|
Simon Msuva akionyesha makali yake. Juu kikosi cha Yanga (Picha zote kwa hisani ya Bin Zubeiry |
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Yanga, Mbrazil Genilson Santos 'Jaja' ameendelea kuwapa raha wana Yanga baada ya kuifungia bao pekee lililowapa vijana wa Jangwani ushindi wao wa nne mfululizo ikiwa chini ya kocha Marcio Maximo katika pambano la kirafiki la kimataifa dhidi ya Thika United ya Kenya.
Mechi hiyo iliyochezwa jana kwenye uwanja wa Taifa, ilishuhudia Jaja akiifunga bao hilo katika kipindi cha pili na kuwafanya mashabiki waliokuwa wakitaka mchezaji huyo atolewe dimbani kunyamaza kimyaa.
Jaja alifunga goli hilo akimalizia kwa kuugusa kidogo tu mpira wa krosi murua ya dakika ya 58 kutoka kwa winga Simon Msuva ambaye jana alichezeshwa kama straika wa kati.
Goli hilo liliibua shangwe kwa mashabiki wa Yanga ambao walikuwa kimya katika kipindi cha kwanza kutokana na ubovu uliooneshwa na safu yao ya ushambuliaji ikiongozwa na Mbrazil huyo katika kipindi hicho.
Yanga waliokuwa wameweka kambi ya siku 10 visiwani Zanzibar wakicheza mechi za kirafiki tatu na kushinda zote dhidi ya Chipukizi FC, Shangani FC na KMKM zote za Ligi Kuu ya Zanzibar, walianza mechi hiyo kwa mpira wa polepole uliochagizwa na pasi fupifupi za mfumo wa Kibrazil wa kocha Marcio Maximo.
Kikosi cha kwanza cha Yanga kilichoanza na wachezaji wawili wapya kutoka Brazil, Andrey Coutinho na Genilson Santos 'Jaja' kilimaliza kipindi cha kwanza kikiwa hakijafunga goli hata moja, sawa na wageni wao Thika United waliomaliza msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Kenya wakiwa nafasi ya tano.
Katika kipindi hicho cha kwanza, kiungo wa kimataifa wa Yanga kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima 'Fabregas' alionyesha kiwango cha juu hasa katika dakika 30 za mwanzo akifuatwa na Coutinho ambaye alionekana wazi kuwa kivutio kikubwa cha Wanayanga kutokana na chenga zake za Kibrazil zilizojaa kila aina ya fedheha.
Kabla ya mechi hiyo kuanza, Maximo aliyekuwa anaingia kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa akiwa kocha wa Yanga baada ya kuiongoza kwa mafanikio timu ya taifa (Taifa Stars), aliwanyanyua vitini wapenzi na mashabiki wa Yanga baada ya kuonyesha ishara ya ngumi ambayo ilitafsiriwa kama amedhamiria kurudisha magoli 5-0 ambayo Yanga ilipokea kutoka kwa watani wao wa jadi, Simba misimu mitatu iliyopita.
Maximo, kocha wa zamani wa Stars, aliendelea kuwa kivutio zaidi pale alipojishika kifuani na kutoa ishara kwamba 'anaweza' kuipa mafanikio zaidi timu ya Yanga.
Mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Hashim Abdallah kutoka Dar es Salaam ambaye ana daraja la kwanza la uamuzi, ilishuhudiwa Maximo akibadilisha wachezaji kadhaa kipindi cha pili akiwatoa Jaja, Dilunga, Niyonzima, Coutinho na Msuva na kuwaingiza Hamis Thabit, Omega Seme, Said Bahanunzi na Nizar Khalfan ambao walibadilisha kwa kiasi kikubwa mechi hiyo na kuifanya iwe kivutio kwa Wanayanga.
Kulikuwa na idadi kubwa ya mashabiki hasa wa Yanga waliofurika upande wa Magharibi na Kusini mwa Uwanja wa Taifa huku baadhi ya mashabiki wa Simba wakikaa kwenye jukwaa lao la Kaskazini mwa uwanja huo na kuendelea upinzani wao wa jadi dhidi ya Yanga kwa kuipa sapoti timu ngeni ya Thika United.
ilikuwa ni mechi ya nne ya kirafiki ya Yanga chini ya Maximo na ya kwanza kwa kocha huyo Mbrazil kwenye Uwanja wa Taifa tangu aanze kuifundisha klabu hiyo.
Kocha Maximo alisema baada ya mechi hiyo jana kuwa timu yake inapaswa kubadilika na kutumia nafasi zinazopatikana huku pia akiisifu Thika United akisema ilicheza vizuri kuliko wao licha ya Wanajangwani kuibuka na ushindi.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema jana kuwa baada ya kushinda mechi zao zote nne za kirafiki wanaangalia uwezekano wa kucheza mechi nyingine moja ya kujipima kabla ya kuwavaa Azam FC katika pambano lao la kuwania Ngao ya Jamii la kuashiria ufunguzi wa pazia la Ligi Kuu ya Tanzania Bara Septemba 13.
Vikosi:
Yanga: Deogratius Munishi 'Dida', Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima/ Hussein Javu (dk 73), Hassan Dilunga/ Hamis Thabiti (dk. 46), Genilson Santos 'Jaja' (Said Bahanunzi (dk 75), Simon Msuva/ Omega Seme (dk 73) na Andrey Coutinho/ Nizar Khalfan (dk. 70).
Thika United: Hamza Muwonge, Simon Mbuguo, Sammy Meja, Tonny Kizito, Dirkir Glau, Dennis Odhiambo, Moses Odhiambo, Wyclif Opondo, Michael Olunga, David Kingatua na Joseph Kulia.