STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, December 17, 2014

Ander Herrera akanusha kupanga matokeo

http://www4.pictures.zimbio.com/gi/Manchester+United+v+Valencia+ODBuEmnisftx.jpg
KIUNGO wa klabu ya Manchester United, Ander Herrera amesisitiza kuwa hajawahi kushiriki zoezi lolote la upangaji matokeo wakati akiitumikia timu ya Real Zaragoza.
Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania ametajwa katika kundi la watu 41 wakiwamo  wachezaji, makocha na wakurugenzi katika uchunguzi wa kashfa ya upangaji matokeo katika Ligi Kuu nchini Hispania maarufu kama La Liga.
Herrera aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa facebook kuwa hajawahi na kamwe hatathubutu kujihusisha na suala la upangaji matokeo kwani anaupenda mchezo wa soka na anaamini katika mchezo wa haki ndani na nje ya uwanja.
Waendesha mashitaka katika kashfa hiyo wanadai kuwa fedha taslimu euro 965,000 zililipwa kwa kocha Javier Aguirre na wachezaji tisa wa Zaragoza, ikiwa ni pamoja na Herrera, kabla ya mchezo wa La Liga mwishoni mwa msimu wa 2010-2011.
Herrera aliondoka Zaragoza na kujiunga na timu ya nyumbani kwao ya Athletic Bilbao mwezi Agosti 2011, kabla ya kujiunga na United mwezi Juni 2014.
Wengine waliohuzsishwa na kadhia hiyo ni nahodha wa Atletico Madrid, Gabi na beki Montero na kocha wa zamani wa Zaragoza aliyepo Japan kwa sasa.

Waziri Ghasia akomaa, awafuta kazi wa chini yake

WAZIRI  wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Hawa Ghasia ametangaza kuwafuta kazi Wakurugenzi wa sita na wengine watano kuwasimamisha kutokana na matukio ya kuvurugwa kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliofanyikja Jumapili.
Pia Waziri Ghasia alisisitiza kuwa hawezi kujiuzulu kwa uzembe huo uliotia doa uchaguzi huo na badala yake amewaadhibu wa chini yake na jukumu la kujiuzulu analiacha kwa mamlaka iliytomteua licha ya kukiri uzedmbe uliofanywa na wasaidizi wake umelitia hasara taifa..
Akizungumza leo jijini Dar, Waziri Ghasia aliwataja wakurugenzi waliofutwa kazi ni Benjamin A Majoya aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mkuranga, Mkurugenzi Mtendaji wa Kaliua, Abdallah Ngodi, Masalu Mayaya wa Kasulu, Goody Pamba wa Serengeti, Julisu Madiga wa Sengerema na Simon Mayeye wa Bunda.
Wakurugenzi waliosimamishwa kazi ni Felix Mabuiga wa Hanang', Fortrunatus Fwema wa Mbulu, Isabela Chilumba wa Ulanga, Pendo Malabeja wa Kwimba na William Shimwela wa Sumbawanga Manispaa.
Waziri Ghasia alisema waliosimamishwa ni sababu ya kupisha uchunguzi na waliofutwa watapangiwa kazi nyingine za taaluma zao na kuongeza wakurugenzi wengine watatu wamepewa onyo kali.
Walioonywa niu Mohammed Maje wa Rombo, Hamis Yuna wa Busega na Ilala, Mvomero na Hai.
Uchaguzi huo uliofanyika Jumapili ulikumbwa na dosari mbalimbali zikiwamo kucheleweshwa kwa vifaa vya kupigia kura, karatasi kuwa na kasoro mbalimbali na kukwamisha kufganyika kwa uchaguzi kwa baadhji ya maeneo na kwingine kurudiwa.

Sikinde yapangua safu ya uongozi, Hemba 'aula'

BENDI kongwe ya muziki wa dansi nchini, Mlimani Park 'Sikinde' imepangua safu yake ya uongozi kwa kuunda Kamati Maalum inayoongozwa na wanamuziki watatu wa bendi hiyo.
Akizungumza na MICHARAZO, Katibu wa Kamati hiyo ya bendi, Abdallah Hemba alisema kuwa karibu mwezi mzima sasa bendi yao imepangua safu ya uongozi na kuunda kamati ambayo anaiongoza yeye na wenzake wawili.
Hemba alisema viongozi wenzake wanaoiongoza Sikinde ni mcharaza gitaa mahiri, Mjusi Shemboza na Ally Jamwaka.
"Kwa sasa Sikinde inaongozwa na Kamati maalum ambayo naiongoza mimi na akina Mjusi Shemboza na Ally Jamwaka," alisema Hemba ambaye ni muimbaji mahiri wa bendi hiyo.
Katika hatua nyingine, Hemba alisema kwa sasa bendi yao inasikiliza ofa toka kwa waratibu wa muziki kwa ajili ya shoo na mahasimu wao Msondo Ngoma.
"Bado hakuna hakika kama tutafanya shoo na Msondo ili tunasikiliza ofa, sisi tupo tayari wakati wowote kupambana na wapinzani wetu," alisema Hemba mmoja ya wanamuziki  waandamizi wa bendi hiyo iliyoanzishwa rasmi mwaka 1978.

Shamsa: Sikuwa naigiza, kipigo cha Simba kiliniliza Taifa

Shamsa Ford katika pozi
Shamsa akiangua kilio jukwaani wakati Yanga wakitungulia 2-0 na Simba
MUIGIZAJI nyota wa filamu nchini, Shamsa Ford ambaye alimwaga chozi wakati Yanga ikikandikwa mabao 2-0 na Simba, amesema hakuwa anaigiza 'kilio' isipokuwa uchungu wa kipigo ndiyo uliomfanya amwage machozi hadharani.
Shamsa, amesema yeye ni shabiki na mpenzi mkubwa wa Yanga kiasi kwamba amekuwa hakosekani kwenye mechi zao na kipigo hicho toka kwa Simba kilimuuma na kinaendelea kumuuma isivyo kawaida.
"Mungu wangu, kuna watu wamenipiga picha! Jamani...Ni kweli kipigo kiliniliza na kinaendelea kuniuma mpaka sasa...kwa nini iwe kwa Yanga tu kila mara," alihoji Shamsa.
Muigizaji huyo ambaye anatamba kwa sasa na filamu ya 'Chausiku' alisema mpaka sasa hajui kitu gani kilichoikuta Yanga kwenye uwanja wa Taifa katika pambano la Nani Mtani Jembe la kucharazwa mabao 2-0 ikiwa ni mara ya pili baada ya mwaka jana kunyukwa mabao 3-1.
Shamsa ni miongoni mwa waigizaji walio mashabiki wa Yanga, wengine ni Vincent Kigosi 'Ray' ambaye alikuwa na wakati mgumu juu ya matokeo hayo baada ya 'kupinga' na jacob Stephen Jacob 'JB' ambayer ni mnazi wa kutupwa wa Simba.

TANZIA! Mnenguaji Aisha Madinda afariki Dar

image
Aisha Madinda enzi za uhai wake
TASNIA ya sanaa imezidi kupata majozi baada ya aliyekuwa mnenguaji wa bendi za African Stars 'Twanga Pepeta' na Extra Bongo, Aisha Mohammed Mbegu 'Aisha Madinda' amefariki dunia mchana huu akiwa ndani ya Bajaj wakati akiwahi hospitali ya Mwananyamala.
Taarifa ambazo MICHARAZO imezipata zinasema kuwa Aisha Madinda alikodisha Bajaj na wakiwa kwenye foleni alikumbwa na mauti na mwili wake kwa sasa upo hospitali ya Mwananyamala ukiwa umehifadhiwa.
Akiongea na EATV Mkurugenzi wa bendi ya Twanga Pepeta amesema kuwa alipewa taarifa na daktari mmoja kuwa wameona kama mwili wa Aisha Madinda hospitalini hapo, ndipo akatuma watu kwenda kuangalia akiwemo Luiza Mbutu ili kuhakikisha kama kweli ni yeye ndipo walipogundua ni yeye.
“Mimi nipo njiani natoka Kigoma kuja Dar es Salaam, ni habari ya kusikitisha sana maana Aisha amefariki katika mazingira ya kutatanisha sana, jana alikuwa mzima na anachati na watu kwenye simu leo napigiwa simu mwili wake umekutwa umehifadhiwa kwenye hospitali ya Mwananyamala, hata sielewi nini kimetokea,” amesema Asha Baraka.
Hata hivyo taarifa ambazo hazijathibitishwa zinadai kuwa Madinda aliita dereva wa bajaj nma kuomba apelekwe Mwananyamala Hospitali na kukumbwa na mauti njiani bila dereva kujua mpaka akiwa hospitalini hapo.
Inaelezwa kuwa msiba wa marehemu Aisha uko Kigamboni na huenda akazikwa kesho huko huko.
MICHARAZO inaendelea kufuatilia na kitakachopatikana tutawafahamisha zaidi juu ya msiba huu ambao umekuja siku mooja tu baada ya Mkongwe Shem Ibrahim Karenga kufariki na kuzikwa jana jijini Dar.