BENDI kongwe ya muziki wa dansi nchini, Mlimani Park 'Sikinde' imefytua nyimbo mbili mpya maalum kwa ajili ya kuwahamasisha wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kwa neema walizojaliwa.
Kwa mujibu wa Katibu wa Sikinde, Hamis Mirambo nyimbo hizo ni 'Fursa Zimefunguliwa' na 'Neema Kubwa ya Gesi' ambazo tayari zimeshasambazwa ili kurushwa hewani.
Mirambo aliiambia MICHARAZO nyimbo hizo zimetungwa maalum kwa ajili ya kuwahamasisha na kuwaelimisha wakazi wa mikoa hiyo juu ya neema zilizogundulika katika mikoa yao ikiwamo Gesi.
"Ni nyimbo ambazo za kuhamasisha na kuelimisha juu ya wakazi wa mikoa hiyo ya Kusini mwa Tanzania kuitumia vyema neema na fursa zilizopo katika mikoa yao kujiletea maendeleo," alisema.
Mirambo aliongeza kuwa bendi yao tayari imekamilisha nyimbo za albamu yao mpya na wanajipanga kwa ajili ya kuzizidua sambamba na kuzitengenezea video zake.
Albamu hiyo itakayofahamika kama 'Jinamizi la Talaka' itakuwa na nyimbo saba badala ya sita ilivyozoeleka kwa albamu za bendi za muziki wa dansi.
Pia, alidokeza kuwa kuanzia sasa siku ya Jumamosi watakuwa wakitoa burudani kwenye ukumbi wa Wipes Bar Bandari, Kurasini huku siku ya Ijumaa kama kawaida wanakamua Break Point, Posta Mpya na Jumapili uwanja wa nyumbani wa DDC Kariakoo.
No comments:
Post a Comment