeza kwa wachezaji 20 katika siku ya kwanza ya mazoezi yao ni muitikio mzuri na imani nyota wao sita waliokosekana watajumuika kadri siku zinazoendelea.
Wachezaji waliokosekana kwenye mazoezi hayo ni pamoja na kipa Jackson Chove, George Mkoba, Steohen Marashi, Sadick Gawaza na Gideon Sepo.
Katibu huyo aliongeza kuwa mazoezi ya timu hiyo yataendelea kila siku asubuhi hadi Januari 10 wakati timu hiyo itapoingia rasmi kambini sambamba na kuanza kucheza mechi za kirafiki za kujipima nguvu na timu watakazokubaliana nazo.
"Kambi rasmi ya timu yetu itaanza Januari 10, kwa sasa wachezaji watakuwa wakitokea majumbani kuja mazoezini kila siku jioni, wiki mbili baadae ndipo kikosi chetu kitaanza kucheza mechi za kirafiki za kujiweka tayari kwa ligi hiyo," alisema Abdallah.
Abdallah alisema wanatarajia kucheza mechi tatu za kujipima nguvu na timu za Ligi Kuu Tanzania Bara, ingawa hakuweza kuzitaja majina yake kwa madai ni mapema mno.
Moro United ni miongoni mwa timu nne zilizopanda daraja msimu huu zikitokea Ligi Daraja la Kwanza. Nyingine ni Villa Squad, Coastal Union na JKT Oljoro.

Mwisho

Matumla alilia ushindi kwa Maneno, mratibu ampuuza




BINGWA wa zamani wa Dunia wa Ngumi za Kulipwa, Rashid Matumla 'Snake Man', ameibuka na kudai alistahili kuwa mshindi wa pambano lake dhidi ya Maneno Oswald 'Mtambo wa Gongo' lililofanyika Desemba 25 jijini Dar es Salaam.
Pia bondia huyo amewalalamikia waandaaji wa mchezo huo kwa madai ulingo ulikuwa una utelezi, kiasi cha kumfanya aanguke mara kadhaa na kupelekea kuumia mkono na mguu.
Katika pambano hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa Heinkein Pub, Mtoni Kijichi, Matumla na Maneno walishindwa kutambiana baada ya kutangazwa wametoka sare kwa kupata pointi 99-99, kitu ambacho Maneno alikipinga akidai alistahili yeye ushindi.
Hata hivyo, Matumla naye ameibuka na kudai yeye alistahili kutangazwa mshindi kwa namna alivyocheza na kumdhibiti mpinzani wake aliyekiri ni mmoja wa mabondia wazuri nchini.
"Kwa kweli licha ya kwamba mwamuzi na majaji ndio watu wa mwisho katika maamuzi na kukubaliana na maamuzi ya kutangaza droo baina yangu na Maneno, lakini naamini nilistahili kuwa mshindi kwa jinsi nilivyocheza," alisema Matumla.
Matumla, alisema hata baadhi ya mashabiki waliofurika kwenye ukumbi huo walikuwa wakilalamikia droo iliyotangazwa kitu kinachoonyesha mechi ile haikustahili kuwa hivyo.
Pia, alisema kuanguka kwake mara kwa mara ulingoni kulitokana na ulingo kuwa na utelezi na kutoa ushauri wa waandaaji wa ngumi wawe wakiepuka vitu kama hivyo ili kusaidia kufanya mabondia waonyeshe uwezo wao na kuwapa burudani mashabiki.
"Waandaaji wawe makini na maandalizi ya michezo yao, wajaribu kuandaa ulingo wenye ubora sio kama ilivyotokea katika pambano letu ambapo kulikuwa na utelezi na kusababisha niumie mkono na miguu kwa kuanguka wakati wa mchezo,"alisema.
Muandaaji wa pambano hilo, Shaaban Adios 'Mwayamwaya' ameyapinga madai ya Matumla kwa ulingoni ulikuwa na utelezi kwa kudai kuwa ulingo huo kwa miaka mingi ndio 'Snake Man' amekuwa akiutumia kuwapiga wapinzani wake.
Adios alisema ulingo huo uliletwa na DJB Promotion, ambao ndio waliowakodisha na juu ya kuanguka kwa Matumla, alisema alimueleza viatu vyake vilikuwa vimelika 'kashata'.
"Kama ulingo ulikuwa unateleza mbona Maneno hakuwa akianguka, pia ndio ulingoni mkubwa na wenye ubora wa hali ya juu kati ya ulingo zote nchini na ambao Matumla amekuwa akiutumia kuwapiga wapinzani wake," alisema Adios.

Mwisho