STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, February 22, 2011

Dokii ana scandal na JB



MSANII nyota wa muziki na filamu, Ummy Wenceslaus 'Dokii' amefyatua kazi yake mpya iitwayo 'Scandal' iliyowashirikisha wakali kadhaa wa fani hiyo nchini.
Filamu hiyo inayozungumzia masuala ya mapenzi na hila za baadhi ya watumishi wa Mungu, inatarajiwa kuachiwa mitaani kuanzia mwezi ujao ikiwa imetungwa na Dokii mwenyewe na kuongozwa na Adam Kuambiana.
Akizungumza na micharazo, Dokii, aliyeng'ara na michezo ya kuigiza kupitia kituo cha ITV akiwa na kundi la Mambo Hayo, alisema ndani ya filamu hiyo aliyoitunga mwenyewe, kuna wasanii mahiri kama Jacob Stephen 'JB'.
"Baada ya kimya tangu nilipoachia filamu ya Money Transfer, nimekamilisha kazi mpya iitwayo Scandal' ambayo nimeigiza na wasanii kadhaa nyota akiwemo mkali, JB, Colleta Raymond, Tini White na wengine," alisema Dokii.
Dokii aliwataja wasanii wengine waliopo ndani ya filamu hiyo ni pamoja na Jacqueline Pentezel 'Jack wa Chuz', Ramadhani Ally 'Taff', Tini White, Kishoka na wengine.
"Ni filamu ya kusisimua kwa jinsi ilivyoigizwa na ujumbe uliopo ndani ya kazi hiyo mpya," alisema Dokii.
Dokii, ambaye pia ni muimbaji wa muziki wa Injili amewahi kutamba na filamu kama Yoland, Hard Love Moro, Bad Friend, My Nephew, Lonely Heart na nyinginezo.
Kwa muda mrefu msanii huyo alikuwa wakiwachanganya mashabiki wake wakidhani ni Mkenya kutokana na kupenda kwake kuigiza lafudhi ya taifa hilo, ingawa ukweli yeye ni mwenyeji wa mkoa wa Morogoro.

Mwisho

Msalaba Wangu upo kwa Teddy

MTUNZI anayekuja juu katika fani ya utunzi wa riwaya, Teddy Chacha, amejitosa kwenye filamu na kuibuka na kazi mpya iitwayo 'Msalaba Wangu'.
Filamu hiyo inayozungumzia masuala ya kijamii na hasa kuwepo kwa imani potofu juu ya watu wenye ulemavu, imeshirikisha 'vichwa' kadhaa nyota vya fani ya uigizaji nchini akiwemo Pembe, 'Bi Hindu' na Charles Magali 'Mzee Magali'.
Akizungumza na Micharazo, Teddy alisema filamu hiyo ni zao la moja ya hadithi zake zinazochapishwa kwenye magazeti mbalimbali likiwemo NIPASHE, ambapo inazungumzia familia moja inayomkataa mtoto wao aliyezaliwa mlemavu wa akili.
Teddy, alisema filamu hiyo ni kama simulizi la kweli kutokana na kisa alichowahi kusimuliwa na kusema ni moja ya kazi yenye kuelimisha na kuiasa jamii juu ya kuepukana na mila na desturi potofu.
"Ni moja ya kazi yenye mafunzo na hasa kutokana na wahusika kubeba uhusika wao kwa kiwango cha hali juu," alisema Teddy.
Aliongeza kuwa filamu hiyo aliyotunga na kuiongoza mwenyewe, imerekodiwa na kampuni ya Magambo Entertainment na kwa sasa inamalizwa kuhaririwa kabla ya kutafutiwa soko tayati kuwapa wadau wa filamu burudani yenye mafunzo kwao.
Teddy, aliwataja washiriki wa filamu hiyo ni pamoja na Pembe, Bi Hindu, Mzee Magali, mtoto Yasin Kamba ambaye ndiye mhusika mkuu, Mohammed Hamis, Josephine Joseph na wengine.

Aisha Bui: Kisura anayetamba Bongo Movie




HANA muda mrefu tangu atumbukie kwenye faini ya uigizaji, lakini makali yake kupitia baadhi ya kazi alizoshiriki, zimemfanya Aisha Fat'hi maarufu kama Aisha Bui, kuwa tishio kwa waigizaji wakongwe wa kike.
Mwenyewe anakiri aliingia rasmi kwenye fani hiyo mwaka juzi kutokana na kuvutiwa na Wema Sepetu, licha ya kudai alipenda uigizaji licha ya kutowahi kujaribu tangu alipokuwa mdogo.
"Wema ndiye aliyechangia kujiingiiza kwangu kwenye filamu kutokana na kuvutiwa nae, ila tangu utotoni nilikuwa naipenda fani hiyo sambamba na ile ya uchoraji," alisema.
Alisema alipenda sana kuchora utotoni, kipaji ambacho anaamini kama angekiendeleza angefika mbali kwa vile alikuwa mahiri kuliko maelezo.
Filamu yake ya kwanza kumtangaza mwanadada huyo ni My Book, kisha kushiriki zingine kama Saturday Morning, Better Days, Not Without My Son, Continous Love na sasa ameibuka na Second Wife.
Aisha anayependa kuogelea, kufanya mazoezi na kupika, alisema kati ya kazi zote alizoshiriki ile ya Saturday Morning ndio filamu bomba kwake kwa jinsi alivyoigiza kwa umahiri.
"Saturday Morning, ndiyo picha kali kwangu wala sio siri," alisema kisura huyo.
Akiwa na ndoto za kuja kuwa muigizaji wa kimataifa, Aisha anasema hakuna anachochukia maishani mwake kama dharau ya uongo.
"Uongo na kufanyiana dharau ni vitu nisivyopenda maishani mwangu,"
Aisha Fat'hi aliyezaliwa mwaka 1983, alisema fani ya filamu nchini inazidi kupiga hatua, ingawa alisema bado haijawa na tija ya kutosha kutokana na kuwepo kwa wizi wa wajanja wachache.
Kisura huyo ambaye waliwahi kuhusishwa na marehemu Meddy Mpakanjia, hajaolewa wala
hana mtoto na mipango yake ni kujikita zaidi katika fani hiyo ili afike mbali ikiwezekana aje kumiliki kampuni yake binafsi ya kuzalisha filamu.
"Hizi ndizo ndoto zangu, kutamba kimataifa na kuja kumiliki kampuni yangu binafsi," alisema.
Aisha, alisema kwa umri wake na kiu ya mafanikio aliyokuwa nayo naamini atafika huko
akutakapo, muhimu Mungu amjalie umri na afya njema.