STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, October 6, 2014

Kassim Selembe achekelea kunolewa na Rishard Adolph

KIUNGO mshambuliaji mpya wa Polisi Moro, Kassim Suleiman 'Selembe' amesema anajisikia faraja kubwa kufanya kazi chini ya nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania Mohammed Rishard 'Adolph'.
Aidha mchezaji huyo aliyekuwa akiichezea Coastal Union, alisema kusuasusa kwa Polisi kwa sasa kunatokana na 'ugeni' wao wa Ligi Kuu, ila kadri watakavyokuwa wakiizoea watawashangaza watu.
Akizungumza na MICHARAZO, Selembe, alisema anajisikia furaha kufanya kazi na kocha Adolph, nyota wa zamani wa Yanga, Pan Africans na Taifa Stars ikizingatiwa ni moja wa nyota wa Tanzania waliojijengea jina kubwa Afrika.
"Kwa mchezaji yeyote anayejitambua kufanya kazi na mtu kama Adolph ni fahari kwa sababu alijijengea jina kubwa ndani na nje ya Tanzania enzi za uchezaji wake, wachezaji tunamfurahia," alisema.
Kiungo wa zamani wa Azam alisema kocha Adolph ni bonge la kocha na anawafanya wachezaji wa Polisi kujiamini na kurejea Ligi Kuu kabla ya yeye kuungana nao akitokea Coastal Union.
Juu ya mwenendo wa kikosi chao, Selembe alisema wanazidi kuimarika kadri wanavyoizoea ligi na kwamba hawana hofu ya kurejea walikotoka akidai ni mapema mno kujadili jambo hilo.
Timu hiyo ilipanda daraja sambamba na Ndanda na Stand United na ilianza kwa kufungwa mechi moja na kuambulia sare mbili katika mechi zao tatu za awali ya ligi hiyo inayoenda mapumziko.
Ligi hiyo itakuwa likizoni kwa wiki moja kupisha mchezo ya kimataifa ya kirafiki unaotambuliwa FIFA Taifa Stars itakapovaana na Benin na itaendelea tena kuanzia Oktoba 18.

Jahazi la QPR lazidi kutota, wapigwa 2-0 na West Ham

QPR  defender Rio Ferdinand
Rio Ferdinand akiwajibika na QPR akifikisha mechi ya 500 katika miaka ya 18 ya kucheza kwake
West Ham United v QPR
Ooh kitu! Wachezaji wa QPR hawaamini wakitunguliwa bao na West Ham
West Ham v QPR
Yebaaa! Wachezaji wa West Ham wakipongeza kwa kupata ushindi wa mabao 2-0 kwa vibonde QPR
JAHAZI la timu ya QPR linaloongozwa na kocha Harry Redknapp limezidi kuzama baada ya jana kucharazwa mabao 2-0 na West Ham United katika mfululizo wa Ligi Kuu ya England.
QPR wenye pointi na kuburuza mkia walianza vibaya mchezao huo baada ya beki wake kutoka Nigeria Chinedum Onuoha, aliyewahi kuichezea Mancjester City kujifunga bao dakika ya tano tu ya mchezo huo uliochezwa Uptown Park.
Kipindi chja pili kilikuwa majanga zaidi kwa wageni baada ya Diafra Sakho kuongeza bao la pili kwa West Ham kwa kuunganisha mpira wa kichwa katika dakika ya 55 na kuifanya West Ham kuchupa toka nafasi ya tisa katika msimamo wa ligi hiyo hadi ya saba, wakati QPR wakiendelea kung'ang'ania mkiani.
QPR haijawahi kushinda mechi yoyote ya uwanja wa ugenini tangu Machi 2, 2013.

Allan Kamote, Thomas Mashali mabingwa wapya wa UBO

Allan Kamote (kulia) akionyeshana umwamba na Osgood Kayuni wa Malawi katika pambano lao la kuwania Mkanda wa Dunia wa UBO na Kamote kushinda kwa pointi.
Thomas Mashali akimrushia konde Ramadhani Ali 'Alibaba' katika pambano lao lililochezwa jana kwenye uwanja wa Mkwakwani na Mashali kushindwa kwa TKO ya raundi ya tatu na kutwaa ubingwa wa UBO Afrika
MABONDIA Allan Kamote na Thomas Mashali wametawazwa kuwa mabingwa wa UBO baada ya kushinda mapambano yao ya ngumi za kulipwa yaliyofanyika jana uwanja wa Mkwakwani-Tanga.
Kamote alifanikiwa kutwaa ubingwa wa Dunia wa UBO baada ya kumshinda kwa pointi bondia Osgood Kayuni kutoka Malawi katika pambano la raundi 12 la uzani wa Light.
Naye bondia Thomas Mashali alimchapa kwa TKO ya raundi ya tatu Mtanzania mwenzake Ramadhani Ali 'Alibaba' na kutwaa mkanda wa UBO Afrika katika pambano lao la raundi 10 na uzito wa kati. Michezo hiyo iliratibiwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST) na ilishuhudiwa pia Francis Miyeyusho akimshinda kwa pointi bondia wa Tanzania anayeishi Kenya Emilio Norfat.
Bondia Kamote licha ya kufanikiwa kutwaa mkanda huo wa Dunia wa UBO, lakini pia amefanikiwa kulipa kisasi kwa mpinzani wake kutoka Malawi aliyewahi kupigana naye mara mbili na kupigwa.
Katika pambano hilo mabondia wote walikuwa wakiviziana na kutupiana makonde kwa ufundi, hali ambayo iliwafanya mashabiki kuwa roho juu kwa kutojua nani atakayeibuka na ushindi hadi jaji alipotangaza matokeo yaliyompa ushindi Kamote.
Katika mechi nyingine za utangulizi, bondia Francis Miyeyusho alimshinda kwa pointi Emilio Norfat, huku Jacob Maganga na Said Mundi wakishindwa kutambiana kwa kutoka sare.

Ronaldo azidi kutesa La Liga, Messi abakisha 2 tu!

Cristiano Ronaldo
Ronaldo akishangilia moja ya mabao yake matatu usiku wa jana
Lionel Messi of Barcelona
Messi akifunga bao lake la 349 katika La liga dhidi ya Rayo Valecano
WAKATI Lionel Messi akiwa amesaliwa na mabao mawili tu ili kufikia rekodi ya mabao katika Ligi Kuu ya Hispania, mpinzani wake Cristiano Ronaldo usiku wa jana alifunga hat-trick yake ya 22 wakati akiisaidia Real Madrid kushinda nyumbani kwa mabao 5-0 dhidi ya Athletic Bilbao.
Ronaldo alifunga mabao hayo katika dakika za 2, 55 na 88 akisaidiwa na Gareth Bale na Pepe, huku mabao mengine yakiwekwa kimiani na Karim Benzema katika dakika za 41 na 69 na kuifanya Madrid kufikisha jumla ya pointi 15, nne nyuma ya vinara Barcelona ambao wameendelea kushinda mfululizo katika ligi hiyo.
Mabao hayo yamemfanya Ronaldo kufikia rekodi ya ha trick nyingi za gwiji wa Madrid Alfredo de Stephano na Telmo Zarra waliowahi kufunga pia hat trick 22 akimtangulia Messi mwenye ha trick 19 akikamata nafasi ya tano.
Hata hivyo Messi aliisaidia Barcelona kushinda mechi yao ya sita na kuweka rekodi ya kutoruhusu kufungwa bao lolote katika mechi saba mfululizo wakati wakiizamisha Rayo Valecano kwao kwa mabao 2-0.
Messi alifunga bao lililomfanya afikishe jumla ya mabao 349 katika La Liga na kushika nafasi ya pili nyuma ya  gwiji wa zamani wa Athletic Bilbao, Telmo Zarra aliyetamba miaka ya 1940-50 aliyefunga mabao 351, ikiwa na maana akifunga mabao mawili tu atamfikia na kuifukizia rekodi mpya katika ligi hiyo maarufu.
Bao jingine la wababe hao wa Nou Camp liliwekwa kimiani na Neymar na kuwafanya wachezaji hao wawili wanaotoka mataifa hasimu katika soka Amerika ya Kusini, Argentina na Brazil kufikisha jumla ya mabao 13 wakicheza pamoja..
Katika mechi nyingine za ligi hiyo Atletico Madrid iokiwa ugenini ilikumbana na kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Valencia, huku Cordoba na Getafe walitoka sare ya 1-1 na Eibar kulazimishwa sare ya mabao 3-3 na Levante.
Almeria na Elche zilitoshana nguvu kwa sare ya 2-2 na Malaga ikaifumua 2-1 Grenada waliwafuata nyumbani kwao, huku Sevilla ikipata ushindi mnono nyumbani dhidi ya Deportivo la Coruna waliowafumua mabao 4-1 na Celta Viro ililala nyumbani 3-1 kwa Villarreal na Espaniol ilitaka nyumbani kwa kuilaza Real Sociedad kwa mabao 2-0.
ANGALIA WAKALI WA HAT TRICK LA LIGA
Cristiano Ronaldo 22
Alfredo Di Stefano 22
Telmo Zarra 22
Edmundo Suarez 19
Lionel Messi 19
Barcelona's Lionel Messi and Neymar
Neymar na Messi wakishangilia mabao yao wakati wakishinda ugenini na timu iliyopoteza wachezaji wao wawili uwanjani kw akandi nyekundu Rayo Valecano.