|
Mzee Small enzi za uhai wake |
|
Mzee Small (kati) akimpa tuzo Man Walter huku Bi Chau akiwa pembeni yake kulia |
|
Mzee Small akiwa na Bi Chau enzi za uhai wake, wawili hawa walikuwa wakiigiza kama mke na mume |
MSANII maarufu wa maigizo, Said Ngamba 'Mzee Small' anatarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya Tabata jijini Dar es Salaam baada ya kufariki juzi usiku akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa anatibiwa.
Msiba wa msanii huyo nguli uko nyumbani kwake Tabata nyuma ya Ofisi za Mwananchi, jijini Dar es Salaam.
Taarifa zilizotolewa jana mchana na mtoto wa marehemu, Muhiddin Said, zilieleza kuwa maandalizi ya kukamilisha safari ya mwisho ya marehemu yalikuwa yanaendelea vizuri na wanatarajia maziko yatafanyika saa 10 jioni.
"Tunatarajia maziko yatafanyika kesho (leo) saa 10 huku huku Tabata," alisema mtoto huyo.
Mzee Small jina lilitokana na ufupi wake alikuwa ni miongoni mwa waigizaji wa mwanzoni nchini waliofungua njia kwa wengine wengi wanaotamba kwa sasa.
Msanii huyo alipata umaarufu zaidi wakati alipokuwa akiigiza kama mume wa Chausiku Salum ‘Bi Chau’ kuanzia katika maigizo ya redioni hadi kwenye vituo vya televisheni.
Mzee Small alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kupooza na kusababisha kuacha kufanya kazi zake za sanaa kwa muda wa miaka miwiki.
Maisha na sanaa
Kwa historia fupi ya maisha yake, Mzee Small alizaliwa mwaka 1955 na kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Mingumbi huko Kilwa mkoani Pwani. Mbali na kuwa mkongwe, pia Mzee Small kila alipozungumza alikuwa na kawaida ya kujitamba kuwa yeye ndiye msanii wa kwanza kabisa Tanzania Bara kuchekesha katika luninga.
Pamoja na kuwa yeye ndiye aliyekuwa mwanzilishi wa kuonyesha vichekesho kupitia luninga, lakini bado alisimama kufanya maigizo ingawa alianza sanaa hiyo miaka 30 iliyopita na akiwa amefundishwa na Said Seif ‘Unono’ (ambaye kwa sasa ni marehemu).
Mbali na kushiriki sanaa katika vikundi mbalimbali, pia Mzee Small alicheza sanaa katika vikundi vya mashirika kama vile Reli, NASACO na mengine mengi, ambayo kwa sasa hayajihusishi tena na shughuli hizo.
Kuanza kupata umaarufu
Mzee Small alianza kujulikana sana katika fani ya uchekeshaji hasa pale alipoibuka na mchezo unaojulikana kama 50, 50, 100, na ule wa Mjini Shule unaomwelezea mwanamke mmoja wa kijijini aliyeolewa mjini.
Pia aliibuka na kitu kingine kiitwacho “Nani Kama Shule" huku akiwa amewashirikisha Majuto, Kingwendu na wachekeshaji wengine wanaotamba sasa nchini Tanzania.
Kundi binafsi na usanii wake
Mzee Small alikuwa akimiliki kundi lake la sanaa linalojulikana kama Afro Dance ambalo alilisajili mwaka 1994 kwenye Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na kupata usajili rasmi mwaka huo huo wa 1994.
NIPASHE