STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, May 6, 2018

Simba hii ya Lechantre tema mate chini, Okwi motoooo!

Kikosi cha Simba wanaelekea kubeba taji lao la 19 la Ligi Kuu Bara msimu huu
Emmanuel Okwi

NA RAHMA WHITEWAMESHINDIKANA. Ndio, hakuna tena wa kuizuia Simba kwani vinara hao wa Ligi Kuu Bara wamebakisha mchezo mmoja tu kabla ya kutangazwa mabingwa wa msimu huu baada ya jioni ya leo kuwatandika Ndanda FC ya Mtwara kwa bao 1-0.
Katika mchezo huo mkali uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam Simba iliandika bao lake kupitia kwa nyota wake, Emmanuel Okwi lililomfanya afikishe bao la 20 na kuipa Simba alama tatu muhimu wakitimiza pointi 65 baada ya mechi 27.
Kama wataenda kuitandika Singida United kwenye Uwanja wao wa nyumbani wa Namfa, Singida basi watawavua rasmi watani zao Yanga taji la Ligi Kuu baada ya Vijana wa Jangwani kulishikilia kwa misimu mitatu mfululizo.
Simba ikishinda Jumamosi ijayo dhidi ya Singida, itawafanya wafikishe alama 68 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote akiwamo Yanga ambayo imesaliwa na michezo minne mkononi huku ikiwa na alama 48 tu. Yanga ikishinda mechi zote ina uwezo wa kufikisha pointi 66 tu. Azam waliokuwa wakitarajiwa kuiletea kauzibe Simba yenye jioni a leo imekubali kichapo cha mabao 2-1 toka kwa Chama la Wana na kuifanya isaliwe na alama zao 49 ikisaliwa na mechi tatu ambazo kama itashinda zote itawapa nafasi ya kufikisha pointi 58 tu ambazo zimeshapitwa na Simba kitambo.
Katika mchezo wa leo Simba ililianza pambano kwa kasi na kufanya mashambulizi mfululizo langoni mwa Ndanda, lakini umakini mdogo wa washambuliaji wao uliwanyima bao mpaka dakika ya 44 Okwi alipowapa furaha mashabiki wa Msimbazi.
Okwi alipokea pasi ndefu ya Shomary Kapombe aliyekuwa katikati ya uwanja na kukimbia na mpira akifukuzwa na mabeki watatu wa Ndanda waliokuwa wakidhani atatoa pasi kabla ya kuhamisha mpira kutoka mguu wa kulia na kuuweka kushoto na kufumua shuti kali lililomshinda kipa Daniel Makonga.
Bao hilo limemfanya Okwi afikishe bao la 20 msimu huu na kuzidi kumsogeza kwenye nafasi ya kunyakua Kiatu cha Dhahabu, huku pia akiwinda kuvunja rekodi za Amissi Tambwe aliyefunga mabao 21 misimu miwili iliyopita yakiwa mabao mengi kwa nyota wa kigeni katika Ligi Kuu Bara.
Hata hivyo Okwi atapaswa katika mechi tatu zilizosalia za timu yake afunge mabao sita ili angalau kufikia rekodi ya muda mrefu ya straika wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Mohammed Hussein 'Mmachinga' ya kufunga mabao mengi katika msimu mmoja.
Machinga alifunga mabao 26 katika Ligi Kuu enzi za Ligi Daraja la Kwanza katikati ya 1990 na imedumu kwa zaidi ya miaka 20 bila kuvunjwa, japo Abdallah Juma aliyewahi kutamba Mtibwa Sugar kukaribia kuivunja kwa kufunga mabao 25 msimu wa 2006.
Kipigo hicho cha leo kimeifanya Ndanda kujiweka katika mbaya zaidi ya kusalia katika Ligi Kuu kwa msimu ujao kwani imebaki nafasi ya 15 ikiwa na alama 23, moja zaidi ya timu inayioburuza mkia, Njombe Mji ambayo jana ilitandikwa mabao 4-0 na Singida.

No comments:

Post a Comment