STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, June 6, 2012

Mwenyekiti Villa Squad ajiuzulu, kisa...!

MAKAMU Mwenyekiti wa klabu ya Villa Sqaud aliyekuwa pia akikaimu nafasi ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ramadhani Uledi ametangaza kujiuzulu kuiongoza klabu hiyo kwa kile alichodai kutaka kulinda heshima yake. Habari za kuaminika toka katika klabu hiyo iliyoshuka daraja toka Ligi Kuu na yenye maskani yake eneo la Magomeni Mapipa, jijini Dar na kuthibitishwa na Uledi mwenyewe zinasema mwenyekiti huyo ameamua kubwaga manyanga tangu jana. Sababu zilizomfanya Uledi ajiondoe uongozini ni kutokana na kusakamwa na wanachama na kutengwa na viongozi wenzake baada ya kushindwa kushindwa kuinusuru Villa Squad isishuke daraja. Chanzo cha habari cha awali kilisema kutokana na shinikizo kubwa la wanachama hao, Uledi aliamua kubwaga manyanga akiandika barua ya kujitoa madarakani. Hata hivyo MICHARAZO lilipowasiliana na Uledi kutaka kuthibitisha taarifa hizo, alikiri juu ya kujiuzulu kwake, akidai amefanya hivyo ili kulinda heshima yake kutokana na kuona hali si shwari ndani ya klabu yao. Uledi, alisema tangu alipochaguliwa hakuwahi kupata ushirikiano wa kutosha kwa viongozi na wanachama, ila aliichukulia hali hiyo kama changamoto wake, lakini kwa hali inavyozidi kwenda mrama klabu kwao ameona bora ajiengue ili Villa itulie. "Ni kweli nimejiuzulu kutokana na hali ya mambo iliyopo klabuni, pia nahofia kuvunjiwa heshima, hivyo nimewaachia wanachama klabu yao, ingawa bado nitaendelea kuwa ndani ya timu hiyo kwa hali na mali kama mwanachama hai," alisema. Uledi, aliongeza anadhani chokochoko zote zilizopo Villa Squad kwa sasa zimetokana na timu hiyo kushindwa kubaki ligi kuu, japo alidai yapo mambo mengi yaliyochangia timu hiyo kutohimili ushindani hasa kutokana na hali mbaya ya kifedha iliyokuwa nayo. Mwenyekiti huyo na wenzake walichaguliwa kwenye uchaguzi mkuu uliokuwa umejaa mizengwe Juni 25 mwaka jana, huku nafasi ya Mwenyekiti na wajumbe watatu zikiwa wazi baada ya Kamati ya Uchaguzi wa TFF, kuwaengua waliokuwa wagombea wake kwa kukosa sifa za kuwania nafasi hizo ikiwemo suala la elimu zao.

Muziki wa Dansi walilia nafasi redioni, runingani

BAADHI ya wamiliki wa bendi za muziki wa dansi wameomba nyimbo za muziki huo zipewe nafasi ya kutosha katika vipindi vya televisheni na redio ili zisikike kama ilivyo sasa kwa taarab na bongofleva. Walitoa ombi hilo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wao na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari huku wakibainisha kuwa nyimbo za muziki huo kwa sasa hazina nafasi kubwa kama zamani. Mratibu kamati ya muda wa wamiliki wa bendi, Khaleed Chuma 'Chokoraa' alisema kuwa wamefikia kutoa ombi hilo baada ya kuona hali inavyokwenda sivyo ndivyo na hivyo kuwa na hofu muziki huo ukapotea kama hautapewa nafasi ya kutosha kwenye vyombo hivyo vya habari. "Tunachofanya sasa ni kujaribu kuwaunganisha wamiliki wote wa bendi za muziki wa dansi wa ndani na nje ya Dar es Salaam kwa lengo ya kufanya mkutano wa pamoja ili kuzungumzia hali hii," alisema Chokoraa. Alisema kuwa tayari baadhi ya wamiliki hao wameshakubaliana katika hilo na kwamba huenda mkutano huo ukafanyika wiki chache zijazo kama watakuwa wamewasiliana kikamilifu na wamiliki wote. "Lengo letu ni kuwaomba wahusika angalau kuangalia uwezekano wa kuufanya muziki wa dansi uwe na nafasi ya kutosha kwenye redio na televisheni ili kuwaibua wanamuziki wachanga nao wajulikane, p[ia muziki wa dansi uwe na vipindi maalum kama ilivyo kwa Bongofleva na Taarab ambao karibu kila redio na televisheni una vipindi," alisema. Naye Msemaji wa kamati hiyo ya muda, Ally Choki, alisema muziki wa dansi ni muziki wa zama na zama, na umekuwa ukisaidia vijana wengine kupata ajira, kwa wamiliki kama wao kuwaajiri, lakini kama hawapewi nafasi ya kutangazika ni vigumu wamiliki kuendelea kutoa ajira hizo. Choki, alisema kama walivyoweza kupewa nafasi na kutangazika wao wakati wakiibuka ndivyo vijana walioingia katika muziki huo nao wanapaswa kutangazwa kama ilivyo kwa wenzao wa miondoko mingine. "Siombi hili labda kwa kutaka nitangazwe, ila kuna vijana ambao wapo kwenye muziki huo hawapati nafasi na hivyo kuwatia unyonge na kusababisha dansi kufa tukiondoka kizazi chetu," alisema. Aliongeza kuwa, kama bendi wamekuwa wakilipa matangazo katika redio na televisheni kwa gharama, lakini fadhila ya matangazo hayo hawayaoni kwa muziki wao kutopewa nafssi katika vituo hivyo. Pia alidai kwamba muziki wa dansi ni mrefu kwa wimbo mmoja sio ukweli kwani wimbo mmoja wa dansi hauzidi dakika 8, lakini taarab wimbo mmoja huchukua hadi robo saa, lakini wanapewa nafasi, kadhaalika nyimbo za kikongo huwa na muda zaidi lakini nazo pia zinapigwa na vituo hivyo, jambo analohisi kinachofanyika ni kama hujuma kwa dansi. Aidha, alisema kwa uchunguzi wao wamebaini watangazaji wengi wa redio na televisheni wamekuwa na mzuka na miondoko mingine zaidi ya dansi kwa vile baadhi yao ni mameneja wa wasanii wa bongofleva na wengine hutumia vikundi vya taarab kuandaa maonyesho kama waratibu hivyo hutoa upendeleo kwa ajili ya masilahi yao binafsi. Choki alisisitiza kilio chaao sio kama kuvilaumu vituo hivyo, ila wanaombwa nao wapewe nafasi kama miondoko mingine kwa sababu muziki wa dani una historia kubwa ya nchi hii pi ni ajira za watu hivyo kama bendi zinazopiga muziki huo zitasahaulika, basi hata ajira za wanamuziki zitakuwa shakani pia. Mratibu huyo alikiri kwamba muziki wa dansi unachezwa na vituo hivyo vya runinga na redio lakini akadai kuwa si kama ilivyo kwa taarab na bongofleva ambao umekuwa ukipewa nafasi kubwa.

Uchaguzi Mkuu Yanga kumekucha, wanawake waitwa Jangwani

WAKATI zoezi la uchukuaji na urudishaji fomu kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa klabu ya Yanga ukitarajiwa kufungwa rasmi leo saa 10:00 jioni, wanachama vibopa wa klabu hiyo wamejitokeza kuwania uongozi na kuonyesha namna gani Jangwani walivyopania kufanya mabadiliko ya kuondokana na viongozi 'ombaomba'. Miongoni mwa waliojitokeza kwa jana kuchukua fomu za kuwania madarakani katika uchaguzi huo utakaofanyika Julai 15 ni pamoja na Yono Kevella wa Yono Auction Mart, Muzzammil Katunzi na Mussa Katabalo wanaowania nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo. Wanachama wengine waliochukua fomu jana kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Eliakim Mmaswi, Lameck Nyambaya, Ahmed Gao na wachezaji nyota wa zamani wa klabu hiyo ambao ni Edgar Fongo, Ramadhani Kampira, Ally Mayai na Aaron Nyanda. Uchaguzi mdogo wa Yanga unatarajiwa kufanyika Julai 15, hatua inayotokana na idadi kubwa ya viongozi waliokuwa madarakani hapo awali kutangaza kujizulu hivi karibuni, akiwemo Lloyd Nchunga aliyekuwa akishikilia nafasi ya uenyekiti. Tofauti na wagombea wengine, Katunzi na Katabalo wao walichukuliwa fomu na wazee wa klabu hiyo ambao wako chini ya mwenyekiti wao Jabir Katundu na katibu, Ibrahim Akilimali. Akimkabidhi fomu Katunzi, Akilimali alisema kuwa lengo la kumtaka mwanachama huyo wa Yanga kugombea ni kuimarisha safu yao ya uongozi ambayo itakuja na jukumu moja tu la kuiendeleza Yanga na kuokoa jahazi lao ambalo anaamini kwamba lilikuwa likizama. Akilimali alisema kuwa Yanga inahitaji wanachama wenye uwezo wa kuisaidia timu wakati wowote ili ifanye vizuri na kurejesha furaha kwa wanachama wao. "Hatuhitaji waomba dagaa, tunataka kiongozi mwenye uwezo ambapo inapohitajika Sh. 300,000, yeye atatoa Sh. 600,000," alisema Akilimali. Hadi kufikia jana, waliochukua fomu kuwania kutwaa mikoba ya Nchunga ni pamoja na John Lambele, huku Ayuob Nyenzi ambaye katika uchaguzi uliopita alijitoa kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, akichukua fomu ya kuomba kuchaguliwa kwenye cheo hicho. Wengine waliochukua fomu wakiwania nafasi za ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga ni Jumanne Mwamwenya, Peter Haule, Gaudecius Ishengoma, Abdallah Sheria, Saleh Abdallah, Abdallah Binkleb na Muhingo Rweyemamu. Isack Chanzi amejitokeza kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti ambayo Davis Mosha alijiuzulu mapema mwaka jana baada ya kudai kwamba ameshindwa kutimiza malengo yake kwa kukosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wenzake. Uchaguzi huo unasimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo iliyoko chini ya Jaji Mstaafu John Mkwawa. Hata hivyo mpaka sasa hakuna mwanachama yeyote wa kike wa klabu hiyo aliyejitokeza kuwania uongozi, hali iliyofanya kamati hiyo kutoa wito kwa wanachama hao kujitokeza kwani milango i wazi kwa wote.

John Kitime ajitosa kwenye utunzi wa vitabu, aja na 'vunja mbavu'

MWANAMUZIKI mkongwe wa muziki wa dansi nchini, John Kitime, amejitosa kwenye utunzi wa vitabu, ambapo kwa sasa yuko hatua za mwisho kukamilisha kitabu chake cha kwanza cha 'vunja mbavu' kiitwacho 'Kucheka ni Muhimu'. Akizungumza na MICHARAZO jana, Kitime ambaye ni mwanamuziki wa bendi ya Kilimanjaro 'Wana Njenje na pia ni mmoja wa wanakamati ya kutetea muziki wa dansi nchini, alisema amepata wazo la kuandika kitabu hicho kutokana na kipaji cha uchekeshaji alichonacho. Kitime ambaye wakati mwingine huwa jaji wa shindano la kusaka vipaji vya kuimba la Bongo Star Search, alisema kitabu hicho kwa sasa kipo katika hatua ya uhariri kabla ya kuanza mipango ya kukichapisha na kukisambaza ili kuwapa burudani wapenzi wa vunja mbavu. "Nipo katika hatua ya mwisho ya kumalizia kitabu changu cha kwanza kiitwacho 'Kucheka ni Muhimu', nadhani muda si mrefu mhakato wake wa kukitoa utafanyika na kuwapa burudani Watanzania," alisema. Aliongeza mbali na kitabu hicho pia ameshaandika vitabu vingine viwili kimoja kiitwacho 'Kilimanjaro Band' ambacho kitakuwa maalum kwa ajili ya kuzungumzia historia ya bendi hiyo ilitoka, ilipo na inapoenda pamoja na wasifu wa wanamuziki wake. "Kitabu kingine cha tatu ni cha 'Haki Miliki'. Nimeamua kuandika hiki kwa nia ya kuwazindua wasanii kufahamu haki zao katika miliki ya kazi zao," alisema mkongwe huo. Kitime anakuwa mwanamuziki wa pili mkongwe kujitosa kwenye fani ya uandishi vitabu, baada ya Tshimanga Kalala Assosa, aliyetunga kitabu cha 'Jifunze Lingala' ambacho kinaendelea kutamba sokoni kwa sasa huku akiandaa kingine cha wasifu wake.

Nassib, Majia kuwania ubingwa wa TPBO

MABONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Nassib Ramadhani na Fadhili Majia wanatarajiwa kupanda ulingoni Juni 9 kuwania taji la taifa la Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO). Pambano hilo la uzani wa Super Fly (kilo 52) litafanyika kwenye ukumbi wa Friend's Corner, Manzese na litasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi. Rais wa TPBO, Yasin Abdallah 'Ustaadh', aliiambia MICHARAZO jana kuwa pambano hilo limeandaliwa na promota Kaike Siraju na kwamba maandalizi yanaendelea vema. Ustaadh alisema tayari mabondia wote wanaendelea kujifua tayari kwa pambano hilo litakalokuwa la raundi 10 ambapo siku moja ya kupanda ulingoni watapimwa afya na uzito wao. "Mabondia wetu mahiri kabisa nchini, Nassib Ramadhani na Fadhili Majia wanatarajiwa kupigana kuwania ubingwa wa TPBO uzani wa Super Fly, litakalofanyika siku ya Jumamosi kwenye ukumbi wa Friend's Corner," alisema. Katika kuzuia vitendo vyovyote vya kihuni, Ustaadh alisema TPBO imejipanga kuhakikisha ulinzi madhubuti katika pambano hilo kwa kuanza kuwasiliana na mkuu wa polisi kituo cha urafiki ili kuwasaidia siku hiyo. "Tayari tumeshamuandikia barua mkuu wa kituo cha Polisi cha Urafiki, Afande Paparika, ili kutupa ulinzi wa kutosha siku ya pambano," alisema. Ustaadh alisema imani yake pambano hilo litawasisimua wengi kutokana na upinzani mkali uliopo baina ya mabondia hao na wale watakapambana katika michezo ya utangulizi siku hiyo na kuwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi.

Bibi Cheka, Dogo Aslay kutambulishwa Kanda ya Ziwa

WASANII wanaokuja juu katika muziki wa kizazi kipya nchini, Asilahi Is'haka 'Dogo Aslay' na Cheka Hija a.k.a 'Bibi Cheka' wanatarajiwa kwenda kutambulishwa rasmi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa wakisindikizwa na wasanii kibao nyota. Meneja wa wasanii hao, Said Hassani 'Mkubwa Fella' aliiambia MICHARAZO kwamba wasanii hao wataenda kutambuliwa katika mikoa ya Mwanza na Mara katika maonyesho yatakayofanyika mwishoni mwa wiki hii. Fella alisema wasanii watakaoenda kuwasindikiza Bibi Cheka anayetamba na wimbo wake wa 'Ni Wewe' alioimba na Mheshimiwa Temba, na Dogo Aslay aliyeachia ngoma mpya ya 'Umbea', ni pamoja na Ferooz, Easy Man, kundi la TMK Wanaume Family na wengine. "Mkubwa tunatarajia kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya maonyesho maalum ya kuwatambulisha Dogo Aslay na Bibi Cheka, shoo hizo zitakuwa tatu mfululizo zikianza Juni 8 mpaka 10 na watasindikizwa na 'vichwa' kibao," alisema Fella. Aliongeza kuwa maonyesho yao mawili ya awali yatafanyika jijini Mwanza kabla ya kumalizia burudani yao mkoani Mara na iwapo watapata fursa zaidi wanaweza kuhamishia utambulisho huo mkoani Shinyanga kabla ya kurejea Dar es Salaam. Alisema mbali na 'Ni Wewe', Bibi Cheka msanii wa muziki wa kizazi kipya mwenye umri mkubwa kuliko wote nchini, atatambulisha wimbo wake mwingine mpya aliouimba kwa kushirikiana tena na Mheshimiwa Temba uitwao 'Mario'.

Warembo Miss Bagamoyo kusaka vipaji J'pili Dar

WAREMBO tisa wanaojiandaa na shindano la urembo la 'Redd's Miss Bagamoyo 2012' wanatarajiwa kuonyeshana kazi katika mchuano wa kusaka kipaji 'Miss Talent' Jumapili ijayo. Mratibu wa shindano hilo, Awetu Salim, alisema shindano hilo la vipaji litafanyika kwenye ukumbi wa Club Masai, Kinondoni kabla ya warembo hao kuelekea mjini Bagamoyo kuwania taji la urembo la mji huo litakalofanyika Juni 15. Alisema warembo hao wanaoendelea na mazoezi kwenye ukumbi wa Club Masai chini ya mkufunzi wao, Sadah Salim wameanza kutambiana kila mmoja akidai ana kipaji kitakachompa ushindi kabla ya kwenda kutwaa taji la urembo. "Warembo wetu wanaendelea vizuri na mazoezi yetu na Jumapili wanatarajia kuchuana kwenye shindano la vipaji, litakalofanyikia kwenye ukumbi wa Club Masai na siku chache baadae wataelekea Bagamoyo kuwania taji la urembo litakalofanyika Juni 15 kwenye ukumbi wa TaSUBA," alisema. Awetu aliwataja warembo hao kuwa ni Zuhura Abdallah, Veronica James, Rose Lucas, Beatrice Bahaya, Diana Exavery, Nancy, Flora, Yvonne Steven na Celline Wangusu. Aidha, Awetu alishukuru kuongezeka kwa wadhamini zaidi katika shindano lao ambapo aliitaja kiwanda cha mvinyo cha Dodoma Wines kuwa ni miongoni mwa wadhamini wapya waliojitosa kuwapiga tafu. Mratibu huyo aliongeza kuwa upande wa burudani katika shindano lao watapambwa na bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' na mshehereshaji wa shughuli hiyo anatarajiwa kuwa Khadija Shaibu 'Dida wa G'.

Aurora afariki, azikwa Dar atakumbukwa kwa mengi

MDAU wa michezo na burudani hapa nchini, Ally Suleiman 'Aurora' amefariki usiku wa kuamkia juzi na kuzikwa jana kwenye makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana ilieleza kwamba Aurora alifikwa na mauti baada ya kuugua kwa muda mrefu na kulazwa kwenye hospital ya Muhimbili. Enzi za uhai wake Aurora aliweza kufadhili mashindano ya urembo, sambamba na michezo mbalimbali ikiwamo ngumi. Miongoni mwa mabondia waliofanikiwa kwa msaada wa Aurora ni bingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Awadh Tamim ambaye alisaidiwa na Aurora kutimiza ndoto hizo. Mbali na Tamim, Aurora aliweza kuisadia timu ya waandishi wa Habari za Michezo nchini 'Taswa FC' katika kufanikisha kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ikiwamo yale ya Media Bonanza yanayofanyika kila mwaka mkoani Arusha. Pia alikuwa akitajwa kama mmoja wa wafadhili wakubwa wa Coastal Union, hivyo kifo chake ni pigo kwa wadau wengi wa michezo na burudani. Mungu Ailaze Roho ya Marehemu Mahali Pema PEPONI Amiin