STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, May 6, 2018

Rostand anatunguliwa na kipa mwenzake

YANGA wanafungwa bao la nne kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na Zammamouche na kuifanya USM kutoka na ushindi mnono wa mabao 4-0. Pambano limeisha mara baada ya mkwaju huo.

Waarabu wanapata penalti

USM wanapata penalti baada ya Dante kucheza faulo ndani ya lango lake.

Zimeongezwa dakika mbili

ZIMEONGEZWA dakika mbili kabla ya pambano la Yanga na USM Alger kumalizika na matokeo bado ni 3-0.

Dante ameumia

BEKI na nahodha wa mchezo wa leo, Dante ameumia na anapatiwa matokeo. Bado dakika mbili mpira kumalizika. Yanga wapo nyuma mabao 3-0. Yohana Mkomola pia kaingia kuchukua nafasi ya Yusuf Mhilu aliyeshindwa kabisa kufurukuta.

Pato anaingia kumpokea Makapu

YANGA imefanya mabadiliko kwa kumtoa Juma Said 'Makapu' na kuingia Pato Ngonyani. USM Alger wamebanwa kwa sasa, lakini bado wanaongoza kwa mabao 3-0.

Darfalou alimwa kadi naye

Oussumana darfalou naye anapewa kadi ya njano kwa kumchezea Abdallah Shaibu Ninja anayekaba hadi kivuli. Dakika ya 70. Mabao bado 3-0.

Juma Mahadhi apewa kadi

JUMA Mahadhi anakuwa mchezaji wa kwanza kupewa kadi ya njano katika mchezo huu, Matokeo bado 3-0.

Rafael anatoka Abdul anaingia

Juma Abdul
YANGA imefanya mabadiliko ya kumtoa Rafael Daud na kumuingiza Juma Abdul ikiwa ni mbinu ya benchi la ufundi la Yanga kuimarisha ulinzi baada ya kuona wasipokuwa makini watapigwa nyingi.
Dakika ya 65' USM 3 Yanga 0

Yanga inapigwa la tatu


MAMBO yanazidi kuwa magumu kwa Yanga baada ya wenyeji kuandika bao la tatu, kutokana na uzembe wa mabeki na kipa Rostand na Abderrahmane Meziane anauweka kimiani mpira ikiwa ni dakika ya 54.
USM Alger 3 Yanga )

Hassan Kessy anaupiga mwingi

BEKI Hassan Kessy ndiye pekee anayeonekana kujitoa uwanjani akihakaka kila mahali.

Waarabu wameanza uhuni wao

MMOJA wa wachezaji wa USM Alger anafanya uhuni wa kupiga mpira na kumgandishia mguu beki Dante na kumfanya apatiwe matibabu. Hata hivyo Dante anaendelea. Matokeo bado 2-0.

Mopira umeanza

Dakika 45 za pili zimeanza, na Yanga wanafika langoni mwa USM Alger. Matokeo bado 2-0.

Timu zinarudi uwanjani

TIMU za Yanga na USM Alger zinarudi uwanjani kuanza kipindi cha pili.

Takwimu za nusu ya kwanza

USM Alger                        Yanga
2              Goals                 0

9              Shots                 3
3              Shots on Target   1
73%         Possession         27%
0              Yellow Card         0
0              Red Card             0
1              Offsides               2
7              Corners               1   

Ni mapumziko sasa

Pambano la Yanga na USM Alger limemaliza dakika 45 na wachezaji wanaenda mapumziko kupewa mawaidha kabla ya kurudi uwanjani kwa kipindi cha pili. USM wapo mbele kwa mabao 2-0.
Wenyeji wameposses mpira kwa asilimia 73 kwa 27 za Yanga.

Imeongezwa dakika moja ya nyongeza

Imeongezwa dakika moja kabla ya mapumziko, Yanga bado ipo nyuma kwa mabao 2-0

Yanga wanakosa bao

Shuti la Mwashiuya linaokolewa na kipa na kuinyima Yanga bao. Bao 2-0

Pengo la Tshishimbi, Chirwa, Ajibu laonekana


Bado dakika tano kabla ya mapumziko, lakini Yanga bado inahaha kurejesha mabao waliyotanguliwa na wenyeji wao, huku mapengo ya nyota watano waliobaki jijini Dar es Salaam yakionekana wazi.
Nyota hao waliokosekana kwenye mchezo huo unaoendelea mjini Algiers ni Papy Kabamba Tshishimbi, Obrey Chirwa, Kelvin Yondani, Ibrahim Ajibu na Thabani Kamusoko.

Mambo bado magumu

Pambano la Yanga na USM Alger bado linaendelea na Yanga wanapigwa bao la pili baada ya kona ya wenyeji kusindikizwa wavuni na Farouk Chafai dakika ya 33 kipa Rostand akifanya makosa yale yale na kufungwa bao rahisi. Mpira wa Chafai unamaliziwa kimiani na Pius Buswita.
USM Alger 2 Yanga 0

Yanga inapata kona ya kwanza

Yanga wanapata kona baada ya shambulizi lao kuokolewa na mabeki, wakati Geofrey Mwashiuya akijiandaa kufunga. Hata hivyo haijazaa matunda. Dk 26

Uwanja umeelemea kwa Yanga

DK 25 Yanga bado wanakimbizwa, licha ya kujitahidi kurudisha mashambulizi, lakini ni kama uwanja umeelemea upande mmoja.
Bao matokeo ni 1-0 wenyeji wapo mbele.

Yanga chupuchupu tena

Yanga chupuchupu wapigwe bao la pili, makosa ya Andrew Vincent 'Dante' na kipa Rostand ambaye amekuwa akitoka ovyo langoni mwake bila hesabu makini.
Dk 23

Yanga wanakoswa koswa

WAWAKILISHI wa Tanzania Yanga, bado wanashambuliwa na USM Alger, huku ikionekana upande wa kushoto unaolindwa na Gadiel Michael ukiwa uchochoro wa mashambulizi mengi ya wenyeji.
Dakika ya 21

Dakika ya 15 mambo bado

Matokeo bado ni 1-0 wenyeji wakiwa mbele, huku nyota wa Yanga wakionekana kuzidiwa na wenyeji.

Yanga yatanguliwa bao la mapema

DAKIKA ya Nne tu, Yanga wamesharuhusu bao la kuongoza la Waarabu wa USM Alger baada ya mabeki na kipa Youthe Rostand kushindwa kuokoa krosi pasi iliyoungwa na Oussama Darfalou
USM Alger 1 Yanga 0.

Hiki ndicho kikosi cha Yanga kitakachoanza dhidi ya USM Alger


Yanga yarahisishiwa kazi Kombe la Shirikisho Afrika

Yanga SC ambao muda mchache ujao watalianzisha kwa USM Alger katika mechi yao ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.
KIGALI, RWANDA
WAKATI Yanga ikijiandaa usiku huu kuvaana na USM Alger mjini Algiers, Algeria, wapinzani wao katika kundi hilo, Rayon Sports ya Rwanda na Gor Mahia ya Kenya wameshindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1 mjini Kigali, Rwanda.
Katika pambano hilo klililochezwa Uwanja wa Nyamirambo, wageni Gor Mahia ndio waliokuwa wa kwanza kuandika bao dakika ya 10 likifungwa na Mnyarwanda Meddie Kagere kabla ya wenyeji kuchomoa kupitia Eric Rutanga dakika ya 24.
Matokeo hayo yametioa nafuu kwa Yanga katika mbio zao za kuwania kutinga robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kundi lao, lakini ikitegemeana na matokeo yake ya usiku huu nchini Algeria.
Baada ya mchezo wao wa usiku huu, Yanga itarudi nyumbani kuisubiri Rayon katika mechi yao ya pili, wakati Gor Mahia itakuwa mjini Nairobi kuipokea USM Alger mechi zikichezwa Mei 16.
Katika mechi nyingine za michuano hiyo, ASEC Mimosas iliwatambia Aduana Stars ya Ghana kwa bao 1-0 mjini Abidjan, Ivory Coast, Berkane ya Morocco nayo ilishinda 1-0 dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan na Enyimba ikiwa nyumba Nigeria iliwatmbia Djoliba ya Mali kwa mabao 2-0.

Simba hii ya Lechantre tema mate chini, Okwi motoooo!

Kikosi cha Simba wanaelekea kubeba taji lao la 19 la Ligi Kuu Bara msimu huu
Emmanuel Okwi

NA RAHMA WHITEWAMESHINDIKANA. Ndio, hakuna tena wa kuizuia Simba kwani vinara hao wa Ligi Kuu Bara wamebakisha mchezo mmoja tu kabla ya kutangazwa mabingwa wa msimu huu baada ya jioni ya leo kuwatandika Ndanda FC ya Mtwara kwa bao 1-0.
Katika mchezo huo mkali uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam Simba iliandika bao lake kupitia kwa nyota wake, Emmanuel Okwi lililomfanya afikishe bao la 20 na kuipa Simba alama tatu muhimu wakitimiza pointi 65 baada ya mechi 27.
Kama wataenda kuitandika Singida United kwenye Uwanja wao wa nyumbani wa Namfa, Singida basi watawavua rasmi watani zao Yanga taji la Ligi Kuu baada ya Vijana wa Jangwani kulishikilia kwa misimu mitatu mfululizo.
Simba ikishinda Jumamosi ijayo dhidi ya Singida, itawafanya wafikishe alama 68 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote akiwamo Yanga ambayo imesaliwa na michezo minne mkononi huku ikiwa na alama 48 tu. Yanga ikishinda mechi zote ina uwezo wa kufikisha pointi 66 tu. Azam waliokuwa wakitarajiwa kuiletea kauzibe Simba yenye jioni a leo imekubali kichapo cha mabao 2-1 toka kwa Chama la Wana na kuifanya isaliwe na alama zao 49 ikisaliwa na mechi tatu ambazo kama itashinda zote itawapa nafasi ya kufikisha pointi 58 tu ambazo zimeshapitwa na Simba kitambo.
Katika mchezo wa leo Simba ililianza pambano kwa kasi na kufanya mashambulizi mfululizo langoni mwa Ndanda, lakini umakini mdogo wa washambuliaji wao uliwanyima bao mpaka dakika ya 44 Okwi alipowapa furaha mashabiki wa Msimbazi.
Okwi alipokea pasi ndefu ya Shomary Kapombe aliyekuwa katikati ya uwanja na kukimbia na mpira akifukuzwa na mabeki watatu wa Ndanda waliokuwa wakidhani atatoa pasi kabla ya kuhamisha mpira kutoka mguu wa kulia na kuuweka kushoto na kufumua shuti kali lililomshinda kipa Daniel Makonga.
Bao hilo limemfanya Okwi afikishe bao la 20 msimu huu na kuzidi kumsogeza kwenye nafasi ya kunyakua Kiatu cha Dhahabu, huku pia akiwinda kuvunja rekodi za Amissi Tambwe aliyefunga mabao 21 misimu miwili iliyopita yakiwa mabao mengi kwa nyota wa kigeni katika Ligi Kuu Bara.
Hata hivyo Okwi atapaswa katika mechi tatu zilizosalia za timu yake afunge mabao sita ili angalau kufikia rekodi ya muda mrefu ya straika wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Mohammed Hussein 'Mmachinga' ya kufunga mabao mengi katika msimu mmoja.
Machinga alifunga mabao 26 katika Ligi Kuu enzi za Ligi Daraja la Kwanza katikati ya 1990 na imedumu kwa zaidi ya miaka 20 bila kuvunjwa, japo Abdallah Juma aliyewahi kutamba Mtibwa Sugar kukaribia kuivunja kwa kufunga mabao 25 msimu wa 2006.
Kipigo hicho cha leo kimeifanya Ndanda kujiweka katika mbaya zaidi ya kusalia katika Ligi Kuu kwa msimu ujao kwani imebaki nafasi ya 15 ikiwa na alama 23, moja zaidi ya timu inayioburuza mkia, Njombe Mji ambayo jana ilitandikwa mabao 4-0 na Singida.

Mkwera kamkalisha mtu kwa KO katika masumbwi


Picha tofauti zikionyesha Idd Mkwera bukta nyeusi akimnyoosha Ramadhani Shauri kabla ya mpinzani wake huyo kuokolewa na mwamuzi aliyemshika mkono, baada ya kuinuka alipolambishwa sakafu na pambano lao kumalizika raundi ya 9 kwa KO. Mkwera akishinda.
NA RAHIM JUNIOR
HANA hamu. Ndivyo unavyoweza kusema kwa Bondia Ramadhani Shauri kumkuta ya kumkuta baada ya kupigwa KO ya raundi ya 9 na Idd Mkwera katika pambano lao lililokuwa la raundi 10 lililofanyika juzi kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Katika pambano hilo mabondia wote walionekana kukamiana na kutupiana masumbwi kwa kupokezana kabla ya Mkwera kumzidi ujanja mpinzani wake katika raundi za sita, saba na nane kabla ya raundi ya tisa, Shauri kukata pumzi kwa kulamba sakafu.

Baada ya kuhesabiwa vya kutosha, mwamuzi wa pambano hilo aliamua kumaliza mchezo kutokana na Shauri kuonekana wazi amesalimu amri na asingeweza kuendelea kupokea makonde na Mkwera.
Mara baada ya pambano hilo Mkwera anayenolewa na Kocha Rajab Mhamila 'Super D' alisema licha ya kupewa mkataba wa pambano hilo ndani ya siku 16, lakini alijifua vema na ndio maana ameibuka na ushindi huku akimsifia mpinzani wake kuwa sugu kwani alipaswa kupigwa KO mapema.
Mbali na pigano hilo pia kulikuwa na michezo mingine ambapo Amani Bariki  alijikuta akipoteza kwa pointi mbele ya Haidar Mchanjo, huku Said Chino  alimchapa kwa pointi Hamza Mchanjo na James Kibazange alimpiga K.O ya raundi ya 3 Karimu Ramadhan.
Katika michezo hiyo mvua ilikatisha uhondo kwani mashabiki walijitokeza kiasi chake, lakini waliofika walipata burudani ya aina yake kutokana kwa mabondia waliopigana.