STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, February 2, 2014

Ruvu Shooting yawasemehe akina Maguli, kocha Olaba anena yake

Elias Maguli
WAKATI wachezaji Elias Maguli na Ali Kani wakianza mazoezi na wenzao baada ya kusamehewa na uongozi wa Ruvu Shooting kwa kitendo cha utoro wa kwenda Oman bila ruksa, kocha Tom Olaba amesema anaendelea kuwaangalia kwanza.
Wachezaji hao walitoroka mapema mwezi uliopita kwenda kusaka timu ya kujiunga nayo kwa soka la kulipwa, wakati klabu yao ikijianda na duru la pili na waliporejea uongozi uliwapiga 'stop' kwa kitendo hicho cha utovu wa nidhamu.
Hata hivyo kwa mujibu wa Afisa Habari wa klabu hiyo, Masau Bwire wachezaji hao waliuangukia uongozi kwa kuomba radhi na kuwaomba msamaha wachezaji, makocha na TFF na wao wamewasamehe.
"Tumewasamehe na wamerejeshwa kundini wakianza mazoezi na wenzao tangu Alhamisi na kocha Tom Oloba atakuwa na maamuzi ya kutaka kuwatumia kama watamfaa kwa mechi zijazo," alisema Bwire.
MICHARAZO liliwasiliana na Oloba kwa njia ya simu jana na kukiri kurejea kikosi kwa wachezaji, lakini alisema ni mapema mno kuwaelezea wachezaji hao na kujua kama ataweza kuwatumia katika mechi mbili zijazo za ugenini wiki hii.
Mkenya huyo alisema licha ya wachezaji hao kuanza mazoezi na wenzao tangu Alhamisi, bado anaendelea kuwaangalia  ili kupima uwezo wake na kama wana fiti katika mfumo wake na kuweza kuwatumia kwa mechi hizo zijazo.
"Ni kweli akina Maguli na Kani wameshaanza mazoezi na ninawangalia pamoja na wenzao kuona wachezaji gani nitakaoteua kuondoka nao kwenda Tanga na Mbeya, hivyo naendelea kuwangalia kwanza," alisema Olaba.
Olaba anatarajiwa kuteua kikosi chake kesho saa chache kabla ya safari yao ya Tanga kwenda kuvaana na Mgambo JKT siku ya Jumatano katika uwanja wa Mkwakwani.
Baada ya mechi hiyo timu hiyo itaunganisha hadi jijini Mbeya kucheza mechi yao ya kiporo dhidi ya wenyeji wao maafande wa Prisons kwenye uwanja wa Sokoine.
Mechi yao ya awali iliyokuwa ichezwe Janauri 25 iliahirishwa kutokana na tatizo la uwanja wa Sokoine uliokuwa umefungiwa na TFF kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati.

Hatimaye Babi apumua, familia yake yamfuata Malaysia

Babi na mkewe Mariam Abdulkadir waki-show Super Market nchini Malaysia baada ya mkewe huyo kutua na watoto wao
KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa nchini Malaysia katika klabu ya Ligi Kuu ya UiTM, Abdi Kassim 'Babi' amepumua baada ya familia yake kutoka visiwani Zanzibar kuwasili nchini Malaysia.
Akizungumza na MICHARAZO  kutoka Malaysia, Babi alisema familia yake ikiongozwa na mkewe, Mariam Abdulkadir iliwasili wikiendi hii ikiwa na mkewe Mariam Abdulkadri aliyeambatana na watoto wake.
Babi alisema kutua kwa familia yake kwa ajili ya kuishi nayo nchini Malaysia wakati akitumikia mkataba wake wa mwaka mmoja UiTM imempa faraja kubwa kwani alikuwa hana amani alipokuwa mbali na familia hiyo.
"Kwa kweli nimefurahi na kufarijika kuwasili kwa familia yangu nchini hapa, sikuwa na amani na pengine sasa nitacheza maradufu kuisaidia timu yangu kuliko ilivyokuwa siku za nyuma familia ikiwa Zanzibar," alisema Babi.
Babi anayetarajiwa kushuka tena dimbani na klabu yake katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Ijumaa hii, baada ya kuiongoza mechi mbili zilizopita kwa kushinda dhidi ya Kuala Lumpur na nyingine kupata sare ya 1-1 dhidi ya Johor, bao la timu yake akilifunga yeye.
Kiungo huyo nahodha wa zamani wa Yanga, amesajiliwa UiTM akitokea KMKM ya Zanzibar iliyomnyakua msimu huu baada ya kuachana na Azam aliyokuwa akiichezea kwa mkataba wa misimu miwili iliyopita.

Huyu ndiye Ali Badru: Straika aliyekimbia vurugu Misri akiamini Simba itampeleka Ulaya


Ali Badru akiwajibika uwanjani
 KAMA siyo vurugu za kisiasa zilizoibuka miaka miwili iliyopita nchini Misri na kusababisha kusimamishwa kwa ligi ya nchi hiyo baada ya tukio la fujo zilizoua mashabiki zaidi ya 70, huenda mshambuliaji mpya wa Simba, Ali Badru asingerejea nchini.
Mchezaji huyo alikuwa akiichezea klabu ya Al Canal (El Qanah) kabla ya kurejea hivi karibuni na kujiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili.
Badru anasema alikuwa ametoka kuisaidia timu hiyo kupanda Ligi Kuu, lakini vurugu na kusimamishwa kwa ligi kwa muda kuliwafanya wachezaji wakose la kufanya huku kiuchumi wakiyumba na kuona bora arejee nyumbani.
"Kwa kweli nisingerejea mapema nyumbani kama siyo vurugu zilizopo Misri zilizotishia amani na kule kusimamishwa kwa ligi ya nchi hiyo (tayari inaendelea kwa sasa), kazi yangu ni soka hivyo sikuona sababu ya kubaki huko," anasema.
Nyota huyo wa zamani wa Jamhuri-Pemba, anasema hajutii uamuzi wa kurudi nyumbani kwa sababu amejiunga na klabu bora aliyoiota tangu utotoni, akiamini itamsaidia kucheza soka la kulipwa Ulaya.
Anasema mfumo wa Simba wa kuruhusu nyota wake wanaopata timu nje ya nchi unamfanya aamini ndoto zake za kucheza Ulaya zitatimia.
"Nimefurahi kutua Simba klabu ninayoipenda tangu utotoni, ina mfumo mzuri wa kuwapa nafasi wachezaji wake kwenda nje, itanisaidia  kutimiza ndoto za kucheza Ulaya," anasema.
Anaongeza hali ya ushindani aliyokutana nayo Simba katika kuwania namba inazidi kumfanya afurahi kwa kuamini itamjenga zaidi kisoka.
Badru anayeichezea timu ya Taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes', anasema ndani ya Simba hakuna mchezaji mwenye namba ya kudumu hivyo kufanya kila mchezaji muda wote kuongeza bidii ili wasiachwe nyuma, akimsifu pia kocha Zdravko Logarusic  kwa ufundishaji wake uliotukuka na unaotaka nidhamu zaidi.
"Ushindani upo Simba, unajua hii ni klabu kubwa kila mchezaji anataka nafasi ili ajitangaze, hivyo inavutia na kutufanya wachezaji tusibweteke," anasema.


FURAHA
Badru aliyevutiwa kisoka na mshambuliaji wa zamani wa klabu anayoishabikia ya Arsenal anayeichezea kwa sasa Manchester United, Robin van Persie anasema hakuna tukio la furaha kwake kama aliposajiliwa Al Canal ya Misri ikiwa daraja la kwanza na kuipandisha Ligi Kuu.
Anasema fursa ya kucheza nje imemfanya ajifunze mambo mengi ikiwamo kuona tofauti ya mfumo wa soka kati ya Tanzania na Misri hasa namna ya kuthaminiwa kwa wachezaji.
"Kwa kweli kucheza kwangu soka la kulipwa Misri ni jambo la furaha kama ninavyofurahia sasa nikiwa Simba," anasema.
Badru anayependa kutumia muda wake wa ziada kupunga upepo ufukweni na kubadilishana mawazo na rafiki zake, anasema hakuna tukio la simanzi kwake kama kifo cha mdogo wake kilichotokea akiwa mdogo.
"Mpaka leo nikikumbuka tukio hilo naumia sana, nilimpenda sana mdogo wangu," anasema.
Badru anayelitaja pambano lao la mwisho la kuwania kupanda Ligi Kuu Misri na kushinda bao 1-0 kuwa ndilo gumu kwake, anasema anashukuru soka kumsaidia kwa mengi kimaisha na kiuchumi.
"Siwezi kukufuru, soka limenisaidia mengi ikiwamo kuitunza familia yangu, na kusafiri nchi mbalimbali kwa sababu ya mchezo huo," anasema.
Mkali huyo anayemudu pia nafasi ya kiungo, anawataka wachezaji wenzake kujituma, kuwa na nidhamu nje na ndani ya uwanjani na kutambua soka ni ajira yao hivyo waiheshimu ili waweze kufika mbali kimaisha.
Badru anawaomba viongozi wa FA na klabu kuwajali na kuwathamini wachezaji pamoja na kuwezesha maandalizi mazuri kwa timu zao ili kufanya vyema kwenye michuano inayoshiriki.
"Viongozi wakifanya maandalizi mazuri na kuwatimizia mahitaji wachezaji wao ipasavyo, ni rahisi timu kufanya vizuri, pia wazingatie kuwekeza kwenye soka la vijana," anasema.


LIGI
Badru aliyezaliwa mwaka 1990 mjini Pemba, alianza kucheza soka tangu akisoma Shule ya Msingi na klabu yake ya chandimu ni Finya Champion ya visiwani humo kisha kucheza Chasasa United kabla ya kudakwa na mabingwa wa zamani wa Zanzibar, Jamhuri.
Baada ya kutamba na Jamhuri, mwaka juzi alienda Misri kucheza soka la kulipwa kabla ya Simba kumnyakua hivi karibuni huku akiichezea timu ya Taifa ya Zanzibar.
Kuhusu duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara iliyoanza wiki iliyopita, anasema ni la ushindani mkubwa.
"Ligi ni ngumu, kila timu itataka kushinda ili ijiweke pazuri hali inayofanya isiwe rahisi kutabiri matokeo ya uwanjani," anasema.
Badru anayependa kula vyakula vya kawaida visivyo na madhara na kunywa vinywaji laini hasa juisi halisi, anaitabiria klabu yake ya Simba kuwa itafanya veme kwa jinsi ilivyojiandaa chini ya kocha Logarusic.
"Wapinzani wetu wakae chonjo, tupo fiti na wachezaji tuna ari kubwa ya kuona Simba inafanya vyema kwenye duru hili la pili baada ya kumaliza duru lililopita nafasi ya nne chini ya kocha mwingine," anasema Badru aliyetoa pasi kwa Ramadhani Singano 'Messi' na kumwezesha kufunga bao pekee wakati wakiilaza Rhino Rangers 1-0.
Anasema licha ya kutokuwa na uzoefu na ligi hiyo, lakini anajiamini atafanya mambo makubwa akiaminiwa na makocha wake kwa sababu anajiamini na kujua soka.
Badru aliyeanza kucheza soka la kulipwa mwaka 2006 anawashukuru wazazi, wajomba zake, kocha Mohammed Malik na wote waliomsaidia kufika alipo sasa, akidai zaidi ya yote ni Mungu aliyemuumba.
"Naamini bila ya Mungu kunijalia kipaji na kunipa afya njema ya kucheza, leo nisingekuwa hapa, ninamuomba anizidishie zaidi ili nitimize malengo yangu," anasema.
Badru anasema kama siyo soka alitamani baadaye kuwa 'Injinia' au mfanyabiashara, huku akidai kwa hapa nchini hakuna mchezaji anayemsumbua dimbani.

David Naftal afichua siri adai , soka la Bongo limejaa fedha bila mikakati

David Naftal
KIUNGO mkabaji wa zamani wa klabu ya Simba anayecheza soka la kulipwa nchini Kenya, David Naftal amesema soka la Tanzania limejaa fedha, lakini linazidiwa umahiri katika uendeshaji wa klabu na majirani zao wa Kenya.
Naftal alisema kutokana na soka la Tanzania kuwa fedha nje nje, imewafanya wachezaji wengi wa kigeni kupigana vikumbo kuja nchini hata wale ambao viwango vyao siyo vya kuridhisha kwa vile hupapatikiwa na wenyeji wao.
Akizungumza na MICHARAZO toka Kenya, kiungo huyo aliyewahi kuichezea pia AFC Arusha, alisema klabu za Kenya zipo makini katika uendeshaji wa shughuli zake na mipango mkakati ya kukuza soka la Kenya tofauti na Tanzania ambazo 'siasa' zimezidi kiasi cha kufanya soa lake lidumae kwa miaka mingi.
Naftal alisema viongozi wa klabu za Kenya ni weredi na makini katika kuendesha shughuli zao na wanathamini sana wachezaji na ni nadra kusikia wakiwatuhumu wachezaji kufanya hujuma kama ilivyo Tanzania.
"Huku viongozi wapo makini na kazi zao na wanathamini wachezaji, huwezi kusikia kiongozi akimtuhumu mchezaji kufanya hujuma timu zinapopata matokeo kwa kutambua soka ndivyo lilivyo, tofauti na huko Tanzania," alisema.
Hata hivyo alisema soka la Kenya halina fedha nyingi kama Tanzania ambapo imekuwa mvuto wa wanasoka wa nchi mbalimbali kukimbilia.
"Kwa kweli kuna tofauti kubwa ya mfumo wa soka wa Kenya na Tanzania, wenzetu hapa wapo makini katika kupanga mikakati ya kuinua timu zao na soka lao kwa ujumla tofauti na Tanzania, japo hawana fedha nyingi kamka ilivyo huko nyumbani Tanzania," alisema.
"Kutokana na fedha kuwa za kumwaga Tanzania na wadau wake kuwa wepesi kumwaga mamilioni, imefanya wachezaji wengi wa nje kupenda kuja kucheza Tanzania hata kama hawana viwango vikubwa kama wazawa," aliongeza.
Naftal aliongeza kutokana na tofauti aliyoiona Kenya tangu alipotua nchini humo kuichezea Bandari ya Mombasa inayoshiriki Ligi Kuu, imemfanya kukosa hamu ya kutaka kurudi Tanzania badala yake azidi kusonga mbele