STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, January 29, 2014

Libya yatangulia fainali za CHAN 2014, Zimbabwe yafa kiume!

Libya vs Zimbabwe
LICHA ya kukomaa kwa muda wa dakika 120 na kulazimisha pambano lao la Nusu Fainali dhidi ya Libya kuingia hatua ya kupigiana penati, Zimbabwe imejikuta ikikwama kufuzu Fainali ya CHAN 2014.
Zimbabwe iliyofuzu  kimiujiza kwenye hatua ya mtoano, ilijikuta ikilala kwa mikwaju 5-4 dhidi ya Libya iliyotangulia kwenye fainali na kusubiri mshindi wa mechi ya nusu fainali ya pili kati ya Nigeria na Ghana.
Pambano hilo la Nigeria na Ghana linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa kandanda barani Afrika linatarajiwa kuanza muda mfupi baadaye na timu yoyote ikifanya vema itaunga na Libya kusubiri kupepetana Jumamosi.
Mshindwa katika mechi hiyo atakutana na Zimbabwe mapema siku hiyo ya Jumamosi kucheza pambano la kuwania nafasi ya tatu.
Katika pambano la Zimbabwe na Libya lilikuwa kali na timu zote zilifanya kosa kosa za hapa na pale, huku zikibadilisha wachezaji kwa nia ya kuongeza nguvu vikosi vyao, lakini dakika 90 zilimalizika na hata zile 30 za nyongeza nazo ziliisha patupu ndipo ikafuata hatua ya kupigiana penati.
Kwenye hatua ya penati Libya ilipata penati zake kupitia kwa Elmutasem Abushnaf, Mohamed Al Ghanodi  Abdelrahman Fetori, Mohamed Elgadi na Mohamed Fathi Abdaula, huku Mohamed Mahfudh, Ali Salama
na Motasem Sabbou walikosa penati zao.
Zimbabwe ilipata mikwaju yake kupitia Eric Chipeta, Danisa Phiri, Hardlife Zvirekwi na Patson Jaure, huku Simbarashe Sithole, Peter Moyo, Milton Ncube na Ali Sadiki walikosa penati zao.

TASWA kuchaguana Februari 16

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhf0BHUHvIcL5-2NP5BJ1cLGd-dO7nkX4M6QQQQ1juGpgd4p19qMpmQJ-7rGHrMW7-u3bn6Oy2uDW3HDTt5h0-0pXsaq3YjJigDZwWW1xCe4mwGMvqtctAng9pJasFadQ85OFyN9NuOFJ4/s640/amii+mhando.jpg
Makatibu wa TASWA wanaomaliza muda wao, George John na Amir Mhando

UCHAGUZI Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), utafanyika Februari 16 mwaka huu jijini Dar es Salaam kama ulivyopangwa na Kamati ya Utendaji ya chama.
 
Hata hivyo sekretarieti ya TASWA imekubaliana kusogeza mbele muda wa kulipia ada kwa wanachama hadi Jumanne Februari 4 mwaka huu, badala ya Ijumaa Januari 31, 2014 iliyokuwa imepangwa awali, lengo likiwa ni kuwezesha wanachama wengi zaidi kulipia ada zao ili waweze kushiriki uchaguzi huo.
 
Wanachama wote walioshiriki uchaguzi wa mwaka 2007 ama 2010 au Mkutano Mkuu wa mwaka 2012 wana sifa ya kushiriki uchaguzi huo wanachotakiwa kufanya ni kulipia ada zao kuanzia mwaka 2011.
 
Malipo yafanywe kwa Mhazini Msaidizi, Mohammed Mkangara, 0658-123082 na hakuna mwanachama mpya atakayekubaliwa kujiunga na chama kwa sasa mpaka baada ya Uchaguzi Mkuu.
 
Nawasisitiza wanachama kuhakikisha wanatumia vizuri muda uliobaki kwa kulipia ada zao ili waweze kushiriki mkutano huo. Kamati ya Uchaguzi ya TASWA inatarajiwa kukutana Jumatatu ijayo kuzungumzia mambo mbalimbali yahusiyo uchaguzi huo.
 
 Nawasilisha.
 
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
29/01/2014.

Huyu ndiye msanii aliyejinyonga Gesti baada ya kuigiza filamu


 
 Marehemu Victor Peter enzi za uhai wake.
****
MSANII Victor Peter kutoka Bongo Movie amefariki dunia usiku wa juzi kuamkia jana 28/01/2014 kwa kujinyonga katika nyumba ya wageni (guest House) moja iliyotambulika kwa jina la SAFARI JUNIOUR iliyoko maeneo ya Kisosora mkoani Tanga.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Bombo mkoani Tanga .

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mmoja kati ya wasanii walioshirikishwa na marehemu katika filamu yake ya mpya ya mwisho inayokwendakwa jina la Chozi, aliyokuwa akirekodi kabla ya kujinyonga, ambayo hadi sasa  bado haijatoka, Msanii huyo aliyetambulika kwa jina la Koba alisema kuwa 
''Siku moja kabla ya tukio hilo Victor, alifanya nao Shooting ya filamu iliyotambulika kwa jina OUR FAMILY ambayo ilikuwa ndio filamu ya pili ya marehemu Victor tangu ajikite katika tasnia ya filamu Bongo Movie.

Filamu hiyo mhusika mkuu alikuwa ni marehemu Victor na katika filamu  alicheza scene inayohusu msiba wa baba yake aliyefariki na yeye mwenyewe mwisho wa filamu alijinyonga.

Baada ya kumaliza zoezi hilo la kurekodi filamu, marehemu aliondoka na wasanii kadhaa wakaelekea katika ATM iliyo maeneo ya mjini kwa ajili ya kutoa hela ili awalipe wasanii waliohusika katika kazi yake.

Akiwa katika ATM hiyo, mtandao ulikuwa ukisumbua na wakati akisubiri  kusubiria mtandao ukae sawa marehemu Victor alibadilika na kuonekana kama amechanganyikiwa, na baada ya muda ATM ilianza kufanya kazi na  akatoa hela wakaelekea Hospitali ya Ngamiani mkoani Tanga, Kufika Ngamiani daktari akatoa tamko kwamba apelekwe Hospitali kuu Bombo.

Hospitali ya Bombo akapimwa kila kitu na kukutwa mzima asiye na tatizo lolote, ikabidi warudi Gest walikofikia maeneo ya Kisosora, Marehemu akawalipa wasanii wote na kuwauliza kuwa kuna mtu anayemdai? 

Wakamjibu hakuna. Kila msanii akaingia chumbani kwake na kuendelea na ratiba binafsi na marehemu aliingia chumbani kwake.

Asubuhi yakuamkia jumanne 28/01/2014 Wasanii wenzake walimgongea mlango wakaona kimya wakapatwa na wasiwasi ikabidi wamuite mwenye nyumba hiyo ya wageni, ambapo alichukua uamuzi wa kutoa taarifa kwa mwenye kiti wa Serikali za mitaa mwenye kiti akatoa taarifa Polisi, Gari ya Polisi ikatia timu katika eneo la tukio na kuvunja mlango, ambapo walimkuta akiwa tayari ameshafariki dunia mwili ukiwa umening'inia'', alisimulia mmoja kati ya wasanii hao.

 M/mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema.

Yanga yashushwa kileleni, Azam yazidi kupaa, Mbeya City yabanwa Mlandizi


MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga a.k.a Wazee wa Uturuki wameshushwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kulazimishwa suluhu na Coastal Union jijini Tanga huku Azam ikipata ushindi mwembamba na kukalia kiti.
Bao pekee lililofungwa na Kipre Tchetche limeiwezesha Azam kufikisha pointi 33 baada ya kupata ushindi mbele ya Rhino Rangers ya Tabora.
Pointi hizo ni moja zaidi ya za Yanga ilitoka suluhu na Coastal katika pambano kali lililochezwa Mkwakwani.
Nayo Mbeya City ilipunguzwa kasi na Ruvu Shooting baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye uwanja wa Mabatini, Mlandizi ikiwa ni pointi ya kwanza kwa kocha Tom Olaba tangu aanze kuinoa Ruvu.
Ruvu walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Jerome Lembeni kabla ya Jeremia John kusawazisha. Mabao yote yakifungwa katika dakika 15 za awali za kipindi cha kwanza.

Hivi ndivyo MCD alivyokuwa akienda kupumzishwa leo





PICHA TOFAUTI ZINAZOONYESHA JENEZA LA MCD LIKIELEKEA MAKABURINI NA BAADA YA KUZIKWA KATIKA MABAKURI YA NJORO MJINI MOSHI

Athuman Idd 'Chuji' arejeshwa kikosini Yanga

Athuman Idd 'Chuji' aliyerejeshwa kikosini Yanga

KIUNGO mkabaji wa timu ya Young Africans Athuman Idd Athuman "Chuji" amerejeshwa kundini kuungana na wachezaji wenzake baada ya awali kuwa amesimamishwa na uongozi kutona na kitendo cha utovu wa nidhamu aliouonyesha mwishoni mwa mwaka jana.
Athuman Idd "Chuji" alisimamishwa na uongozi na Young Africans baada ya kuonyesha utovu wa nidhamu na kuamua kuondoka vyumbani kuelekea nyumbani kabla ya mchezo kumalizika kitu ambacho alikiri ni makosa mbele ya uongozi.
Kwa mujibu wa mtandao wa klabu hiyo ni kwamba uongozi wa Young Africans ulifikia kumpa barua ya kumsimamisha Chuji ambaye alikiri kufanya kosa hilo na kisha kukiri mbele na kuandika barua ya kuomba msamaha na kuahidi kutorudia tena kitendo hicho au kufanya kitendo kingine chochote cha utovu wa nidhamu.
Baada ya kuandika barua kwa uongozi kuomba msamaha, Chuji alipewa onyo kali na uongozi na kupewa kipindi cha matazamio ambapo kwa kipindi cha mwezi mmoja ameonekana kubadilika na kurejea katika nidhamu ya hali ya juu ndani na nje ya uwanja. 
Chuji ataungana na kikosi cha Young Africans keshokutwa kitakapo rejea jijini Dar es salaam tayari kwa mikikimikiki ya Ligi Kuu pamoja na mashindinao ya Klabu Bingwa Afrika ambayo yanatarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki ijayo kwa Young Africans kuanza na timu ya Komoronize ya Visiwa vya Comoro.

Easy Man ayarudia Mashetani


MSANII anayetajwa kama mfalme wa mchiriku kwa sasa nchini, Is'haka Saleh 'Easy Man' ameurejea upya wimbo wake wa 'Mashetani', huku akijiandaa kuutolea video yake.
Akizungumza na MICHARAZO, staa huyo wa wimbo wa 'Kasoro Wewe' ameurudia wimbo huo baada ya kupewa ushauri kwamba awali haukuwa na kiwango kizuri.
Easy alisema baada ya ushauri huo aliamua kurejea tena katika studio za Natal Records zilizopo Mburahati.
"Nimeamua kuurejea tena wimbo wa 'Mashetani' kuurekodi wimbo huo pale Natal Records chini ya Abba Process. Yaani wacha nijisifie kwa jinsi nilivyoomba, ni bonge la wimbo," Easy alisema.
Easy alisema wimbo huo atauachia rasmi hewani wikiendi hii wakati akianza mchakato wa kufyatua video yake.
"Natarajia kuiachia mwishoni mwa wiki wakati nafanya mchakato wa kurekodi video yake ili kusuuza roho za mashabiki wangu," alisema Easy.
Hata hivyo, Easy hakuweza kubainisha video hiyo ataitoa kupitia kampuni gani, ila alisema itafanywa mapema iwezekanavyo

Cheka kutoa 'hogo' leo, akijianda kuwania ubingwa wa dunia

WAKATI Francis Cheka akitarajiwa kutoa 'hogo' alililofungwa kwenye mkono wake wa kulia leo, bondia huyo sasa atapigana na mpinzani wake kutoka Russia, Valery Brudov kuwania ubingwa wa dunia wa WBF uzito wa Lightheavy.
Cheka aliumia mkono huo katika maandalizi ya pambano lake dhidi ya Brudov ambalo awali lilipangwa kufanyika Februari 8, lakini sasa limesogezwa mbele hadi Machi Mosi.
"Cheka anatarajiwa kutolewa plasta gumu (P.O.P) mkononi na kuangaliwa hali yake na daktari kesho (leo) na kama maendeleo yake ni mazuri ataanza kujifua kwa ajili ya pigano lake Machi Mosi," alisema Msangi.
Mratibu wa pambano hilo, Juma 'Jay' Msangi' aliiambia MICHARAZO kuwa, Cheka anatarajiwa kutolewa 'hogo' hilo leo kabla ya kuanza maandalizi ili kujiweka fiti kwa pambano hilo litakalofanyika ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam.
Msangi alisema tofauti na ilivyokuwa awali, pambano la Cheka na Brudov sasa litakuwa la kuwania ubingwa wa dunia uzani wa kilo 82 (Light Heavy Weight) na imani yake bingwa huyo wa IBF Afrika atawatoa kimasomaso Watanzania.
Aidha, mratibu huyo alisema mapambano mengine yaliyokuwa yamepangwa kuchezwa Februari 8 yatafanyika kama ilivyopangwa na sasa pambano la bondia Francis Miyeyusho na Victor Chornous kutoka Ukraine ndilo litakalokuwa pambano kuu siku hiyo.
Msangi alisema licha ya pambano la Miyeyusho, bingwa wa kimataifa wa UBO uzito wa Bantam pia siku hiyo kutakuwa na michezo mingine kadhaa ya utangulizi likiwemo la Mohamed Matumla dhidi ya Nassib Ramadhan.
Mabondia hao wawili walipigana hivi karibuni kuwania pikipiki na Matumla ambaye ni mtoto wa bingwa wa zamani wa WBU, Rashid Matumla 'Snake Man', aliibuka kidedea dhidi ya mpinzani wake na kunyakua 'bodaboda' hiyo.

Arsenal yabanwa, Liverpool ikiua, Mata aibeba Mashetani Wekundu

Arsena wakishangilia bao lao
Manchester United wakishangilia bao la kwanza

Nyota wa Liverpool wakipongezana

WAKATI Arsenal iking'ang'aniwa na 'vibonde' Southampton, huku Liverpool wakitoa kichapo cha aibu kwa wapinzani wao wa jadi, Everton, Juan Mata ameanza kibarua chake vyema kwa Mashetani Wekundu baada ya kuisaidia kupata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Cardiff City.
Arsenal iliyokuwa ugenini imejikuta ikipata sare hiyo ugenini huku ikimpoteza kiungo wake Flamin aliyeoonyeshwa kadi nyekundu na kufanya ishindwe kuwakimbia Manchester City ambayo leo itashuka dimbani na iwapo itashinda itakalia kiti cha uongozi kinachoshikiliwa na The Gunners kwa sasa.
Mathieu Flamini alionyeshwa kadi ya moja kwa moja na kuifanya Arsenal icheze pungufu, huku wenyeji wakitangulia kupata bao la kwanza lililofungwa na Jose Fonte dakika ya 21 bao lilidumu hadi wakati wa mapumziko kabla ya kipindi cha pili kuanza kwa Oliver Giroud kuisawazishia Arsenal bao dakila ya 48.
Santi Cazorla aliipa uongozi vijana wa Arsene Wenger dakika ya 52 kabla ya Adam Lallana kusawazisha dakika mbili baadaye na kuifanya Arsenal iendelee kukaa kileleni ikiwa na pointi 52, moja pungufu na Man City itayocheza na Tottenham Hotspus ugenini.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo ya England, Liverpool iliiadhibu Everton kwa kuilaza mabao 4-0 mabao yaliyofungwa na nahodha Steven Gerrard, Daniel Sturridge aliyetupia mawili na jingine na kinara wa mabao  Luis Suarez.
Manchester United ikiwa uwanja wa nyumbani ilipata ushindi wa mabao 2-0 huku nyota wake mpya, Juan Mata aliyesajiliwa kutoka Chelsea akionyesha thamani halisi ya fedha alizonunuliwa kwa kuisaidia timu yake kuwafunika Cardiff City.
Mabao ya Robin van Persie na jingine ya Ashley Young yalitosha kumfariji kocha David Moyes ambaye amekuwa hana amani kwa kipindi kirefu tangu aanze kuinoa timu hiyo akitokea Everton.
Mechi nyingine zilishuhudia Swansea City ikiifunga Fulham kwa mabao 2-0, Crystal Palace wakishinda nyumbani vao 1-0 dhidi ya Hull City na Norwich City na Newcastle United walitoka suluhu ya 0-0.
Ligi hiyo itashuhudiwa ikiendelea tena leo kwa michezo kadhaa ukiwamo wa Spurs dhidi ya Manchester City, Aston Villa itakwaruzana na West Bromwich, huku Sunderland  itaikaribisha Stoke City na Chelsea itaumana na West Ham United.
Msimamo wa Ligi unaonyesha Arsenal wanaoongoza wakiwa na pointi 52 kwa michezo 23, ikifuatiwa na Man City yenye 50 na Chelsea ni ya tatu na pointi zake 49, huku LIverpool ikifuatia na pointi 46 baada ya ushindi wa jana.