STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, December 29, 2012

KOCHA  SIMBA KUTUA LEO KUSHUHUDIA MECHI YAO NA TUSKER


KOCHA mpya wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba SC, Mfaransa Patrick Liewig anatarajiwa kuwasili leo nchini na atakuwapo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuishuhudia timu hiyo ikimenyana na mabingwa wa Kenya, Tusker FC.
Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga amesema kwamba, awali kocha huyo alitarajiwa kuawasili nchini juzi, lakini ilishindikana baada ya kukosa nafasi kwenye ndege na sasa mashabiki wa timu hiyo wamtarajie leo.
Alisema kocha huyo ambaye anakuja kurithi mikoba ya Mserbia Profesa Milovan Cirkovick, atakishuhudia kikosi cha Simba kikicheza mechi hiyo kabla ya kuendelea na taratibu nyingine ikiwemo kusaini mkataba wa kazi na baadaye kuanza kutumikia kibarua chake kipya.
Liewig ni kocha wa zamani wa Akademi ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa, ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Club Africain ya Tunisia, Patrick Liewig na ana Stashahada ya Juu ya ukocha na Shahada ya tatu ya ualimu wa soka ya vijana aliyotunukiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ufaransa, Gerard Houiller na amehudhuria pia kozi za ufundishaji mazoezi ya viungo Juni mwaka 1999 katika Chuo Kikuu cha Dijon.
Kwa upande wa uzoefu, Liewig alifanya kazi PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 kama Kocha Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa pia katika programu za timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa Under 20, Under 18 aliowawezesha kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na Under 16.
Kuanzia mwaka 1989 hadi 1990:  alikuwa Meneja Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa Henri Michel, 1991 hadi 1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa Msaidizi wa Luis Fernandez, 1996 hadi 1998: alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998 hadi 1999 alikuwa Msaidizi wa Alain Giresse.
Liewig pia alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi 2001, ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.
Januari mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika fainali za Afrika za U20 nchini Burkina Faso.
Kuanzia mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast aliyoipa mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005 na 2006, Super Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu Fainali.
Amekuwa Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004, 2005 na 2006 na tangu Septemba mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa Club Africain ya Tunisia
Kuelekea mchezo wa leo, Simba itamenyana na Tusker FC ambayo ilianza vema ziara yake nchini, baada ya kuichapa Yanga 1-0 katika mchezo ulipigwa kwenye Uwanja wa Taifa Jumatano.
Simba SC na Tusker zinatarajiwa kukutana pia kwenye Kundi la Mapinduzi visiwani Zanziabr hivi karibuni, kwani zimepangwa kundi moja, A pamoja na Bandari ya Unguja na Jamhuri ya Pemba.
Aidha, katika Kundi B, washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Bara, Azam FC ya Dar e Salaam pia, imepangwa na Mtibwa Sugar ya Morogoro, Coastal Union  ya Tanga na Miembeni ya Unguja.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambayo ni maalum kwa ajili ya kuherehekea Mapinduzi matukufu ya Zanzaibar, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 2, hadi kilele cha miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, mwakani, huku ikishirikisha timu kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo iliyotolewa na Kamati Maalum ya Kusimamaia michuano hiyo, inaonesha kuwa katika mchezo wa kwanza utakaochezwa siku ya ufunguzi itakuwa ni kati ya Bandari kutoka Unguja ambayo itacheza na Jamhuri kutoka kisiwani Pemba ambao ni wawakilishi wa Zanzibar katika Kombe la Shirikisho Barani Afrika, pamabanolitakalochezwa katika uwanja wa Mao Tse Tung mjini Unguja, huku usiku wa siku hiyo hiyo katika Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja pambano la ufunguzi rasmi katika mashindano hayo likiwakutanisha mabingwa wa soka nchini Tanzania, Simba SC ambao watapambana na mabingwa wa soka nchini Kenya, Tusker.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo jumla ya timu nane zitashiriki katika mashindano hayo ambayo yamejipatia umaarufu mkubwa visiwani hapa, timu hizo zimegawanya katika makundi mawili ambayo ni kama ifuatavyo:
Awali michuano hiyo ilitarajiwa kuanza kisiwani Pemba tarehe 1 Januari, lakini kutokana na kujitoa katika mashindano kwa klabu ya Al-Ahly ya Misri kutokana na klie kilichoelezwa sababu za kiusalama, mechi zote sasa zitachezwa kisiwani Unguja na ufunguzi ukipangwa kuanza tarehe 2 badala ya tarehe 1 januari.
Bingwa wa michuano hiyo ataondoka na zawadi ya kombe na fedha taslim Tsh.Milioni kumi (10,000,000), mshindi wa pili Milioni tano (5,000,000), pamoja na zawadi nyengine ambazo zimegawanywa katika makundi tofauti ikiwemo zawadi ya mfungaji bora, mchezaji bora, mwamuzi bora, kipa bora, mwandishi wa habari bora, timu bora na zawadi nyinginezo.

No comments:

Post a Comment