STRIKA
USILIKOSE
Sunday, May 6, 2018
Mkwera kamkalisha mtu kwa KO katika masumbwi
NA RAHIM JUNIOR
HANA hamu. Ndivyo unavyoweza kusema kwa Bondia Ramadhani Shauri kumkuta ya kumkuta baada ya kupigwa KO ya raundi ya 9 na Idd Mkwera katika pambano lao lililokuwa la raundi 10 lililofanyika juzi kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Katika pambano hilo mabondia wote walionekana kukamiana na kutupiana masumbwi kwa kupokezana kabla ya Mkwera kumzidi ujanja mpinzani wake katika raundi za sita, saba na nane kabla ya raundi ya tisa, Shauri kukata pumzi kwa kulamba sakafu.
Baada ya kuhesabiwa vya kutosha, mwamuzi wa pambano hilo aliamua kumaliza mchezo kutokana na Shauri kuonekana wazi amesalimu amri na asingeweza kuendelea kupokea makonde na Mkwera.
Mara baada ya pambano hilo Mkwera anayenolewa na Kocha Rajab Mhamila 'Super D' alisema licha ya kupewa mkataba wa pambano hilo ndani ya siku 16, lakini alijifua vema na ndio maana ameibuka na ushindi huku akimsifia mpinzani wake kuwa sugu kwani alipaswa kupigwa KO mapema.
Mbali na pigano hilo pia kulikuwa na michezo mingine ambapo Amani Bariki alijikuta akipoteza kwa pointi mbele ya Haidar Mchanjo, huku Said Chino alimchapa kwa pointi Hamza Mchanjo na James Kibazange alimpiga K.O ya raundi ya 3 Karimu Ramadhan.
Katika michezo hiyo mvua ilikatisha uhondo kwani mashabiki walijitokeza kiasi chake, lakini waliofika walipata burudani ya aina yake kutokana kwa mabondia waliopigana.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment