STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, February 4, 2011

Ray, Kanumba na Msondo kila mtu kivyake

Ray ana 'Second Wife, Deception noma!


WAKATI filamu ya Family Disaster ikiendelea kutamba mitaani kwa sasa, msanii nyota wa fani hiyo nchini, Vincent Kigosi 'Ray', yupo mbioni kuachia kazi nyingine mpya iitwayo 'The Second Wife'.
Filamu hiyo ya kimapenzi, imewashirikisha wasanii kadhaa nyota pamoja na waigizaji chipukizi ambao wameibuliwa na kampuni iliyotayarisha filamu hiyo, RJ Production.
Miongoni mwa waigizaji walioshiriki filamu hiyo ni pamoja na Ray mwenyewe, Colleta Raymond, Aisha Bui, Riyama Ally, Msungu, Ramla na mtoto aitwae Aisha ambaye ni chupukizi.
Ray ameanika kwenye mtandao wake kuwa, filamu hiyo ambayo ameigiza kama muumini wa Kiislam ipo katika hatua ya mwisho kabla ya kuachiwa ni moja ya kazi yenye mafunzo makubwa kwa jamii.
"Kama nilivyofanya kwenye The Divorce ndani ya filamu hii mafunzo ni yale yale na mashabiki mkae mkao wa kula kupata uhondo," alisema Ray.
Kwa mujibu wa taarifa hizo kama filamu zake nyingine, 'The Second Wife' itasambazwa na kampuni ya Steps Entertainment.
Wakati huo huo filamu mpya ya Steven Kanumba iitwayo Deception, aliyoigiza pamoja na Bakari Makuka, Rose Ndauka na Patcho Mwamba imekuwa ikinunuliwa kama njugu tangu iigizwe sokoni mapema wiki hii.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Nipashe, filamu hiyo imekuwa ikigombewa kununuliwa sambamba na Pete ya Ajabu na Family Disaster ambayo ina karibu mwezi sasa sokoni.
***


Msondo wapeleka mpya Songea


BENDI kongwe ya muziki wa dansi ya Msondo Ngoma, kesho inatarajiwa kuzitambulisha nyimbo zao mpya zinazoandaliwa kwa ajili ya albamu ya 2011 mjini Songea mkoani Ruvuma.
Msondo inayotamba na albamu ya ya Huna Shukrani, itatumbuiza kwenye ukumbi wa Serengeti Bar, mjini huo.
Kwa mujibu wa kiongozi wa bendi hiyo, Said Mabera 'Diblo' ni kwamba Msondo itatumbuiza kwenye ukumbi huo nyakati za usiku, wakati jioni watakuwepo kwenye dimba la Majimaji kushuhudia pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Yanga na wenyeji Majimaji-Songea.
Mabera, alisema katika onyesho hilo, bendi yao itapiga nyimbo zao za zamani pamoja na zile mpya zinazoendelea kuandaliwa kwa ajili ya albamu yao ijayo.
"Tupo Songea na kesho tutafanya onyesho kwenye ukumbi wa Serengeti, wakazi wa Songea wakae mkao wa kupata uhondo mtupu," alisema Mabera mmoja wa wapiga solo mahiri nchini na mwanamuziki aliyedumu kwa muda mrefu Msondo tangu alipojiunga mwaka 1973.
Mabera alizitaja baadhi ya nyimbo watakazozipiga kwenye onyesho hilo ni pamoja na zile za albamu za Demokrasia ya Mapenzi, Ndoa Ndoana, Kilio cha Mtu Mzima, Piga Ua Talaka Utatoa, Kaza Moyo, Kicheko kwa JIrani na Huna Shukrani.
"Pia tutawapigia na kuzitambulisha nyimbo mpya za Lipi Jema, Dawa ya Deni, Kwa Mjomba Hakuna Urithi na Baba Kakura, yaani ni burudani kwa kwenda mbele," alisema.
Baadhi ya wanamuziki wa Msondo ambayo wiki iliyopita ilimpoteza mmoja wa waimbaji wake mahiri, Hamis Maliki 'Super Maliki' watakapanda jukwaani leo ni pamoja na Mabera, Roman Mng'ande, Huruka Uvuruge, Ibrahim Kandaya, Juma Katundu, Is'haka Katima, Eddo Sanga na wengineo.
***

No comments:

Post a Comment