Kipa Aishi Manula |
Manula, miongoni mwa wachezaji chipukizi waliopo kikosi cha Kim Poulsen kinachojiandaa na mechi ya kukamilisha ratiba kati ya Tanzania na Gambia, alisema kwa mwendo ulianza kwenye ligi hiyo ni wazi msimu huu ni mgumu.
Kipa huyo aliyewahi kuwa kipa bora wa michuano ya Uhai Cup 2011, alisema matokeo ya kustaajabisha yaliyojitokeza katika mechi za raundi mbili za awali ni dalili za kuwa na msimu mgumu ulioweza kutabirika kirahisi.
"Nafurahishwa na namna ligi ilivyoanza, inaonyesha itakuwa ya aina yake msimu huu kwani timu zinaonyesha kupania kufanya vyema na ndiyo maana mechi mbili za awali za kila timu kumekuwa na matokeo yaliyostaajabisha, " alisema. Manula, alisema kwa upande wa klabu yake ya Azam anaamini huu utakuwa ni msimu wake wa kuweka rekodi kwa kunyakua ubingwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka nenda taji hilo kuzunguka klabu za Simba na Yanga.
Kipa huyo aliyekuwa dimbani wakati Azam ikizamishwa bao 1-0 na Yanga katika mechi ya Ngao ya Hisani, alisema haoni kitakachoizuia Azam isitimize ndoto ya kutwaa taji la Ligi Kuu mwaka 2013-2014.
Azam washindi wa pili wa misimu miwili mfululizo, ilianza ligi hiyo kwa mechi za ugenini ikipata sare ya 1-1 kwa Mtibwa Sugar kabla ya kuilaza Rhino Rangers 2-0 mjini Tabora na mechi ijayo itakuwa Kagera kuvaana na Kagera Sugar.