Rais wa TFF, Leodger Tenga mmoja wa viiongozi wanaotarajiwa kuhudhuria fainali za Kombe la Kawambwa zinazofanyika leo mjini Bagamoyo, Pwani. |
FAINALI za soka za kuwania ya Kombe la Kawambwa, inatarajiwa kufanyika leo mjini Bagamoyo kwa kuzikutanisha timu za Beach Boys na Mataya.
Pambano hilo la fainali za michuano hiyo iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo ambaye pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo, Dk Shukuru Kawambwa litafanyika kwenye uwanja wa Mwanakalenge, mjini humo.
Timu hizo zitakazoumana fainali zimepata nafasi hiyo baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali, ambapo Beach Boys yenyewe iliizabua Matimbwa mabao 2-0 na Mataya kuigagadua Chaulu kwa mabao 3-1.
Msemaji wa michuano hiyo, Masu Bwire alisema fainali hizo zinatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodger Tenga na Waziri Dk Shukuru Kawambwa.
Mgeni rasmi wa fainali hizo kwa mujibu wa msemaji huyo ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk Fenella Mukangara.
Bwire, aliongeza viongozi wengine watakaohudhuria fainali hizo ni Meneja wa kampuni ya Konyagi wadhamini wakuu wa michuano hiyo, David Mgwasa na viongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA).
Aliongeza maandalizi ya fainali hizo yamekamilika zikiwamo zawadi za washindi na wale watakaotwaa tuzo mbalimbali za michuano hiyo iliyoanza rasmi Septemba 25 kwa kushirikisha jumla ya timu 84 zilizopo jimboni humo.
Alisema mbali na washindi wa kwanza hadi watatu kuzawadiwa seti za jezi, mipira, vizuia ugoko na fedha taslim, pia Kipa Bora, Mchezaji Bora, na Mwamuzi Bora wa michuano hiyo kila mmoja atazwadiwa Sh. 50,000.
Bwire alisema bingwa wa michuano hiyo atanyakua Sh 400,000, Kombe, jezi seti mbili, mipira miwili na vizuia ugoko seti moja, huku wa pili atazawadiwa Sh 200,000, seti mbili za jezi, mipira miwili na vizuia ugoko seti moja.
Mshindi wa tatu wa michuano hiyo atajinyakulia seti moja ya jezi, mpira mmoja, seti moja ya vizuia ugoko na fedha taslim Sh 100,000.
No comments:
Post a Comment