Na Suleiman Msuya
TAASISI ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR)
imesema ipo kwenye majaribio ya dawa ya kudhibiti virusi vya Ukimwi ambayo
imegunduliwa na imewasilishwa kwenye taasisi hiyo na mmoja wa waganga wa jadi wa
hapa nchini.
Hayo yamebainishwa
na Mkurugenzi wa Kuratibu na Kukuza Utafiti NIMR Dk. Julius Massaga wakati
akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Habari Maelezo jijini Dar
es Salaam.
Dk. Mssaga alisema
mganga huyo wa jadi aliyegundua dawa hiyo ambayo imepewa jina la warburgistat
aliitunza katika vifungashio vya kawaida ambapo NIMR wao wameweza kufanyia
maboresho kwa kuitengenezea kwenye mfumo wa vidonge.
Alisema kulingana
na taarifa za Mganga huyo wagonjwa 20 wa awali ambao walitumia dawa hiyo
wamepona kabisa na hamna madhara yoyote ambayo yamepatikana.
"Tunapenda
kuwaambia watanzania kuwa ipo dawa ya kudhibiti virusi vya ukimwi ambayo
iliwasilishwa NIMR na baada ya kuifanyia uchunguzi tunapata matumaini kuwa
inaweza kufanya kazi hiyo,'' alisema.
Mkurugenzi huyo wa
Kuratibu na Kukuza Utafiti NIMR alisema dawa hiyo wameiwasilisha Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ambapo
wanatarajia baada ya uchunguzi wataingiza sokoni ili iweze kutumika rasmi.
Alisema NIMR
imekuwa ikishirikiana na nchi zingine mbalimbali kama Afrika Kusini na
Swaziland katika kufanya utafiti dhidi ya dawa asili ambazo zimekuwa zikileta
matokeo makubwa kwa jamii.
Dk. Massaga alisema
NIMR inawakaribisha waganga wa jadi ambao wana amini kuwa wana dawa ambazo zinaweza kusaidia jamii ili wao waweze
kuzifanyia utafiti kwa uthibitisho zaidi.
Mkurugenzi huyo
alisema pamoja na dawa hiyo pia wamefanikiwa kuboresha dawa za tiba asili kwa
ajili ya matumizi ya binadamu kama vile TMS 2001 tiba ya malaria, hepacure
inatibu ini, persician tiba ya kisukari, persivin tiba ya tezi dume, nimrex
tiba ya kikohozi na nimrevit kinywaji kinachoboresha afya ya kuongeza damu.
Pia alizitaja dawa
zingine ni mundex dawa ya kuongeza nguvu jinsia ya kiume, fukuza mbu dawa ya
kupakaa inayofukuza mbu,usambara balm dawa ya kupaka kwa ajili ya kutuliza homa
na mafua,usambara mosquito repellent mshumaa unafukuza mbu na takasa maji tiba
ya maji ya kunywa dhidi ya vimelea vya magonjwa yakiwemo ya kuhara na homa ya
matumbo.
Kwa upande mwingine
Dk. Massaga alisema NIMR inakabiliwa na changamoto mabalimbali kama kukosekana
kwa uhamasishaji na uwezeshaji katika eneo la kilimo cha miti dawa hali ambapo
inasababisha ukosefu wa dawa asili.
Changamoto nyingine
ni kukosekana na mitaala ya wataalamu wa tiba ya kisasa (madaktari, wafamasia
na manesi) ambao wamenyimwa fursa ya kuelewa kwa kina na kupata maarifa juu ya
tiba asilia na matumizi yake katika tiba.
Aidha changamoto
nyingine ni uhusiano mdogo kati ya watafiti, wataalamu wa tiba asilia na tiba
ya kisasa katika suala zima la tiba asili na kutokuwepo kwa orodha ya miti dawa
na taarifa ya matumizi yake katika tiba na maingiliano yake na dawa za kisasa.
Dk. Massaga alisema
pamoja na changamoto hizo NIMR inatarajia kusajili dawa na kiwanda kabla ya
uzalishaji katika mwaka huu wa fedha, kuanzisha uzalishaji wa kati wa dawa za
asili kulingana na mahitaji na kuuingiza dawa asali katika mfumo wa tiba.
Hata hivyo alisema
katika mwaka wa fedha wa 2013/14 serikali imetenga kiasi cha sh800 milioni kwa
ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuboresha tiba asilia pamoja na mitambo ya
kuzalishia dawa hizo.
Ambapo kwa sasa
serikali imeikabidhi NIMR mitambo midogo ya daraja la kwanza ya utendenezaji wa
dawa asili kwa matumizi ya binadamu na kujenga kiwanda cha daraja la kwanza cha
kisasa kwa ajili ya utafiti na utengenezaji wa tiba asili katika eneo la Mabibo
jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake
Mtafiti Mwandamizi wa NIMR Hamis Malebo alitoa wito kwa wananchi kuwa makini na
ongezeko la baadhi ya watu ambao wanajiita waganga wa jadi.
Alisema kwa muda
sasa hasa katika jiji la Dar es Salaam kumekuwepo na ongezeko kubwa la watu wa
aina hiyo hali ambayo inahatarisha maisha ya wananchi ambao wamekuwa wakitumia
dawa hizo.
"Jamani kuweni
makini wapo watu (matapeli) ambao wapo tayari hata kutumia mapumba ya mbao
kuwapa watu kama dawa jambo ambalo si sahihi hata kidogo," alisema.