STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, February 28, 2011

Nyawela atuma salamu kwa wapinzani wa Extra



DANSA maarufu nchini ambaye kwa sasa ni kiongozi wa safau ya unenguaji wa bendi ya Extra Bongo, Hassan Mohammed 'Super Nyamwela', amewataka wapinzani wake kukaa chonjo na ujio wake mpya akiwa na bendi hiyo.
Nyamwela, aliyetokea African Stars 'Twanga Pepeta' amesema muda wa mwezi mmoja waliokuwa kambini amefanya mambo makubwa ambayo anaamini yatawasambaratisha wapinzani wao mara watakapotoka mafichoni.
Akizungumza mara baada ya bendi hiyo kutambulisha 'shoo' pamoja na moja ya vibao vyao vipya kwa waandishi wa habari jana, kwenye kambi yao iliyopo Mbezi-Louis jijini Dar es Salaam, Nyamwela alisema wapo kamili kwa vita.
Nyamwela alisema muda mmoja wa mwezi waliokaa kambini wameweza kuandaa shoo mpya ambazo hazijawahi kuonwa kokote.
"Kama ulivyoo, hiyo ni sehemu tu ya kazi ambazo tumekuwa tukizifanya tangu tuingie kambini na ambazo zitaanza kuonekana hadharani Ijumaa tutakapotoka mafichoni na kufanya shoo za mwishoni mwa wiki," alisema.
Alisema kikosi chao kinachoundwa na wanenguaji tisa akiwemo yeye Super Nyamwela, Super Danger, Master B na King Lion ambao ni wanaume, huku wa kike ni Angela Alloyce, Otilia Boniface, Husna Ramadhani, Lavia Edward na Jamila Nassor.
Naye rapa mpya wa bendi hiyo, Saulo John 'Ferguson' amewataka mashabiki wa muziki wa dansi kusubiri kupata vitu vipya toka kwake kuliko vile walivyokuwa wamezoea kuvipata alipokuwa Twanga Pepeta.
"Nina rapu kibao, lakini sitaki kumaliza uhondo, Ijumaa tunaanza kutoka kwa kufanya onyesho pale New Msasani Club, watu waje wamuone Ferguson mpya," alisema rapa huyo mmoja wa waimbaji wapya wa Extra Bongo.

Mwisho

EXTRA BONGO KUTOKA MAFICHONI




BENDI ya Extra Bongo iliyokuwa kambini kwa muda wa mwezi mmoja, inatarajiwa kutoka mafichoni Ijumaa wiki hii tayari kufanya maonyesho matatu ya kuzitambulisha nyimbo zao mpya pamoja na kuwaanika hadharani wanamuziki walya iliyowanyakua wakiingia kambini.
Hata hivyo kambi hiyo iliyokuwa eneo la Time Square Resort, Mbezi Louis, jijini Dar es Salaam, itavunjwa rasmi Jumatatu kabla ya kupata boti kwenda visiwani Zanzibar kutumbuiza.
Akizungumza kwenye utambulisho wa nyimbo na staili yao ya uchezaji kwa waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa bendi hiyo, Ally Choki 'Kamarade' aliiambia Micharazo kuwa, bendi yao iliyokuwa kambini kwa muda wa mwezi mmoja itatoka mafichoni Ijumaa kwa ajili ya kufanya maonyesho matatu mwishoni mwa wiki kabla ya kwenda Zanzibar Machi 12.
Choki, alisema siku watakayotoka mafichoni, Extra Bongo itafanya onyesho kwenye ukumbi wa New Msasani Club, na siku itakayofuata itakuwa TCC Changombe na kumalizia burudani zao za utambulisho wa nyimbo, wanamuziki na unenguaji wao mpya pale Mango Garden, Kinondoni.
"Tunatarajia kutoka hadharani Ijumaa, ambapo tutafanya maonyesho matatu siku ya Ijumaa, Jumamosi na Jumapili kwa kutambulisha nyimbo mpya na unenguaji tuliokuwa tunapika tukiwa kambini, ila kambi tutaivunja rasmi Jumatatu," alisema Choki.
Choki alisema baadhi ya nyimbo zilizokuwa zikipikwa wakiwa kambini ambazo zitatambulishwa rasmi kwa mashabiki ni Mtenda Akitendwa, Neema, Fisadi wa Mapenzi na nyinginezo.
"Hizo ni baadhi ya nyimbo tulizokuwa tukiziandaa, na tutazitoa sambamba na kuwatambulisha wanamuziki wetu wapya na aina ya uenguaji chini ya uongozi wa Super Nyamwela," alisema.
Choki alisema kuwepo kwao kambini kumeijenga vema bendi yao na watatoka hadharani kwa nia ya kuleta changamoto na mabadiliko katika muziki wa Tanzania.
"Tumekuja kuleta mabadiliko na wapenzi watarajie mambo makubwa toka kwetu kwani kikosi cha wanamuziki 23 tuliopo ni jeshi la maangamizi, kizuri ni kwamba tunatambulisha nyimbo mpya na video ya Mtenda Akitendwa,ambayo tumepiga tukiwa kambini," alisema Choki.
Naye mmoja wa marapa wa bendi hiyo, Ramadhani Mhoza 'Pentagone' alisema kambi imewaivisha na kwamba mashabiki wa muziki watarajie mambo makubwa toka kwao.
"Aisee asikuambie mtu tumeiva vya kutosha tukiwa tayari kwa kazi, ebu piga picha hapa Pentagon, kule Ferguson, Shikito, Bob Kissa, Hegga, Choki, Nyamwela na wengine unadhani atapona mtu kweli hapa?" alisema Pentagoni.
Kiongozi wa wanenguaji, Super Nyamwela, alisema kile walichokuwa wakikipika kimeshaiva na wapenzi wa muziki wajiandae kupata burudani kabambe toka kwao wakiwa ni tofauti na Super Nyamwela aliyekuwa Twanga Pepeta.
Kikosi kamili cha Extra Bongo kilichokuwa kambini na kinacghotarajiwa kuanza kuwasha moto jijini kabla ya kwenda Zenji, kisha wakati wa Pasaka kukimbiza Kanda ya Ziwa ni pamoja na Ally Choki 'Kamarade', Ramadhani Mhoza 'Pentagone', Saulo John 'Ferguson', Rogart Hegga 'Catapillar', Bob KIssa' na Athanas Montanabe 'Shikito' ambao ni waimbaji.
Wapiga gitaa ni Ephraem Joshua 'Kanyaga Twende' na Mfaume Zablon 'Baba Watoto' (solo), Sara Kindeki (Rhythms) na Hoseah Mgohachi (Bass), huku wapiga Kinanda wakiwa ni Pablo Mwendambali na Sebastian Lundandikija.
Anayekung'ita ngoma mbili maarufu kama Tumba au Conga ni Salum Issa 'Cha Kuku', wakati mkaanga chips (Drums) ni Victor Machine, wakati wanenguaji mbali na Super Nyamwela, pia kuna Danger Boy, Master B, King Lion, Otilia Boniface, Husna ramadhani, Angela Alloyce, Lavia Edward na Jamila Nassor 'Queen Jamila'.