|
Michael Wambura |
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Soka
Tanzania (FAT sasa TFF), Michael Wambura na kiongozi wa zamani wa klabu
iliyokuwa Ligi Kuu ya Moro United ‘Chelsea ya Bongo’, Muhsin Balhabou ni
miongoni mwa wadau wa soka walichukua fomu jana kuwania nafasi mbalimbali za
uongozi ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Wambura amechukua fomu kuwania umakamu wa
rais huku Balhabou akiwania nafasi ya ujumbe katika kamati ya uchaguzi ya TFF.
Uchaguzi huo utafanyika Februari 24 jijini Dar es Salaam
Tayari wagombea wengine wawili, Makamu wa
Pili wa Rais anayemaliza muda wake, Ramadhan Nassib na Mjumbe wa Kamati ya
Utendaji inayomaliza muda, Wallace Karia wameshachukua fomu za kuwania nafasi
anayoiwania Wambura.
Wanamichezo wengine waliochukua fomu jana
ni pamoja na Mbasha Matutu, Salum Chama, Titus Osoro na Zafarani Damoder ambao
wote wanawania pia nafasi za ujumbe wa kamati ya utendaji ya TFF.
Wagombea wengine waliojitokeza kuchukua
fomu za kuwania ujumbe ni Salum Chama anayewania kupitia Kanda ya Kagera na
Geita, Mugisha Galibona, Samuel Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano (Mara na
Mwanza), Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Charles Mugondo,
Elly Mbise na Twahili Njoki (Arusha na Manyara) huku Yusuph Kitumbo (Kigoma na
Tabora).
Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja na
Selemani Kameya (Katavi na Rukwa) na James Mhagama (Njombe na Ruvuma), Athuman
Kambi (Lindi na Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart Masima (Dodoma na Singida),
Farid Nahdi (Morogoro na Pwani), Khalid Mohamed (Kilimanjaro na Tanga) na
Muhsin Balhabou, Shaffih Dauda na Zafarani Damoder (Dar es Salaam).
Taarifa iliyotolewa jana na Afisa Habarin
wa TFF, Boniface Wambura, imeeleza kuwa jumla ya waliochukua fomu hadi sasa ni
watu 26, lakini idadi hiyo ni ya wale wanaochukua fomu hizo katika ofisi za
TFF. Fomu hizo huchukuliwa pia kupitia tovuti ya TFF (www.tff.or.tz) na mwisho wa kuchukua
na kuzirejesha ni keshokutwa Ijumaa, saa 10:00 jioni.
Mwaka 2004, Wambura pamoja na aliyekuwa
Mwenyekiti wa FAT, Muhiddin Ndolanga, waliangushwa na Tenga lakini mwaka 2008,
Wambura alijitosa tena katika nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais lakini jina
lake lilienguliwa kwa maelezo kwamba hakuwa na sifa ya uadilifu.
Hata hivyo, mwaka jana Wambura akiwa
anawania nafasi ya uenyekiti wa Chama cha Soka cha Mkoa wa Mara (FAM), jina
lake lilienguliwa na baada ya kukata rufaa lilirejeshwa lakini muda wa uchaguzi
ulikuwa umeshamalizika na hivyo alishindwa kuwania cheo hicho kama
alivyodhamiria.
Juzi, Tenga alitangaza wazi kwamba hatawania
tena cheo hicho na hivyo kuwapunguzia 'presha' wale waliokuwa wakihofia kutwaa
fomu za kuwania uenyekiti wa shirikisho hilo kwa sababu yake.
Katika hatua nyingine, Said Mohamed
amechukua fomu ya kuwania umakamu mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board).