BAADA ya kutwaa Kombe la Mapinduzi mwishoni mwa wiki visiwani
Zanzibar, Azam FC inatarajiwa kuondoka nchini Alhamisi kwenda Nairobi, Kenya kwa
ziara ya wiki moja ya michezo ya kirafiki, kujiandaa na mzunguko wa pili wa
Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho.
Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Idrisa ameiambia BIN
ZUBEIRY leo kwamba katika ziara hiyo watacheza mechi tatu za kujipima
nguvu dhidi ya timu za Sofapaka, AFC Leopards na Gor Mahia kabla ya kurejea
nchini Januari 23.
Nassor alisema ziara hiyo ni maalum kwa ajili ya kuiweka sawa
timu yao kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara na Kombe la
Shirikisho Afrika.
Nassor amesema anaamini timu za Kenya ni nzuri na zitawapa
changamoto nzuri kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na kuingia
kwenye Kombe la Shirikisho.
“Tumekuwa katika programu ndefu ya maandalizi tangu Desemba,
tukianzia Kongo (DRC) ambako tulicheza mashindano na kuchukua Kombe, tumetoka
tumeingia kwenye Kombe la Mapinduzi tumeshiriki na kuchukua Kombe, na sasa
tunakwenda Kenya,”alisema Nassor.
Katibu huyo alisema kikosi kizima cha Azam kitakwenda Kenya
kwenye ziara hiyo na baada ya hapo timu itarejea tayari kwa mzunguko wa pili wa
Ligi Kuu.
IMEHAMISHWA: BIN ZUBEIRY
No comments:
Post a Comment