Mkenya Pascal Ochieng |
WACHEZAJI Pascal Ochieng na Shija Mkina
wameiponza klabu ya Simba baada ya uongozi wa mabingwa hao wa soka Tanzania
Bara kutakiwa kufika mbele ya Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji
ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa maelezo kuhusiana na madai
mbalimbali ya wachezaji hayo.
Mkenya Ochieng aliwasilisha barua katika
ofisi za (TFF) Desemba 19 mwaka jana akiliomba shirikisho hilo kumsaidia kupata
haki zake zikiwamo fedha zake za usajili, Sh. milioni sita na mashahara wake wa
mwezi mmoja (Novemba 2012), ambao hata hivyo hakuwa tayari kutaja ni kiasi gani
kwa madai kuwa ni siri yake na Simba.
Ochieng, ambaye alilazimika kuununua
mkataba wake wa miezi sita na klabu ya AFC Leopards ya Kenya ili ajiunge na
Simba, alinukuliwa akisema kuwa anaidai Simba dola za Marekani 8,000 (Sh. milioni
12.6) na kwamba hajapatiwa barua ya kuvunjwa kwa mkataba wake na klabu hiyo,
hivyo anaamini kuwa bado yeye ni mwajiriwa wa ‘Wekundu wa Msimbazi’.
Kwa upande wake, Mkina ambaye hivi sasa
anaichezea kwa mkopo klabu ya ligi kuu Bara ya Kagera Sugar (akitokea Simba),
anadai Simba haijamlipa Sh. milioni sita zilizokuwa zimebaki baada ya kusaini
mkataba nao kwa makubaliano ya Sh. milioni 10 na kwamba walimlipa fedha ya
utangulizi Sh. milioni nne mwaka 2010.
Mkina pia anadai kuwa uongozi wa Simba
umekuwa ukimzungusha katika malipo ya fedha zilizobaki na kwamba anawadai pia
fedha za mshahara wake wa miezi mitatu (Septemba – Novemba, 2012).
Akizungumza jana jijini Dar es
Salaam jana, Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kuwa Kamati ya
Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ili ilikutana jijini Dar es Salaam
Jumamosi kupitia masuala mbalimbali yakiwamo madai ya wachezaji hao.
Wambura alisema kuwa baada ya kamati hiyo
kupitia madai ya Ochieng na Mkina, iliamua kuzikutanisha pande zote (Simba na
wachezaji wanaolalamika) ili iwahoji kwa pamoja Jumamosi ya Januari 19.
“Ni kweli tulipata barua za wachezaji
hao. Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ilikaa Jumamosi iliyopita
ikaamua kuwaita viongozi wa Simba na wachezaji wanaolalamika ili wahojiwe kwa
pamoja Jumamosi,” alisema Wambura.
Baada ya kumalizika kwa mzunguko wa
kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Novemba mwaka jana huku timu yao ikifanya
vibaya na kuangukia katika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, viongozi
wa Simba waliamua kusitisha mikataba ya baadhi ya wachezaji wao wakiwamo beki
Ochieng na mshambuliaji Daniel Akuffor wa Ghana.
No comments:
Post a Comment