STRIKA
USILIKOSE
Friday, December 30, 2011
Kazimoto atajwa mrithi wa Gagarino
KIUNGO mahiri wa klabu ya soka ya Simba, Mwinyi Kazimoto ametajwa kuwa ndiye mrithi wa kiungo nyota wa zamani aliyewahi kutamba nchini na timu za Simba na Yanga, Hamis Gaga 'Gagarino' kwa namna ya uchezaji wake.
Beki wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Willy Martin 'Gari Kubwa', ndiye aliyemtawaza Kazimoto kurithi mikoba ya Gagarino ambaye kwa sasa ni marehemu.
Martin, alisema kwa namna ya uchezaji wake kuanzia umiliki wa mipira, kugawa vyumba na kuburudisha uwanjani, Kazimoto ndiye haswa anayeonekana kufuata nyayo za Gagarino.
Hata hivyo Martin, aliyewaji kuzichezea timu za Simba, Yanga na Taifa Stars, alisema Kazimoto, amekuwa akishindwa kuonyesha makali yake kutokana na kuwa majeruhi mara kwa mara.
"Ukitaka nikuambie ni mchezaji gani ambaye anafuata nyayo za nyota wa zamani ambao walikuwa wakiwatendea haki watazamaji uwanjani, basi ni Mwinyi Kazimto kwani kwa uchezaji wake hana tofauti kabisa na Gagarino," alisema Martin.
Beki huyo aliyewahi kuzichezea pia timu za Majimaji-Songea na Bandari-Mtwara, alisema kwa yeyote anayependa burudani na ufundi dimbani basi kwa Kazimoto kila kitu kipo kama alivyokuwa marehemu Gagarino kiungo mahiri kuwahi kutokea nchini.
Martin, alisema anaamini Kazimoto asingekuwa akisumbuliwa na majeraha huenda angeibeba Tanzania katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars na klabu anazochezea.
Mwinyi Kazimoto alitua Simba msimu huu akitokea JKT Ruvu, ambapo amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa viungo bora kwa namna ya 'ufundi' aliokuwa nao na amewahi kuitwa Stars mara kadhaa kabla ya kuenguliwa kutokana na kuwa majeruhi.
Mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment