STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, February 4, 2011

Wasanii wa kike tujiheshimu-Regina



MMOJA wa waigizaji wa filamu anayekuja juu nchini, Regina Mroni amewaasa wasanii wenzake hususani wa kike, kujiheshimu na kuepukana kufanya matendo yanayowachafua mbele ya jamii pamoja na kuidhalilisha fani yao kuonekana kama kazi ya wahuni.
Mroni, aliyeng'ara kwenye filamu kama Trip to Amerika, Mastress, Siri y Mama, Aisha na nyinginezo, alisema kuna baadhi ya wasanii hasa wa kike wamekuwa wakiona raha kujianika utupu na kuhusishwa na skendo chafu, wakiamini wanakuza majina yao wakati wanajidhalilisha.
Alisema umaarufu wa msanii yeyote unapatikana kutokana na ubora na umahiri wa kazi zake na sio matendo machafu na hivyo kuwataka wasanii wa kike wajiamini, kujituma na kuithamini kazi yao ili jamii iwaheshimu.
"Wapo baadhi yetu wamekuwa wakijihusisha na matendo machafu na kuandikwa kila mara, kitu ambacho tofauti na fikra zao kuwa wanajijengea majina na umaarufu, wanajidhalilisha na kuonekana mbele ya jamii kama watu wasio na maadili kitu ambachio ni kibaya," alisema Mroni.
Mroni, aliyetumbukia kwenye fani hiyo miaka miwili iliyopita akitokea kwenye urembo ambapo aliwahi Miss Utalii Morogoro, Miss Ukonga, Miss Singida na kushiriki Miss Tanzania, alisema sanaa ni kazi kama kazi nyingine na wanaishiriki waithamini na kuipenda.
Alisema 'wavamizi' wachache kwenye fani hiyo wasio na vipaji ndio wanaojiachia na kujianika na mwisho wa siku wanadhalilika na kisha kupotea wakiwaacha wasanii wa kweli wakiendelea kutamba.

Mwisho

TAFF yapewa kifyagio kwa tamasha la filamu la Nyerere

SHIRIKISHO la Filamu Tanzania, TAFF, limepewa heko kwa ubunifu wake wa kuanzisha tamasha la filamu za Kibongo ambalo litafanyika Februari 14-19 jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo la kwanza kufanyika nchini kwa filamu za Kitanzania litafanyikia kwenye viwanja vya Leaders kwa kuzunduliwa na Rais Jakaya Kikwete na kufungwa na mke wa hayati baba wa taifa, Mwl Nyerere, Mama Maria Nyerere.
Baadhi ya wadau wa filamu wakiwemo wasanii wa fani hiyo wamesema kitendo cha TAFF kubuni tamasha hilo ni jambo la kupongezwa kwa vile litasaidia kuinua soko la kazi za wasanii wa kibongo, mbali na kutoa fursa kwa wananchi kupata mwamko wa kuzipenda kazi hizo.
"TAFF wamefanya jambo la maana ambalo wadau wa filamu Bongo tulikuwa tunalisubiri kwa muda mrefu, kitu cha muhimu waliendeleze kama mengine," alisema Leila Mwambungu wa Kimara.
Leila, alisema tamasha hilo linaweza kusaidia kuamsha hisia wa watanzania kupenda kazi za nyumbani kwa madai wapo wengine wanazichukulia poa filamu za Kibongo na kuhusudu kazi za Nigeria au Marekani.
Mtayarishaji wa filamu anayekuja juu, Husseni Ramadhani 'Swagger' alisema tamasha hilo ni kama njia ya wadau wa filamu kujitangaza na kuwahimiza wenzake kujitokeza kwa wingi kulishiriki kuanzia mwanzo wake hadi siku ya ufungwaji wake.
"Nafasi kama hizi ni muhimu kuzichangamkia, kwa kweli nalipongeza TAFF kwa kubuni kitu kama hiki, kwani itatusaidia wengine kujifunza makubwa zaidi ya yale tunayoyajua katika sanaa hiyo kutokana na ukweli tumesikia kuna mafunzo kadhaa yatakayotolewa hapo," alisema Swagger ambaye anatamba na filamu kama Hazina, Who is a Killer na sasa Bangkok Deal.
TAFF kupitia viongozi wake chini ya Rais Simon Mwakifamba, walitangaza kuanzisha kwa tamasha hilo litakalozinduliwa wiki ijayo na Rais Kikwete kwa ajili ya kuonyesha kazi za kitanzania pamoja na kupambwa na burudani kadhaa za sanaa na mada mbalimbali za kifani.
***

Ray, Kanumba na Msondo kila mtu kivyake

Ray ana 'Second Wife, Deception noma!


WAKATI filamu ya Family Disaster ikiendelea kutamba mitaani kwa sasa, msanii nyota wa fani hiyo nchini, Vincent Kigosi 'Ray', yupo mbioni kuachia kazi nyingine mpya iitwayo 'The Second Wife'.
Filamu hiyo ya kimapenzi, imewashirikisha wasanii kadhaa nyota pamoja na waigizaji chipukizi ambao wameibuliwa na kampuni iliyotayarisha filamu hiyo, RJ Production.
Miongoni mwa waigizaji walioshiriki filamu hiyo ni pamoja na Ray mwenyewe, Colleta Raymond, Aisha Bui, Riyama Ally, Msungu, Ramla na mtoto aitwae Aisha ambaye ni chupukizi.
Ray ameanika kwenye mtandao wake kuwa, filamu hiyo ambayo ameigiza kama muumini wa Kiislam ipo katika hatua ya mwisho kabla ya kuachiwa ni moja ya kazi yenye mafunzo makubwa kwa jamii.
"Kama nilivyofanya kwenye The Divorce ndani ya filamu hii mafunzo ni yale yale na mashabiki mkae mkao wa kula kupata uhondo," alisema Ray.
Kwa mujibu wa taarifa hizo kama filamu zake nyingine, 'The Second Wife' itasambazwa na kampuni ya Steps Entertainment.
Wakati huo huo filamu mpya ya Steven Kanumba iitwayo Deception, aliyoigiza pamoja na Bakari Makuka, Rose Ndauka na Patcho Mwamba imekuwa ikinunuliwa kama njugu tangu iigizwe sokoni mapema wiki hii.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Nipashe, filamu hiyo imekuwa ikigombewa kununuliwa sambamba na Pete ya Ajabu na Family Disaster ambayo ina karibu mwezi sasa sokoni.
***


Msondo wapeleka mpya Songea


BENDI kongwe ya muziki wa dansi ya Msondo Ngoma, kesho inatarajiwa kuzitambulisha nyimbo zao mpya zinazoandaliwa kwa ajili ya albamu ya 2011 mjini Songea mkoani Ruvuma.
Msondo inayotamba na albamu ya ya Huna Shukrani, itatumbuiza kwenye ukumbi wa Serengeti Bar, mjini huo.
Kwa mujibu wa kiongozi wa bendi hiyo, Said Mabera 'Diblo' ni kwamba Msondo itatumbuiza kwenye ukumbi huo nyakati za usiku, wakati jioni watakuwepo kwenye dimba la Majimaji kushuhudia pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Yanga na wenyeji Majimaji-Songea.
Mabera, alisema katika onyesho hilo, bendi yao itapiga nyimbo zao za zamani pamoja na zile mpya zinazoendelea kuandaliwa kwa ajili ya albamu yao ijayo.
"Tupo Songea na kesho tutafanya onyesho kwenye ukumbi wa Serengeti, wakazi wa Songea wakae mkao wa kupata uhondo mtupu," alisema Mabera mmoja wa wapiga solo mahiri nchini na mwanamuziki aliyedumu kwa muda mrefu Msondo tangu alipojiunga mwaka 1973.
Mabera alizitaja baadhi ya nyimbo watakazozipiga kwenye onyesho hilo ni pamoja na zile za albamu za Demokrasia ya Mapenzi, Ndoa Ndoana, Kilio cha Mtu Mzima, Piga Ua Talaka Utatoa, Kaza Moyo, Kicheko kwa JIrani na Huna Shukrani.
"Pia tutawapigia na kuzitambulisha nyimbo mpya za Lipi Jema, Dawa ya Deni, Kwa Mjomba Hakuna Urithi na Baba Kakura, yaani ni burudani kwa kwenda mbele," alisema.
Baadhi ya wanamuziki wa Msondo ambayo wiki iliyopita ilimpoteza mmoja wa waimbaji wake mahiri, Hamis Maliki 'Super Maliki' watakapanda jukwaani leo ni pamoja na Mabera, Roman Mng'ande, Huruka Uvuruge, Ibrahim Kandaya, Juma Katundu, Is'haka Katima, Eddo Sanga na wengineo.
***

Extra Bongo yaivunjavunja Twanga Pepeta





NENO zuri la kusema ni kwamba African Stars 'Twanga Pepeta' imevunjwavunjwa baada ya wanamuziki wake nyota saba kuihama bendi hiyo kwa mpigo na kutua Extra Bongo 'Wana 'Next Level' iliyoingia rasmi kambini kujiwinda na albamu mpya ya pili.
Wanamuziki hao saba walitambulishwa rasmi leo asubuhi na Mkurugenzi wa Extra Bongo, Ally Choki, ambapo alisema lengo la kuwanyakua wakali hao ni kutaka bendi yake iwe matawi ya juu na kuleta mabadiliko ya muziki wa dansi nchini.
Choki aliwatambulisha wanamuziki hao ambapo ni waimbaji wawili, wapiga gitaa wawili na madansa watatu akiwemo mkali Hassani Mussa 'Super Nyamwela'.
Mbali na Nyamwela aliyeitumikia Twanga kwa miaka 11 mfululizo bila kuhama ni Rogart Hegga 'Catapilla' na Saul Ferguson ambao ni waimbaji, Hosea Mgohachi mpuiga gita zito la besi na Godi Kanuti anayecharaza magita yote.
Wanenguaji wengine waliomfuata Nyawela Extra Bongo ni Otilia Boniface na Issack Burhan maarudu kama Danger Boy.
Choki alisema wanamuziki hao wote wana mikataba na bendi yao na mchana huu wanatarajia kuungana na wanamuziki wenzao kambini eneo la Mbezi Mwisho kujipanga kwa albamu mpya.
Alisema kambi hiyo ya muda wa wiki tatu itatumika kuwapa fursa wanamuziki hao wapya kuzoeana na wenzao kabla ya kuanza kufanya vitu vyao hadharani wakiwa wamezaliwa upya.
Mkurugenzi huyo aliyesema tukio kama hilo la kuibomoa Twanga liliwahi kumtokea miaka minne iliyopita alipochukuliwa wanamuziki wa idadi kama hiyo na ASET na kuifanya Extra Bongo 3x3 Kujinafasi kuzimika hadi ilipofufuka mwaka jana.
Alisema wanamuziki hao wapya wamenyakuliwa na Extra Bongo tayari kuziba nafasi za waliotemwa akiwemo rapa machachai Greyson Semsekwa na wenzake kadhaa.
Wakizungumza kwenye utambulisho huo, Ferguson na Nyamwela walisema wamekuja kuthibitisha thamani yao na mashabiki wa Extra Bongo watarajie makubwa.
"watarajie kazi bab'kubwa kwani tunafahamika kwa vipaji vya fani hii," alisema Ferguson.

Nyamwela aitema Twanga, adai miaka 11 imetosha





KIONGOZI wa muda mrefu wa madansa wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' Hassan Mussa 'Super Nyamwela', aliyetangazwa jana kujiunga na bendi ya Extra Bongo, amedai amefikia uamuzi huo kwa lengo la kutaka kubadilisha upepo baada ya kukaa bendi yke kwa miaka zaidi ya 10.
Akizungumza kwenye utambulisho wake na wenzake sita toka Twanga, Nyamwela alisema miaka 11 aliokaa ASET imemtosha na ndio maana ameondoka ili kuzaliwa upya.
Nyamwela alisema hata hivyo pamoja na kuondoka Twanga ikiwa ni bendi yake pekee kuifanyia kazi tangu alipochukuliwa toka kundi la Billbum, hawezi kuponda alikotoka kwa vile imemsaidia kwa mengi na kwa sasa akili yake ni kuwapa burudani mashabiki wa bendi yake mopya.
"Nimeondoka kwa kutaka kubadilisha upepo, mnanijua mie sina utamaduni wa kuhamahama, ila kwa kutaka kuleta mabadiliko katika fani na maisha yangu kwa ujumla nimeamua kuoka Twanga na watu wasinchukulie vingine natafuta maisha," alisema dansa huyo bingwa wa zamani wa Bolingo Dar.
Aliongeza kuwa kama alivyokuwa Twanga alipoipa mafanikio makubwa, ndivyo ambavyo amepania kufanya hivyo akiwa Extra Bongo ambao ameungana nao kambini kujiandaa kupakua albamu mpya.
"Nyamwela ni yule yule, ila kwa hapa Extra mashabiki wake watarajie mambo makubwa na mazuri zaidi, na imani kwa ushirikiano na wenzangu Extra Bongo itatisha," alisema Nyamwela.
Mbali na Nyamwela, katika utambulisho huo, pia madansa Otilia Boniface, Isaack Burhani nao walitambulishwa sambamba na wanamuziki, Rogart Hegga 'Catapillar', Saulo Ferguson, Hosea Mgohachi na God Kanuti waliokuwa Twanga Pepeta.
wanamuziki hao walitambulishwa kwa waandishi wa habai jana na Mkurugenzi wa bendi hiyo ya Extra Bongo, Ally Choki 'Kamarade'.