STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, December 29, 2012

RIDHIWANI APONDA MFUMO UENDESHAJI YANGA ADAI AFADHALI WA SIMBA

Ridhiwani akihutubia Waandishi asubuhi ya leo Kiromo Hotel

Na Mahmoud Zubeiry, Bagamoyo
MWENYEKITI wa Kamati ya Kusaidia timu za soka za vijana za taifa, Ridhiwani Kikwete, amesema mfumo wa uendeshwaji wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam ni mbovu kwa sababu unategemea mfuko wa mtu mmoja.
Akizungumza wakati anatoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Hoteli ya Kiromo, Bagamoyo mkoani Pwani, Kikwete alisema kwamba Yanga inahitaji kubadilika kutoka mfumo huo.
Kikwete alisema ni afadhali mfumo wa uendeshwaji wa Simba SC, ambao desturi yao ni kuchangishana.
“Nilijaribu kufanya uchunguzi wa mfumo wa uendeshwaji wa klabu ya Yanga, nikashangazwa ni mfumo mbaya, kwa sababu unategemea mfuko wa mtu mmoja, afadhali Simba wao huwa wanachangishana,”alisema.
Ingawa hakumtaja mtu ambaye mfuko wake unategemewa Yanga, lakini wazi ni Mwenyekiti wa klabu hiyo, Alhaj Yussuf Mehboob Manji.
Kwa ujumla katika hotuba yake, Kikwete alisema haridhishwi na mfumo wa uendeshwaji wa soka ya Tanzania na kwamba unahitaji mabadiliko.
Kikwete aliushauri uongozi wa TASWA upiganie nafasi ya uwakilishi ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kusisitiza juu ya umuhimu wa waandishi nchini kutambua haki zao.
Lakini pia Kikwete aliwaasa waandishi kuepuka uandishi wa kinazi wa Simba na Yanga na badala yake kuzama ndani zaidi katika kuripoti, sambamba na kuripoti michezo yote, badala ya kuegemea kwenye soka pekee.
“Vyombo vya habari lazima viwe na wataalamu tofauti wa kuripoti michezo tofauti, huyu akiegemea kwenye soka, mwingine aegemee kwenye mchezo mwingine, ili kuhakikisha tunafikisha ujumbe vema kwa jamii,” alisema mtoto huyo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Ridhiwani ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, NEC akiiwakilisha Wilaya ya Bagamoyo alisema kwamba ipo haja ya TASWA kuendesha semina kadhaa za kuelimisha Waandishi wa Habari kuweza kuripoti michezo mbalimbali nchini.  
Aidha, katika mkutano huo, wanachama walielimishwa kuhusu uanzishwaji wa Saccos na kuridhia kuanza kwa mchakato wa kuundwa kwa chama cha ushirika wa akiba na mikopo kwa Taswa. Walipendekezwa wajumbe waunde timu ya mpito.

CHANZO:BIN ZUBEIRY

KOCHA  SIMBA KUTUA LEO KUSHUHUDIA MECHI YAO NA TUSKER


KOCHA mpya wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba SC, Mfaransa Patrick Liewig anatarajiwa kuwasili leo nchini na atakuwapo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuishuhudia timu hiyo ikimenyana na mabingwa wa Kenya, Tusker FC.
Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga amesema kwamba, awali kocha huyo alitarajiwa kuawasili nchini juzi, lakini ilishindikana baada ya kukosa nafasi kwenye ndege na sasa mashabiki wa timu hiyo wamtarajie leo.
Alisema kocha huyo ambaye anakuja kurithi mikoba ya Mserbia Profesa Milovan Cirkovick, atakishuhudia kikosi cha Simba kikicheza mechi hiyo kabla ya kuendelea na taratibu nyingine ikiwemo kusaini mkataba wa kazi na baadaye kuanza kutumikia kibarua chake kipya.
Liewig ni kocha wa zamani wa Akademi ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa, ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Club Africain ya Tunisia, Patrick Liewig na ana Stashahada ya Juu ya ukocha na Shahada ya tatu ya ualimu wa soka ya vijana aliyotunukiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ufaransa, Gerard Houiller na amehudhuria pia kozi za ufundishaji mazoezi ya viungo Juni mwaka 1999 katika Chuo Kikuu cha Dijon.
Kwa upande wa uzoefu, Liewig alifanya kazi PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 kama Kocha Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa pia katika programu za timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa Under 20, Under 18 aliowawezesha kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na Under 16.
Kuanzia mwaka 1989 hadi 1990:  alikuwa Meneja Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa Henri Michel, 1991 hadi 1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa Msaidizi wa Luis Fernandez, 1996 hadi 1998: alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998 hadi 1999 alikuwa Msaidizi wa Alain Giresse.
Liewig pia alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi 2001, ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.
Januari mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika fainali za Afrika za U20 nchini Burkina Faso.
Kuanzia mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast aliyoipa mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005 na 2006, Super Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu Fainali.
Amekuwa Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004, 2005 na 2006 na tangu Septemba mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa Club Africain ya Tunisia
Kuelekea mchezo wa leo, Simba itamenyana na Tusker FC ambayo ilianza vema ziara yake nchini, baada ya kuichapa Yanga 1-0 katika mchezo ulipigwa kwenye Uwanja wa Taifa Jumatano.
Simba SC na Tusker zinatarajiwa kukutana pia kwenye Kundi la Mapinduzi visiwani Zanziabr hivi karibuni, kwani zimepangwa kundi moja, A pamoja na Bandari ya Unguja na Jamhuri ya Pemba.
Aidha, katika Kundi B, washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Bara, Azam FC ya Dar e Salaam pia, imepangwa na Mtibwa Sugar ya Morogoro, Coastal Union  ya Tanga na Miembeni ya Unguja.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambayo ni maalum kwa ajili ya kuherehekea Mapinduzi matukufu ya Zanzaibar, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 2, hadi kilele cha miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, mwakani, huku ikishirikisha timu kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo iliyotolewa na Kamati Maalum ya Kusimamaia michuano hiyo, inaonesha kuwa katika mchezo wa kwanza utakaochezwa siku ya ufunguzi itakuwa ni kati ya Bandari kutoka Unguja ambayo itacheza na Jamhuri kutoka kisiwani Pemba ambao ni wawakilishi wa Zanzibar katika Kombe la Shirikisho Barani Afrika, pamabanolitakalochezwa katika uwanja wa Mao Tse Tung mjini Unguja, huku usiku wa siku hiyo hiyo katika Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja pambano la ufunguzi rasmi katika mashindano hayo likiwakutanisha mabingwa wa soka nchini Tanzania, Simba SC ambao watapambana na mabingwa wa soka nchini Kenya, Tusker.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo jumla ya timu nane zitashiriki katika mashindano hayo ambayo yamejipatia umaarufu mkubwa visiwani hapa, timu hizo zimegawanya katika makundi mawili ambayo ni kama ifuatavyo:
Awali michuano hiyo ilitarajiwa kuanza kisiwani Pemba tarehe 1 Januari, lakini kutokana na kujitoa katika mashindano kwa klabu ya Al-Ahly ya Misri kutokana na klie kilichoelezwa sababu za kiusalama, mechi zote sasa zitachezwa kisiwani Unguja na ufunguzi ukipangwa kuanza tarehe 2 badala ya tarehe 1 januari.
Bingwa wa michuano hiyo ataondoka na zawadi ya kombe na fedha taslim Tsh.Milioni kumi (10,000,000), mshindi wa pili Milioni tano (5,000,000), pamoja na zawadi nyengine ambazo zimegawanywa katika makundi tofauti ikiwemo zawadi ya mfungaji bora, mchezaji bora, mwamuzi bora, kipa bora, mwandishi wa habari bora, timu bora na zawadi nyinginezo.

Masai Nyota Mbof adai 2012 ulikuwa nomaa!

Masai Nyota Mbof

MCHEKESHAJI anayejitosa kwenye fani ya muziki nchini, Gilliad Severine 'Masai  Nyota Mbofu', amesema mwaka 2012 utakabaki kuwa wa mchungu kwake kutokana na matukio ya kusikikitisha yaliyotokea ndani ya mwaka huo.
Masai anayejiandaa kufyatua wimbo mpya wa 'Masai ya Wapi' akishirikiana na rapa Kalidjo Kitokololo, alisema vifo na kuugua kwa baadhi ya nyota wa sanaa nchini ndiko kunamfanya ashindwe kuusahau mwaka huo.
Alisema kwa kumbukumbu zake tangu Januari mpaka Desemba fani ya sanaa imekuwa  haina nafuu kutokana na kuandamwa na matatizo ikiwemo vifo, ajali na kuugua kwa wasanii wakiwemo waigizaji wa filamu, wachekeshaji na wasanii wa muziki tofauti.
"Kwa kweli pamoja na kumshukuru Mungu kukaribia kuumaliza mwaka 2012, lakini ni vigumu kuusahau kwa jinsi ulivyokuwa mchungu kwangu na wadau wa sanaa  nchini kwa matukio yaliyotokea miezi yote 12," alisema.
Alisema hata hivyo anamuomba Mungu awalinde wasanii na kuufanya mwaka 2013 uwe wa neema, furaha na mafanikio huku akiwasihi wasanii wenzake kumcha Mungu na kuishi kinyenyekevu ili kutomuudhi Muumbaji wao.
"Tunaomba tuuingie mwaka 2013 kwa amani na utulivu na kujipanga upya kwa 2013 ila muhimu tunapaswa kumrudia Mungu ili atupe baraka zake," alisema Masai anayetamba  na wimbo wa 'Rungu na Mukuki'.
Japo Masai hakuyataja matukio yaliyomtia simanzi, ila vifo vya wasanii kama Mzee Kipara, Steven Kanumba, Mlopero, Sharo Milionea, John Stephano, Mariam Khamis na  kuugua kwa akina Vengu, Mzee Small, Sajuki na ajali kadhaa zilizowatokea wasanii   nchini ni kati ya matukio makubwa yaliyojiri ndani ya mwaka 2012.

Morris, Machuppa, Kussi waibeba Golden Bush


NYOTA wa zamani wa timu za Simba na Yanga, Herry Morris, Athuman Machuppa na Salum Swedi 'Kussi' leo waling'ara 'mchangani' baada ya kuibeba timu ya Golden Bush kwa kuiwezesha kuinyuka timu ya vijana ya Chuo Kikuu kwa mabao 3-2 katika pambano la kirafiki lililochezwa jijini Dar es Salaam.
Morris aliyewahi pia kuzichezea timu za Prisons Mbeya na Moro United, aliifungia Golden Bush mabao mawili katika pambano hilo maalum la kuagia mwaka 2012 lililochezwa kwenye uwanja wa Chuo Kikuu.
Kivumbi uwanjani kati ya pambano la Chuo Kikuu na Golden Bus Veterani.

Kikosi cha Golden Bush, kikijiandaa kuingia uwanjani kuumana na Chuo Kikuu leo asubuhi kwenyue uwanja wa Chuo Kikuu, Dar es salaam.

Hatari langoni mwa timu ya vijana ya Chuo Kikuu, walipokuwa wakiumana na Golden Bush Veterani asubuhi ya leo kwenye uwanja wa Chuo Kikuu, Dar es Salaam. Golden Bush waliibuka washindi wa mabao 3-2.


Katika pambano hilo lililochezeshwa vema na nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Madaraka Seleman 'Mzee wa Kiminyio', Golden ilishuka dimbani na wakali kama Said Swedi 'Pannuci', Athuman Machuppa, Yahya Issa, Steve Marashi, Ben Mwalala, Salum Swedi, Katina Shija na wakali wengine waliotamba Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hata hivyo kikosi hicho kilichompoteza 'nahodha' wake, Onesmop Wazir 'Ticotico' aliyeumia dakika ya tisa tu ya mchezo huo ilijikuta ikitanguliwa kufungwa kwa bao 'tamu' lililopachikwa wavuni na nyota wa Chuo Kikuu, Wonder katika dakika ya 13.
Bao hilo lilisawazishwa katika dakika ya 21 na nyota wa mchezo huo, Katina aliyetoa pande murua kwa Morris aliyefunga kwa shuti kali na baadae Omar Mgonja akaiongezea Golden bao la pili dakika ya 38.
Dakika mbili kabla ya mapumziko Chuo Kikuu ilifunga bao la pili na la kusawazisha kupitia tena kwa Wonder baada ya kuwatoka mabeki wa Golden waliokuwa chini ya Salum Kussi, Yahya Issa na Majaliwa na kufanya hadi mapumziko matokeo yawe 2-2.
Kipindi cha pili kilianza kwa Golden kufanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji na kuongeza kasi yao ya mashambulizi na kujipatia bao la tatu na la ushindi lililofungwa tena na Morris katika dakika ya 63 kwa mkwaju mkali wa karibu.

Mmoja wa mabeki wa Chuo Kikuu akiondoa mpira langoni mwake walipokuwa wakiumana na Golden Bush na kukubali kipigo cha mabao 3-2.


IBF yampongeza Francis Cheka

Bondia Francis Cheka (kushoto) alipokuwa akitunushiana misuli na Chimwemwe kabla ya pambano lao ma juzi mjini Arusha, ambapo Cheka aliibuka mshindi kwa pointi dhidi ya mpinzani wake huyo kutoka Malawi.
SHIRIKISHO la Ngumi la Kimataifa (IBF) limempongeza bingwa mpya wa uzito wa Super Middle wa Bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki yaa Kati, Francis Cheka kufuatia juzi kumtwanga kwa pointi Mmalawi Chiotcha Chimwemwe.
Katika barua yake iliyotumwa kwa Cheka Desemba 28, Mwenyekiti wa Kamati ya Ubingwa wa IBF/USBA, Lindsey Tucker alisema wamefurahishwa na Cheka kutwaa ubingwa na kumtakia kila la heri katika kulishikilia taji hilo.
"Tunachukua fursa hii kukutakia maisha na mafanikio mazuri kama bingwa wa IBF na kumhimiza kuishi kama bingwa". Sehemu ya barua hiyo inasomeka hivyo.
Aidha Tucker amemwagia sifa mpinzani wa Cheka kwa kuonyesha ushupavu na ushindani katika pambano hilo lililofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, ambapo alishindwa kwa pointi na mpinzani wake katika pambano hilo lililokuwa kali..
Katika barua hiyo imemkumbusha Cheka kutetea taji lake hilo ndani ya kipindi cha miezi sita.

Aziz Gilla atoa ya moyoni, adai hana kinyongo na Coastal Union

Aziz Gilla (kulia) alipokuwa Simba

ALIYEKUWA mshambuliaji wa timu ya Coastal Union ya Tanga, Salim Gilla, ameibuka na kusema hana kinyongo cha kitendo cha kutemwa na klabu hiyo.
Hata hivyo mshambulaji huyo wa zamani wa Simba, aliyeng'ara katika fainali za Kombe la Taifa ya 2009 akiteuliwa kuwa Mchezaji Bora wa mashindano alidai taarifa ya kutemwa kwake na Coastal zilimshtua kupita maelezo.
Akizungumza na MICHARAZO juzi kwa njia ya simu, Gilla aliyeoongoza orodha ya wafungaji ndani ya Coastal kwa msimu uliopita, alisema kama mchezaji anayaheshimu maamuzi yaliyofikiwa na benchi la ufundi la timu hiyo ya kuamua kumtema.
Alisema huenda makocha wa timu hiyo waliomuona sio mchezaji wa mipango yao na kuamua kumtema, hivyo hawezi kupingana na uamuzi hayo zaidi ya kuitakiwa kila la heri timu hiyo katika duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara.
"Kwa kweli sina kinyongo na maamuzi yaliyofikiwa juu ya kutemwa kwangu kwani ni uamuzi wa kocha, ila nikiri nilishtushwa mno kusikia jina langu ni mioingoni mwa waliotemwa Coastal Union," alisema Gilla.
Mshambuliaji huyo, alisema ni vigumu kuweza kuiwekea kinyongo Coastal kwa vile ni timu ya mkoa wake na ni klabu anayoipenda kwa dhati moyoni.
"Coastal ni timu ya nyumbani, kufanya kwake vema ni sifa kwa mkoa mzima wa Tanga, hivyo siwezi kuichukua zaidi ya kuitakia kila la heri iendeleze moto wa duru la kwanza ili hatimaye itwae ubingwa msimu huu," alisema Gilla.
Coastal Union ilitangaza kuwatema Gilla na wachezaji wenzake kadhaa katika usajili wa dirisha dogo kama njia ya kukiimarisha kikosi chao.
Wengine waliotemwa na mabingwa hao wa zamani wa soka nchini, ni makipa  Juma Mpongo na Jackson Chove, Juma Jabu, Said Sued, Mohamed Issa na Jamal Bachemanga, huku Phillip Maisela, Razak Khalfan, Gerald Lukindo ‘Sipi’ na Shafii Karumani wakitajwa kupelekwa kwa mkopo kwa timu nyingine.

FAINALI ZA KAWAMBWA CUP KUFANYIKA LEO B'MOYO

Rais wa TFF, Leodger Tenga mmoja wa viiongozi wanaotarajiwa kuhudhuria fainali za Kombe la Kawambwa zinazofanyika leo mjini Bagamoyo, Pwani.

FAINALI za soka za kuwania ya Kombe la Kawambwa, inatarajiwa kufanyika leo mjini Bagamoyo kwa kuzikutanisha timu za Beach Boys na Mataya.
Pambano hilo la fainali za michuano hiyo iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo ambaye pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo, Dk Shukuru Kawambwa litafanyika kwenye uwanja wa Mwanakalenge, mjini humo.
Timu hizo zitakazoumana fainali zimepata nafasi hiyo baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali, ambapo Beach Boys yenyewe iliizabua Matimbwa mabao 2-0 na Mataya kuigagadua Chaulu kwa mabao 3-1.
Msemaji wa michuano hiyo, Masu Bwire alisema fainali hizo zinatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodger Tenga na Waziri Dk Shukuru Kawambwa.
Mgeni rasmi wa fainali hizo kwa mujibu wa msemaji huyo ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk Fenella Mukangara.
Bwire, aliongeza viongozi wengine watakaohudhuria fainali hizo ni Meneja wa kampuni ya Konyagi wadhamini wakuu wa michuano hiyo, David Mgwasa na viongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA).
Aliongeza maandalizi ya fainali hizo yamekamilika zikiwamo zawadi za washindi na wale watakaotwaa tuzo mbalimbali za michuano hiyo iliyoanza rasmi Septemba 25 kwa kushirikisha jumla ya timu 84 zilizopo jimboni humo.
Alisema mbali na washindi wa kwanza hadi watatu kuzawadiwa seti za jezi, mipira, vizuia ugoko na fedha taslim, pia Kipa Bora, Mchezaji Bora, na Mwamuzi Bora wa michuano hiyo kila mmoja atazwadiwa Sh. 50,000.
Bwire alisema bingwa wa michuano hiyo atanyakua Sh 400,000, Kombe, jezi seti mbili, mipira miwili na vizuia ugoko seti moja, huku wa pili atazawadiwa Sh 200,000, seti mbili za jezi, mipira miwili na vizuia ugoko seti moja.
Mshindi wa tatu wa michuano hiyo atajinyakulia seti moja ya jezi, mpira mmoja, seti moja ya vizuia ugoko na fedha taslim Sh 100,000.

Mwalala aamua kutundika daluga, kisa maumivu wa nyonga

Ben Mwalala alipokuwa Yanga

MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa timu za Yanga na Coastal Union, Ben Mwalala, ameamua kutundika daluga na kujikita kwenye ukocha kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya muda mrefu ya nyonga.
Akizungumza na MICHARAZO leo jijini Dar es Salaam, Mwalala aliyewahi kung'ara na timu za Mumias ya Kenya,  Sc Villa ya Uganda na APR Rwanda, alisema maumivu hayo yamekuwa yakimsumbua kwa muda mrefu na ndiyo yaliyomuondoa Coastal Union msimu huu.
Mwalala aliyeichezea Yanga kwa nyakati tofauti kati ya kwa 2006-2009, alisema kwa vile ana mapenzi makubwa na soka ameamua kuendeleza mchezo huo kwa kujikita kwenye ukocha akiwa tayari ameshachukua mafunzo ya awali na ngazi ya kati mpaka sasa.
"Kaka nyonga imenifanya nistaafu soka ningali kijana, hata hivyo bado sijatoka katika katika mchezo huo kwani nimeamua kusomea ukocha ili kuendeleza jahazi na hivi karibuni nimetoka kumaliza kozi za ngazi ya kati iliyoendeshwa na TFF," alisema.
Mwalala aliongeza, mipango yake ni kusomea kozi ya ngazi ya juu ya ukocha wa soka kisha kuja kuwa mwalimu wa timu yoyote itakayokuwa inamhitaji.
Mkenya huyo, ambaye 'amelowea' nchini, alisema anaamini bado ana mchango mkubwa katika soka ndani na nje ya nchi ndio maana imekuwa vigumu kwake kuacha moja kwa moja mchezo huo.
Mwalala anakumbukwa na mashabiki wa Yanga kwa kusaidia kufuta uteja wa miaka nane iliyokuwa nayo klabu hiyo mbele ya watani wao wa jadi, Simba kwa bao pekee alililofunga katika mechi ya kwanza ya msimu wa 2008 iliyoichezwa Oktoba 26.
Pia alikuwa mmoja wa walioifungia  Yanga mabao mawili yalioipa sare ya 2-2 katika mechi ya marudiano na watani zao hao iliyochezwa uwanja wa Taifa, Aprili 19, 2009.