UONGOZI wa klabu ya soka ya Villa Squad, umesema utajitahidi kadri ya uwezo wao kuhakikisha timu yao haishuki daraja kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Villa iliyorejea ligi kuu msimu huu tangu iliposhuka msimu wa 2008, ndiyo inayoburuza mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo ikizibeba timu nyingine 13 na ni moja ya klabu iliyo na hali mbaya kiuchumi kiasi cha kutishia ushiriki wao wa ligi hiyo.
Hata hivyo Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ramadhani Uledi, alisema licha ya kumaliza duru la kwanza wakiwa hoi, uongozi wao umejipanga kuhakikisha timu hiyo haishuki daraja.
Uledi, alisema kitu cha kwanza walichofanya kuhakikisha Villa haiteremki daraja ni kukipangua kikosi chao cha awali kwa kusajili wachezaji wapya kulingana na mapendekezo ya kocha wao, Habib Kondo na wasaidizi wake.
"Cha pili tunachopanga kwa sasa ni kuhakikisha timu inaandaliwa mapema nma kucheza mechi nyingi za kujipima nguvu, ili kutoa fursa kwa wachezaji kupata uzoefu na kumpa nafasi mwalimu kuona na kurekebisha makosa mapema," alisema.
Uledi alisema kwa namna hiyo wanaamini ni vigumu kwa Villa kuendelea kuwa 'mdebwedo' katika duru la pili la ligi hiyo itakayoanza Januari 21.
"Tunawaahidi wanachama na wadau wa soka wa Kinondoni kwamba Villa Squad haitashuka daraja na tunaomba tuungwe mkono kwa kuisaidia kwa hali na mali, viongozi tupo makini na tumerekebisha mambo yote yaliyotukwaza duru lililopita," alisema.
Timu hiyo yenye maskani yake Magomeni Mapipa, imesajili wachezaji wapya 11 wakiwemo sita waliopata kwa mkopo toka Azam Fc na kuwaondosha kikosi baadhi ya wachezaji walioonekana hawastahiki kuichezea timu hiyo.
No comments:
Post a Comment